Amri Kumi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Amri za Mungu)
Amri 10 - taswira ya Lucas Cranach Mzee.

Amri Kumi ni orodha ya amri kuu za Mungu katika Biblia. Za kwanza zinamhusu Mwenyezi Mungu mwenyewe, na zile zinazofuata mpaka mwisho zinahusu jirani, yaani binadamu wengine kuanzia wazazi.

Toleo la awali linapatikana katika kitabu cha Kutoka 20:1-17. Toleo la pili liko katika Kumbukumbu la Torati 5:1-21.

Amri hizi ni sehemu ya Torati ya Kiyahudi na kukubaliwa pia na Wakristo walio wengi kama amri zinazowahusu wao pia, tena kimsingi zinawadai watu wote.

Hata hivyo wafuasi wa Yesu Kristo wanazishika kadiri ya utimilifu wake ulioletwa naye kama Agano Jipya. Mifano ya ukamilisho huo ni mafundisho ya Yesu katika Injili ya Mathayo 5:17-48.

Maneno ya Amri Kumi[hariri | hariri chanzo]

Maneno yanayojulikana kama “Amri Kumi” yanapatikana katika vitabu vya Biblia "Kutoka" na "Kumbukumbu la Torati".

Kitabu cha Kutoka 20:2–17 Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:6–21
2. Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

3. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi. BWANA Mungu wako, ni Mungu wenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6. nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
7. Usilitaje bure jina la BWANA hatamhesabiwa kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
8. Ikumbuke siku ya sabato uitakase. 9. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 10. lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya mlango yako. 11. Maana kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.



12. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.
13. Usiue.
14. Usizini.
15. Usiibe.
16. Usishuhudie jirani yako uongo.
17. Usiitamani nyumba ya jirani yako; wala mke wake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.

6. Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

7. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. 9. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 10. nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
11. Usilitaje bure Jina la Bwana, Mungu wako; maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure.
12. Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru. 13. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 14. lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. 15. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.
16. Waheshimu baba yako na mama yako; kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
17. Usiue.
18. Wala usizini.
19. Wala usiibe.
20. Wala usimshuhudie jirani yako uongo.
21. Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.

Amri Kumi kwa maandishi ya Kiebrania katika sinagogi la Amsterdam.

Mpangilio wa Amri Kumi[hariri | hariri chanzo]

Maneno katika Kutoka 20 huwa na amri mbalimbali. Namba kumi ni hesabu iliyotiwa baadaye katika orodha hii, haikuwa nia asili kuwa na amri “10” kamili. Ila tu wakati wa Biblia ilikuwa kawaida tayari kuziita "amri 10", lakini bila kuonyesha namba au mpangilio katika maneno ya Biblia yenyewe.

Hali hii ilisababisha tofauti ndogo katika hesabu ya amri hizi kati ya mapokeo ya madhehebu mbalimbali. Tofauti kuu ni kati ya Wayahudi wakifuatwa na Wakristo mbalimbali kwa upande mmoja na Wakatoliki pamoja na Walutheri na Wamoravian kwa upande mwingine kuhusu kutokuwa na sanamu za kuchonga. Tangu Agostino wa Hippo Wakatoliki walijumlisha sehemu kuhusu kutoabudu sanamu za kuchongwa pamoja na amri ya kutokuwa na miungu mingine. Kwa kufikia namba kumi Agostino aligawa sehemu ya mwisho kuwa amri mbili. Martin Luther alimfuata Agostino lakini Wareformed waliona mpangilio tofauti wakaihesabu kama amri ya pekee.

Mpangilio wa Amri Kumi katika dini/madhehebu mbalimbali
Amri Wayahudi Waanglikana, Wareformed na wengineo Waorthodoksi Wakatoliki, Walutheri, Wamoravian
Mimi ni Bwana Mungu wako 1 (utangulizi) 1 1
Usiwe na miungu mingine ila mimi 2 1
Usijifanyie sanamu ya kuchonga 2 2
Usilitaje bure jina la Bwana 3 3 3 2
Ikumbuke siku ya sabato uitakase 4 4 4 3
Waheshimu baba yako na mama yako 5 5 5 4
Usiue 6 6 6 5
Usizini 7 7 7 6
Usiibe 8 8 8 7
Usishuhudie jirani yako uongo 9 9 9 8
Usiitamani nyumba ya jirani yako
Usitamani mke wake
10 10 10 9
Usiitamani cho chote alicho nacho jirani yako 10

Amri Kumi katika Ukristo[hariri | hariri chanzo]

Vibao vyenye amri kumi za Mungu

Roho Mtakatifu anayetuweka huru anatuongoza kushika amri za Mungu alizopewa Musa, kwa sababu ni masharti ya upendo yaliyodaiwa na Yesu pia. “Ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili: Umpende jirani yako kama nafsi yako” (Gal 5:13-14). “Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu: tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito” (1Yoh 5:2-3).

Yesu alidai tushike amri za Mungu ili tuufikie uzima wa milele. “Tazama, mtu mmoja alimwendea akamwambia, ‘Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?’ Akamwambia, ‘Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri’. Akamwambia, ‘Zipi?’ Yesu akasema, ‘Ni hizi: Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na, mpende jirani yako kama nafsi yako” (Math 19:16-19).

Tusiposhika amri hizo hatuwezi kutukuzwa mbinguni kwa sababu tunaonyesha hatujali vya kutosha uhai, utakatifu wa ndoa, mali ya watu, ukweli, heshima kwa wakubwa wetu na upendo kwa wenzetu kwa jumla. Kupuuzia tunu hizo muhimu ni kumpuuzia Muumba aliyeziweka zituongoze maishani. “Ee Israeli, tu heri sisi, maana mambo yampendezayo Mungu yamejulishwa kwetu” (Bar 4:4). “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi” (1Kor 6:9-10). “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati, wala mchafu, wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu” (Ef 5:5).

Injili haitaji amri zinazohusu ibada kwa Mungu kwa sababu Yesu aliona haja ya kusisitiza zile zinazohusu jirani, na kwa sababu hakutaka hizo za kwanza zifuatwe na Kanisa lake kama Wayahudi wanavyofanya. “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha... Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu” (Yoh 2:19; 5:18). “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia” (Mk 2:28). “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16-17). “Basi, torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zilezile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao... Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana, maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu” (Eb 10:1; 13:16).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya Agano la Kale bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Amri Kumi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.