Neptun

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kwa elementi ya kikemia nenda Neptuni (elementi), kwa mungu wa Kiroma nenda Neptunus

Neptun ilivyopigwa picha na darubini ya angani Hubble.
Ulinganifu wa Neptun na dunia. Rangi ya bluu ya sayari ya Neptune hutokana na uwepo wa methane katika tabaka lake la hewa.

Neptuni (ing. Neptune) ni sayari ya nane kutoka kwenye Jua na ya nne kwa ukubwa wa kipenyo katika mfumo wa Jua. Masi yake ni mara 17 ya ile ya Dunia. Pamoja na Mshtarii (Jupiter), Zohali (Saturn) na Uranus inahesabiwa kati ya sayari jitu za mfumo wetu.

Neptuni inazunguka Jua kwenye obiti yake katika kipindi cha miaka 164.8 kwa umbali wa kilomita bilioni 4.5 au vizio astronomia 30.

Ugunduzi na jina[hariri | hariri chanzo]

Neptuni haionekani kwa macho matupu. Inawezekana ya kwamba Galileo Galilei, aliyekuwa mtu wa kwanza kutumia darubini kuangalia nyota, aliiona alipotazama anga lakini hakuitambua kama sayari, ila kama nyota mojawapo. Neptuni ilitambuliwa katika karne ya 19 kutokana na makadirio ya kihisabati wakati wataalamu walitafuta maelezo ya mzingo wa sayari jirani ya Uranus na hapo kuwepo wa sayari ya nyongeza ulitabiriwa. Hivyo ilitazamwa kwenye darubini kwa mara ya kwanza tarehe 23 Septemba 1846 karibu na mahali ilipotabiriwa.

Wavumbuzi mbalimbali walivutana kwa muda kuhusu jina na hatimaye mapendekezo ya kutumia jina la Neptunus, mungu wa Kiroma wa bahari, yalikubaliwa.

Tabia za sayari[hariri | hariri chanzo]

Habari nyingi kuhusu Neptuni zimepatikana kutokana na safari ya kipimaanga Voyager 2 iliyopita karibu nayo mwaka 1989.

Nusukipenyo chake ni kilomita 24,765 hivyo mara nne ya Dunia.

Muundo wa Neptuni unafanana na Uranus. Kuna kiini cha mwamba na metali chenye masi inayolingana takribani sawa na Dunia. Kiini hiki kinazungukwa na tabaka nene lenye mchanganyiko wa maji, amonia na methani katika hali ya kiowevu, kwa hiyo sehemu hii inaitwa pia bahari.

Juu yake ziko tabaka za angahewa inayofanywa na gesi kama hidrojeni, heli na methani. Hakuna tofauti kali kati ya sehemu za „angahewa“ na „bahari“ maana hali za mata zinaingiliana kutokana na shinikizo kubwa.

Tabaka za juu za angahewa ni baridi sana zikiwa na jotoridi ya nyuzi za Kelvini °K 55 (°C-218) K. kitovu cha jotoridi kinapanda hadi kufikia takriban °K 5,400 (°C 5,100).

Katika angahewa ya Neptuni zilipimwa dhoruba kali zinazofikia kasi ya zaidi ya kilomita 1600 kwa saa.

Neptuni huwa na mfumo wa bangili uliotambuliwa na Voyager 2.

Miezi[hariri | hariri chanzo]

Mwezi mkubwa unaitwa Tritoni uligunduliwa mwaka 1846, siku chache baada ya sayari yenyewe na kupokea jina lake kutokana na mwana wa mungu wa bahari katika mitholojia ya Kigiriki. Tritoni ina kipenyo cha kilomita 2707. Katika karne ya 20 miezi mingine ilitambuliwa inayozunguka Neptuni, hadi sasa jumla ni 14 lakini mingi ni midogo.

Kuiangalia sayari[hariri | hariri chanzo]

Neptun huwa haionekani kwa urahisi: macho matupu hayawezi kuiona; ni lazima kutumia darubini, na hata hapo huonekana ikiwa imefifia kama kisahani chenye rangi ya buluu-kijani. Rangi hii imetokana na gesi ya methani inayopatikana kwa wingi katika angahewa yake. Kwa kutumia darubini kubwa, sayari huweza kuonekana kama kaduara kadogo chenye kipenyo cha kama sekunde za tao 2.3..

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Wallah, W.B. & Mwamburi, J. Kiswahili mufti darasa la 8: Mwongozo wa mwalimu. Longhorn, 2009. ISBN 99966491066
  2. TESSA - Teacher Education in Sub Saharan Africa. Nishati na Mwendo: Kutoka Ardhini kenda kwenye nyota – kutumia Zana Kifani. Available at: www.tessafrica.net
  3. 3. Waweru, M.; Makombo, H; Vonuoli, A.; Kashihiri, C.; Mwayani, J.Hutua za Kiswahili: Masomo ya Msingi 8. East African Educational Publishers ltd., 1ed, 290p., 2005. ISBN 9966-25-403-X
  4. Maran, Stephen P. (2005). Astronomy for dummies, Inc. Wiley Publishing, Hoboken.
  5. Klimishin, Iwan A. (1991). Modern Astronomy, Akad. Verl Spektrum, Heidelberg.
  6. Birney, Scott D. (1991). Observational astronomy, Cambridge University Press, Cambridge.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Astrowiki.PNG
Mradi wa Astronomia Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Neptun kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.