Unajimu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Mvindaji Orion: watu waliwaza ya kwamba nyota kadhaa zinazoonekana kwa pamoja angani ni picha ya mungu fulani au nguvu muhimu katika ulimwengu, hata kama nyota hizi hali halisi hazina uhusiano kati yao.

Unajimu (wakati mwingine pia: astrolojia) ni mafundisho juu ya uhusiano kati ya nyota na maisha hapa duniani. Wafuasi wa unajimu hufundisha ya kwamba nyota zinaathiri maisha ya watu na matukio duniani kama amani, vita au maafa.

Kuna aina nyingi za unajimu:

  • wengine wanataka kugundua mwendo wa dunia na utabiri wa mambo yajayo kutokana na nyota
  • wengine wanaamini ya kwamba tabia za mwanadamu zinatokana na hali ya nyota wakati wa kuzaliwa kwake
  • wengine wanaona nyota kama alama za miungu au nguvu za mbinguni.

Tofauti ya unajimu na astronomia[hariri | hariri chanzo]

Unajimu na astronomia zilianza pamoja kama kazi ileile zikaendelea hivyo kwa karne nyingi. Tangu mwanzo wa sayansi ya kisasa takriban miaka 500 iliyopita wataalamu walitambua tabia za nyota kuwa magimba ya angani yenye sifa za kifizikia sio pepo, roho au miungu zinazoweza kutawala dunia au wanadamu. Kwa hiyo njia za unajimu (astrolojia) na astronomia zimeachana tangu karne kadhaa. Lakini miaka 400 iliyopita wanasayansi muhimu kama Tycho Brahe, Johannes Kepler, Giordano Bruno au Galileo Galilei walitengeneza horoskopi, ingawa waliweka misingi ya astonomia ya kisasa.

Uchoraji wa Meksiko ya Kale unaonyesha zodiaki ya kundinyota za unajimu wa Waazteki

Asili ya unajimu[hariri | hariri chanzo]

Tangu mwanzo wa historia wanadamu katika sehemu mbalimbali za dunia walitazama nyota.

Nyota zinaonekana wakati wa usiku kwa kufuatana na mwendo wa dunia yetu kuzunguka jua. Kwa namna hiyo kuonekana kwa nyota kunalingana na majira ya mwaka. Kwa hiyo katika dunia kabla ya kupatikana kwa kalenda watazamaji wa nyota waliweza kutabiri mabadiliko ya hali ya hewa, kuja kwa majira ya mvua, baridi, joto na kadhalika. Kati ya nyota zilizotazamiwa hivyo ni kwa mfano Kilimia na Zuhura.

Kwa mfano kuonekana kwa nyota fulani (hii inategemea mahali duniani) inaweza kuwa alama ya kwamba mvua ni karibu, au majira ya baridi inaanza. Sababu yake ni ya kwamba nyota huonekana kwa vipindi fulani wa mwaka tu; wakati wa miezi mingine zingeonekana wakati wa mchana ambako nuru ya jua inaficha nyota zote hazionekani tena. Masaa za usiku kuna vipindi ambako nyota fulani zinaonekana vizuri angani juu kabisa na kwa njia hiyo zinaweza kutambuliwa kama ishara za majira.

Leo hii watalaamu wengi huamini ya kwamba hapo ndipo msingi muhimu wa imani ya kwamba nyota zinaathiri maisha duniani.

Watu wa kale walikuwa hodari sana kutazama nyota na kutambua mabadiliko yao katika mwendo wa wakati. Hali hii haieleweki kirahisi na watu wa leo waliozoea nuru ya taa za umeme wakitumia wakati wa usiku kutazama TV au kompyuta. Lakini kwa watu wa kale -jinsi ilivyo hadi leo kwa watu wengi vijijini au porini- nyota na mwezi zilikuwa taa hasa wakati wa usiku.

Uhusiano ulioonekana kati ya mabadiliko ya nyota na mabadiliko ya majira yalianzisha elimu ya kalenda pamoja na elimu ya unajimu na astronomia.

Kwa wazee hawa ilionekana kama nyota fulani inatawala majira, hali ya hewa na hivyo maisha ya kibinadamu kwa sababu maisha ya jamii yalitegemea majira na mwendo wa mvua, ukame, baridi au joto. Hapo ni asili ya kuziangalia nyota kama miungu au pepo zenye uwezo fulani. Hasa tabia ya hali ya hewa ya kuchelewa au kuwahi kidogo ilijenga imani ya kwamba kuchelewa kwa mvua ni dalili ya hasira ya mungu yule anayeonekana katika nyota fulani.

Alama kwa kundinyota 12 za Zodiaki katika mapokeo ya Ulaya; zinadaiwa kuwa muhimu na kutawala tabia za watu kwenye horoskopi.

Horoskopi[hariri | hariri chanzo]

Kati ya mbinu za unajimu zinazojulikana sana duniani ni horoskopi. Tangu zamani watu walitazama nyota zilizoonekana pamoja kama kundinyota kama nukta angani na kuwaza kuwa na mistari kati yao hivyo kuona picha ya watu, wanyama au miungu. Ni hasa kundinyota 12 za aina hii zilizorudia kila mwaka kukaa juu kwenye anga wakati wa mwezi fulani. Kundinyota hizi zilichukuliwa kama "watawala" wa kipindi ambako zilionekana juu angani wakati wa usiku na kwa pamoja zinafanya "zodiaki" yaani ufuatano wa kundinyota zilizoaminiwa kuwa muhimu. Unajimu unafundisha ya kwamba kila kundinyota kuw na tabia fulani na mtu aliyezaliwa "chini" ya nyota hizi kuwa tabia zilezile na kuwa. Hizi kundivyota za zodiaki ziliunganishwa na athira iliyoaminiwa kutokea kwa sayari ambazo zilipewa pia tabia zao. Hayo yote ni mfumo usioeleweka kirahisi na kuwa msingi wa horoskopi.

Hadi leo chini ya vichwa kama "Nyota zinasema" magazeti mengi huchapisha namna za utabiri wa kila wiki kwa watu kufuatana na tarehe zao za kuzaliwa.

Icon-religion.png Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Unajimu kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.