Nenda kwa yaliyomo

Jan Knappert

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Jan Knappert (14 Januari 1927 – 30 Mei 2005) alikuwa mwanaisimu kutoka nchi ya Uholanzi mwenye umaarufu wa kimataifa, alikuwa mtaalamu hasa wa lugha za Kiswahili na Kiesperanto.

Alifundisha kwenye vyuo vikuu mbalimbali pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Nairobi, School of Oriental and African Studies katika Chuo Kikuu cha London, hadi kurudi Ulaya bara alipofundisha miaka mingi kwenye Chuo Kikuu cha Leuven.

Alikuwa pia na shahada za uzamili katika Kisanskrit, lugha za Kisemiti (pamoja na Kiebrania, Kiarabu na Uislamu), na lugha za Austronesia (pamoja na Kimalay, Kitagalog, Kihawaii na Kimalagasy)[1]

Katika miaka alipokaa Afrika ya Mashariki alikusanya miswada mingi ya Kiswahili iliyoandikwa kwa herufi za Kiarabu[2] akatumikia pia kama Katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki.[3].

Alikabidhi mkusanyo wa miswada ya Kiswahili kwa Chuo Kikuu cha London.[4] ambako sehemu imeshapatikana kwa umma kwa njia ya intaneti.

Aliandika mengi na vitabu vingi. Utafiti wake kuhusu Kiswahili ulikazia hasa utamaduni, ushairi na dini ya Waswahili.

Alikusanya orodha ya istilahi za Kiswahili za kutaja nyota, makundinyota na sayari na hivyo kuhifadhi elimu ya vizazi Waswahili waliokuwa mabaharia na kuvuka bahari katika jahazi zao, ambayo ni elimu inayopotea haraka kutokana na mabadiliko ya teknolojia na ubaharia.[5].

Akiunganisha elimu yake ya lugha mbalimbali alitunga Kamusi ya Esperanto-Kiswahili akatafsiri pia utenzi wa kitaifa ya Kifini (unaoitwa Kalevala) kwa Kiswahili.

Baadhi ya vitabu vyake

  • 1958: Het Epos Van Heraklios (Dutch edition and literal translation; dissertation at Leiden University)
  • 1969: "The Utenzi wa Katirifu or Ghazwa ya Sesebani", Afrika und Übersee, Band LII, 3-4, 81-104.
  • 1970: Myths and Legends of the Swahili. London: Heinemann.
  • 1977: Het Epos van Heraklios. Uit het Swahili vertaald in het oorspronkelijke metrum. Amsterdam: Meulenhoff (Utenzi wa Heraklio, tafsiri ya Kiholanzi kwa kuiga ubeti wa Kiswahili)
  • 1977: Myths and Legends of Indonesia. Singapore: Heinemann Educational Books (Asia) Ltd.
  • 1986: Kings, Gods and Spirits from African Mythology. London: Eurobook Ltd.
  • 1989: The A-Z of African Proverbs London: Karnak House.
  • 1990: African Mythology. London: The Aquarian Press.
  • 1991: Indian Mythology; an Encyclopedia of Myth and Legend. London: Harper Collins.
  • 1993: "The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations." In: Indian Ocean Review, The. Perth, Australia, v, 6 n. 3, September 1993, uk 5-7
  • 1995: Pacific Mythology; an Encyclopedia of Myth and Legend. London: Harper Collins.
  • 2001: The Book of African Fables. New York: Edwin Mellen Press.
  • 2003: The A-Z of African Love Songs. London: Karnak House.
  • 2005: Swahili Culture Book I and II. New York: Edwin Mellen Press.
  1. Author Jan Knappert, tovuti ya Mellenpress, iliangaliwa Mei 2017
  2. Hadi mnamo mwaka 1900 maandiko yote ya Waswahili yaliandikwa kwa kutumia mwandiko wa Kiarabu
  3. http://www.ampltd.co.uk/digital_guides/swahili_manuscripts_parts_1_and_2/Publishers-Note-Part-2.aspx
  4. Knappert Collection at SOAS Ilihifadhiwa 15 Oktoba 2008 kwenye Wayback Machine., tovuti ya SOAS, ilitazamiwa Mei 2017
  5. KNAPPERT, JAN. "The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations." In: Indian Ocean Review, The. Perth, Australia, v, 6 n. 3, September 1993, uk 5-7