Njiamzingo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Obiti)
Njiamzingo ya gimba dogo (kama satelaiti) linalozunguka gimba kubwa (kama Dunia);
kani ya velositi "v" inataka kulipeleka mbele mbali na mahali pake; kani ya graviti "a" inalivuta kuelekea gimba kubwa; tokeo lake ni njiamzingo ya kuzunguka.
Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Njiamzingo (pia: obiti, kutoka neno la Kiingereza orbit lenye asili ya Kilatini orbita "njia, mzunguko") ni njia inayotumiwa na gimba la angani linalozunguka gimba kubwa zaidi katika anga ya ulimwengu ilhali inashikwa na mvuto wa graviti. Mfano wake ni mwendo wa sayari inayozunguka jua, au mwezi unaozunguka sayari yake, au satelaiti inayozunguka dunia.

Uwiano wa kani katika njiamzingo

Fizikia ya njiamzingo inatazama kani au nguvu mbili.

  • Ya kwanza ni velositi ya gimba dogo inayoelekea kwenda mbele mbali na mahali pake.
  • Ya pili ni graviti inayovuta gimba dogo kuelekea gimba kubwa. Njiamzingo ipo pale ambako nguvu hizi mbili zinalingana. Kama kasi ya velositi ikiwa kubwa zaidi gimba dogo lisingezunguka bali ingetoka. Kama kani ya graviti inakuwa kubwa zaidi gimba dogo litaanguka kwenye gimba.

Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Mwanafizikia Isaac Newton aliwaza mfano unaoeleza vizuri kani zinazoathiri njiamzingo. Aliwaza mfano wa mzinga uliowekwa juu ya mlima mrefu. Mzinga huu unaweza kurusha risasi kwa mwelekeo wa ulalo kwa kasi mbalimbali. Athari ya msuguano wa hewa kupunguza kasi dhidi ya risasi aliacha kando au kuwaza mlima mrefu kiasi cha kupenya juu ya angahewa ya dunia.

  • Kama mzinga unarusha risasi yake kwa velositi ndogo itaenda mbele kiasi halafu kuanguka chini (A).
  • Kama kasi au velositi inaongezwa itaanguka mbali zaidi(B).
  • Kasi ya risasi ikiongezeka zaidi kuna hali ambapo risasi haianguki tena inazunguka dunia na kumailisha njiamzingo ya duara (C).
  • Kama kasi inaongezeka tena njiamzingo inachukua umbo la duaradufu. Mahali pa periheli ambapo njiamzingo ipo jirani zaid na dunia ni mahali pa kufyatuliwa na 180° kinyume chake upande wa pili ni afeli ambapo njiamzingo iko mbali na Dunia. (D)
  • Kasi ya risasi ikiongezwa zaidi inafikia velositi ya kuweza kutoka katika graviti ya Dunia. (E).

Kwa hali halisi makadirio ya makombora ya kurusha satelaiti na vyombo vya angani vinafuata maelezo hapo juu. Kama kombora linatakiwa kubeba satelaiti kama vile satelaiti ya televisheni au ya mawasiliano ni lazima kukadiria velositi ya kombora kulingana na uzito wake na mahali panapotakiwa kufikia angani ili kuweza kupeleka satelaiti katika njiamzingo aina ya (C) au (D).

Chombo cha angani kinapotakiwa kupelekwa safari ya kwenda mwezi au sayari nyingine sharti kufikia "velositi ya kutoka" katika graviti ya Dunia.

Historia ya utafiti wa njiamzingo

Zamani watu walifikiri ya kwamba jua lina njiamzingo ya kuizunguka dunia kila siku jinsi inavyoonekana kwa macho: Jua linachomoza upande mmoja wa upeo wa anga wakati wa asubuhi na kuzama chini upande wa pili wakati wa jioni.

Kwa hiyo wataalamu Wagiriki wa Kale kama Klaudio Ptolemaio waliwaza njiamzingo za jua na sayari za kuzunguka dunia na njiamzingo hizi zilikuwa na umbo la duara kamili.

Kuanzia utafiti wa akina Koperniko na Galilei ilitambuliwa ya kwamba dunia ndiyo inayozunguka Jua pamoja na sayari nyingine, kila moja kwenye njiamzingo yake. Ilionekana pia ya kwamba njiamzingo hizo si duara kamili lakini zinalingana zaidi na duaradufu.

Kipindi cha njiamzingo

Kipindi cha njiamzingo ni muda unaotumiwa na gimba kama satelaiti, mwezi au sayari kuzunguka gimba mama.

Kwa mfano kipindi cha njiamzingo ya njiamzingo ya Dunia yetu kuzunguka Jua ni siku 365.25 na kipindi hiki tunaita "mwaka".

Kipindicha njiamzingo ya mwezi wetu ni siku 1; wakati huohuo unazunguka mara moja kwenye mhimili wake na hii ndiyo sababu sisi tunaona upande uleule wa mwezi wetu muda wote.

Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Njiamzingo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.