Utaridi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Ulinganishi wa ukubwa wa Utaridi na Dunia
Picha isiyo na rangi sahihi iliyopigwa na chombo cha angani Mariner 10 inaonyesha uso wa Utaridi ikifanana na mwezi

Utaridi (pia: Zebaki -taz. chini- au umbo la Kiing. Mercury) ni sayari iliyo karibu na jua letu katika mfumo wa jua na sayari zake.

Jina la sayari[hariri | hariri chanzo]

Jina lake limetokana na kiarabu عطارد (soma "`uTaarid") inayomaanisha "mwendo wa haraka"[1] kwa sababu kasi ya Utaridi inapita mwendo wa sayari nyingine kutokana na njia yake fupi ya kuzunguka jua ilhali ni sayari ya kwanza inayozunguka jua katika siku 88 pekee. Majina ya Wagiriki wa Kale Hermes na la Waroma "Mercurius" yalikuwa majina ya miungu yao ya kuwasilisha habari za miungu wengine walioaminiwa kuwa na kasi kubwa kwa kazi hii na chaguo hili lilitokana na tabia ileile ya sayari. Jina hili la Kiroma Mercuriius limeingia katika lugha nyingi za Ulaya. Umbo la kiarabu limekuwa jina la watu katika nchi nyingi zilizoathiriwa na utamaduni wa Kiislamu pia jina la sayari ya kwanza kwa mfano kwa Kituruki au Kimalaysia.

Katika vitabu kadhaa vya Kiswahili sayari inaitwa Zebaki lakini hii inaonekana ni kosa kutokana na jina la Kiingereza "Mercury" kwa sayari hii. Mercury ni pia jina la metali inayoitwa zebaki kwa Kiswahili kutokana Kiarabu "زئبق" (tamka "zibaq"). [2]

Mara chache neno "utaridi" limetumiwa kutaja sayari kibete ya "Pluto" lakini hii ni kwa kukosea pia.[3]

Tabia za Utaridi[hariri | hariri chanzo]

Utaridi ni sayari ndogo. Kipenyo chake kwa ikweta ni 4879.4 km. Kwa sababu iko karibu sana na jua ina mbio wa haraka. Mwaka wa Utaridi ambayo ni muda wa kuzunguka jua ni siku 88 za dunia pekee.

Inazunguka kwenye mhimili wake katika muda wa siku 58.6 za dunia. Kutokana na kuwa karibu na jua kuna joto kali upande unaotazama jua lakini upande wa usiku ni baridi kabisa kutokana na uhaba wa hewa inayoweza kutunza halijoto. Halijoto ya wastani ni +178.8 °C, (usiku -183.15 °C na mchana +426.85 °C).

Mwaka 2012 barafu ya maji ilitambuliwa kwenye data kutoka chombo cha angani MESSENGER iliyochunguza sayari hii. Barafu inapatikana karibu na ncha ya kaskazini isiyofikiwa na mishale ya jua.[4]

Uhaba wa hewa umesababisha uso wa sayari kujaa mashimo ya kasoko. Kasoko hizi zimesababishwa kwa kugongwa na meteoridi. Angahewa kama duniani ingeangamiza meteoridi ndogo na kusababisha kupasuka kwa kubwa lakini Utaridi zote zinafika usoni bila kizuizi. Alama za meteoridi ni mmomonyoko wa pekee unaoonekana hakuna dalili ya mmomonyoko kutokana na hewa au maji ya awali.

Kutokanana na kuwa karibu sana na jua Utaridi inaonekana kama nyota kwa macho katika masaa ya pambazuko na machweo pekee.

  1. ling. طرد tarada : drive way, chase away; مطارد mutarid: chaser, hunter ; cf "Dictionary of Modern written Arabic3" ya Hans Wehr
  2. kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1]
  3. Soma hapa kuhusu matatizo ya matumizi ya majina ya sayari katika kamusi za Kiswahili.
  4. Water Ice Discovered on Mercury (space.com tar. 3 Dis 2012)
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Utaridi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.