Agostino wa Hippo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Picha ya kale zaidi (karne ya 6) ya Agostino katika kanisa la Laterani, Roma (Italia).
Agostino wa Hippo akibatizwa na Ambrosi, mwaka 387.

Agostino wa Hippo (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5.

Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake bora, tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa kanisa.

Maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Agostino alizaliwa mwaka 354 mjini Thagaste katika mkoa wa Numidia. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Aurelius Augustinus. Wakati ule Ukristo ulikuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma; dhuluma dhidi ya Wakristo zilikuwa zimekwisha rasmi mwaka 313 kwa Hati ya Milano iliyotolewa na Konstantino Mkuu ili kuruhusu uhuru wa dini.

Mama yake (Monika, anayeheshimiwa kama mtakatifu) alikuwa Mkristo, kumbe baba (Patrisi) alifuata dini ya jadi ya kuabudu miungu mingi kabla hajabatizwa mwishoni mwa maisha yake.

Katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini wenyeji walikuwa Waberberi kama mama yake, lakini watu wa mjini, kama baba yake, na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Ulaya wakitumia hasa lugha ya Kilatini. Kwa jumla sehemu hii ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi.

Wakati wote wa ujana wake alifuata anasa na uzushi, bila kujali machozi ya mama yake.

Alipata elimu yake Thagaste, Madaura na hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis).

Baada ya kumaliza masomo yake, alifundisha Kilatini huko Thagaste (374), halafu namna ya kuhubiri huko Kartago (375-383), akaendelea nchini Italia, kwanza Roma (384), halafu Milano (384-386).

Wakati huo wote aliendelea kuishi bila ndoa na mwanamke aliyemzalia mtoto wa kiume.

Lakini tangu mwaka 373, aliposoma kitabu fulani cha Sisero, alikuwa anavutiwa na masuala ya kiroho, hata akajiunga kwa karibu miaka 10 na Umani, dini ambayo ilidai kufuata akili na kufafanua sababu ya mabaya kuwepo, ikikataa Agano la Kale ili kufuata Ukristo wa kiroho. Lakini alipokutana na askofu Mmani Fausto, alikosa imani nayo.

Kumbe akakutana na watu, hasa Ambrosi askofu wa Milano, waliomvuta awe Mkristo Mkatoliki.

Mahubiri ya Ambrosi yalimfanya asadiki mamlaka ya Biblia nzima inayosomwa rasmi na Kanisa. Katika barua za Mtume Paulo, Augustino alimtambua Kristo kama mwokozi, si mwalimu tu.

Kisha kuongoka mnamo Agosti 386, akiwa na umri wa miaka 32, aliacha kufundisha na hata kuishi na mama mtoto, akatawa Cassiciaco kwa muda, akarudi Milano alipobatizwa na Ambrosi pamoja na mwanae Adeodato na rafiki yake Alipio.

Baada ya kubatizwa na kunuia kuishi kitawa Thagaste, akarudi Afrika; njiani, huko Ostia, bandari ya Roma, alifiwa mamaye.

Mwaka 391 bila kutarajia alipewa daraja ya upadri huko Hippo, alipoanzisha monasteri, halafu akachaguliwa kuwa askofu msaidizi wa mji huo (395) na mwaka 397 akawa askofu wa jimbo hilo.

Alifanya adhimisho la ekaristi kuwa kiini cha maisha ya jumuia zake.

Mahubiri yake mengi yanaonyesha alivyojua kujadiliana na umati akitumia maneno rahisi na ya kawaida na hata ucheshi katika kulinganisha Neno la Mungu na mazingira yao.

Kwa tabia yake karimu na pendevu, hisia zake, uvumilivu na utayari wa kusamehe alifanya hata maadui kadhaa kuwa marafiki.

Maisha yake ya Kiroho yaliyoongoza uandishi wa kanuni yake kwa watawa yamefuatwa na mashirika mengi ya kiume na ya kike hadi leo.

Kwa miaka 40 mpaka kifo chake, mbali na kutimiza majukumu yake mengi, aliendelea kueleza na kutetea imani sahihi ya Kikristo kwa mahubiri, maandishi na vitabu vingi sana (hata za mitindo mipya) dhidi ya aina zote za uzushi za wakati ule: Wamani, Wadonati, Wapelaji na Waario.

Kwa njia hiyo amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo, hasa wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na katika Uprotestanti uliotokea katika Kanisa hilo. Kwa mfano Martin Luther alimtaja kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mtume Paulo).

Aliaga dunia akiwa Hippo mwaka 430 wakati washenzi wa Kijerumani walioitwa Wavandali walipokaribia kuteka mji wake.

Kaburi la Agostino katika basilika la San Pietro in Ciel d'Oro, Pavia (Italia).

Kazi na mafundisho yake[hariri | hariri chanzo]

Katika historia Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.

Kila wakati ulifurahia zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika kujichunguza na kusimulia siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.

Kazi yake kubwa si kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali na kutoa majibu yenye umuhimu mpaka leo.

Akilinganisha imani na akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu ([[Ukweli] mkuu na Upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wake). Huyo katika roho yake isiyokufa ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu, ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.

Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya mapokeo na kuathiri Kanisa lote la magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi).

Pia alifafanua upya imani kuhusu umwilisho, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451): hali mbili katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”.

Dhambi na neema[hariri | hariri chanzo]

Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyp, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwa watu.

Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.

Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa.

Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho.

Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hiyo ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu.

Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki.

Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Luther, Calvin na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki.

Mji wa Mungu[hariri | hariri chanzo]

Juu ya uhusiano kati ya serikali na kanisa aliandika kitabu "De civitate Dei" (maana yake kwa Kilatini ni: Mji wa Mungu. Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala").

Alieleza kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au Kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa.

Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Agostino alifahamu taratibu za Waroma Wapagani waliotazama makaisari wao kuwa miungu, na vilevile habari za demokrasia ya Kigiriki ya kale. Akafahamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwa moto na maadui katika siku zake jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babeli na Yerusalemu.

Pamoja na "mji" huo alisema upo "mji" wa pili ndio mji wa Mungu ambao ni mji wa upendo na undugu wenye neema yake.

Miji yote miwili iko pamoja ingawa taratibu zao ni tofauti. Mkristo ni raia wa miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu pande zote mbili. Lakini ajue kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Kumbe mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashiriki enzi ya Mungu.

Ndiyo sababu inafaa serikali isikie mawazo ya Kanisa, kwani ni kwa njia ya Kanisa kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu.

Ni kutokana na mafundisho hayo pia kwamba Kanisa la Magharibi lilijifunza umuhimu wa kuwa na msimamo imara mbele ya serikali mbalimbali kama ulivyojitokeza katika historia ndefu ya Kanisa, ingawa Agostino alijua jinsi Kaisari Theodosi alivyotubu kanisani baada ya askofu Ambrosi wa Milano kumtenga kwa sababu aliwatuza wanajeshi wa serikali yake walioua watu wengi ovyo walipotuliza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Watu wengi pamoja na Askofu walisikitikia tendo hilo. Baadaye Theodosi alipotaka kuingia katika ibada, Askofu huyo alimtangaza ametengwa kwa sababu ya kumwaga damu ya Wathesalonike, hivyo hawezi kushiriki meza ya Bwana. Kaisari akakubali kosa mbele ya umati. Hata baadaye viongozi wa Kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano wa Ambrosio na mafundisho ya Agostino.

Mafundisho hayo yaliathiri mawazo na fikra za Wakristo kwa karne nyingi za baadaye.

Tunaweza kuona aina mbili za matokeo ya urithi huo.

Kwa upande mmoja Kanisa lilijaribu kutawala jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za Kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na wale wa Kanisa. Hoja hiyo huitwa "Uklerikali" (clericalism).

Nguvu ya kisiasa ya Kanisa ilifikia kilele chake mwanzoni mwa karne ya 13 wakati wa Papa Inosenti III, halafu ilizidi kupungua hadi kupingwa kabisa na mapinduzi mbalimbali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789).

Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu tofauti na ya mtawala na hata vita.

Agostino aliingiza pia hoja ya "vita halali" katika Ukristo uliowahi kukataa ukatili na vita kama dhambi dhidi ya Mungu. Agostino alieleza kwamba wakati mwingine vita ni halali, na kama ni halali ni wajibu wa Mkristo pia. Maelezo hayo yalitumiwa baadaye na watawala na wanasiasa Wakristo kwa kutetea vita vya kila aina.

Lakini sehemu nyingine ya urithi huo imebaki: kazi ya Kanisa ya kuzitetea haki za binadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kuzigandamiza. Kwa mfano makanisa ndiyo yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika ya Kusini, hata dhidi ya serikali zilizoutetea. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka mzigo wa kupokea wageni maskini kutoka nchi jirani.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Wewe Bwana ni mkuu na unastahili kabisa sifa. Uweza wake ni mkuu na hekima yako haina mipaka. Mtu anataka kukusifu, yeye aliye sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, yeye anayetembea akielekea kifo, ushahidi wa dhambi yake, wa kwamba wewe unapinga wenye kiburi. Hata hivyo mtu, sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, anataka kukusifu. Wewe unamchochea aonje furaha ya kukusifu, kwa kuwa umetuumba kwa ajili yako, na moyo wetu hautulii mpaka ustarehe ndani mwako.

Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto!

Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia. Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako.

Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.

Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka.

Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako.

Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako.

Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako.

Maandishi yake makuu[hariri | hariri chanzo]

Maandishi kuhusu maisha yake[hariri | hariri chanzo]

 • Confessiones (Maungamo) 397-398 - anamoeleza maisha yake pamoja na njia yake ya imani. Ni kitabu ambacho baada ya Biblia kilisomwa zaidi katika Karne za Kati
 • Retractationes (Masahihisho) 426-428 - anamopitia maandiko yake ya awali akitaja mifano jinsi alivyobadilisha mawazo na hoja zake

Maandishi juu ya falsafa na teolojia[hariri | hariri chanzo]

 • De Musica (kuhusu muziki)
 • De civitate Dei (Mji wa Mungu) 413 - 426
 • De Trinitate (Kuhusu Utatu) 400-416 - andiko lake kubwa lenye vitabu 15
 • De doctrina christiana (kuhusu mafundisho ya kikristo) 397-426
 • De libero arbitrio (kuhusu nia huru)
 • De beata vita (kuhusu maisha mema) -- kuhusu raha na kumjua Mungu
 • De magistro (juuy a mwalimu) -- mafundisho kuhusu umuhimu wa lugha
 • De vera religione (kuhusu dini ya kweli) -- kuhusu imani ya kikristo
 • Soliloquia (mazungumzo na nafsi) -- kuhusu uwezo wa akili ya kujijua
 • De immortalitate animae(kuhusu roho isiyokufa)

Marejeo kwa Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

 • MT. AUGUSTINO, Kanuni– tafsiri ya Mapadri Waaugustino – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1992 – ISBN 9976-67-059-1
 • M. CULLEN, O.S.A., Maungamo ya Mtakatifu Augustino kwa Muhtasari – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda – ISBN 9976-63-643-1
 • M. CULLEN, O.S.A., Mtakatifu Monika: Mlinzi wa Akina Mama Wakristu – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 2002 – ISBN 9976-63-641-5

Vyanzo vingine[hariri | hariri chanzo]

g Saint Augustine, pages 30, 144; City of God 51, 52, 53 and The Confessions 50, 51, 52
 • Nelson, John Charles (1973). "Platonism in the Renaissance", Dictionary of the History of Ideas 3. New York: Scribner, 510–15 (vol. 3). ISBN 0684132931. “(...) Saint Augustine asserted that Neo-Platonism possessed all spiritual truths except that of the Incarnation. (...) 
 • Brown, Peter (1967). Augustine of Hippo. Berkeley: University of California Press. ISBN 0-520-00186-9. 
 • Matthews, Gareth B. (2005). Augustine. Blackwell. ISBN 0-631-23348-2. 
 • O'donnell, James (2005). Augustine: A New Biography. New York: ECCO. ISBN 0060535377. 
 • Ruickbie, Leo (2004). Witchcraft out of the Shadows. London: Robert Hale, 57–8. ISBN 0709075677. 
 • Tanquerey, Adolphe (2001). The Spiritual Life: A Treatise on Ascetical and Mystical Theology. Rockford, IL: Tan Books & Publishers, 37). ISBN 0895556596. 
 • von Heyking, John (2001). Augustine and Politics as Longing in the World. Columbia: University of Missouri Press. ISBN 0826213499. 
 • Lubin, Augustino (1659). Orbis Augustinianus sive conventuum ordinis eremitarum Sancti Augustini - chorographica et topographica descriptio. 
 • Pollman, Karla (2007). Saint Augustine the Algerian. Göttingen: Edition Ruprecht. ISBN 3897442094. 
 • Règle de St. Augustin pour les religieuses de son ordre; et Constitutions de la Congrégation des Religieuses du Verbe-Incarné et du Saint-Sacrament (Lyon: Chez Pierre Guillimin, 1662), pp. 28–29. Cf. later edition published at Lyon (Chez Briday, Libraire,1962), pp. 22–24. English edition, (New York: Schwartz, Kirwin, and Fauss, 1893), pp. 33–35.
 • Zumkeller O.S.A., Adolar (1986). Augustine's Ideal of the Religious Life. New York: Fordham University Press. ISBN 0823211053. 
 • Zumkeller O.S.A., Adolar (1987). Augustine's Rule. Villanova: Augustinian Press. ISBN 0941491064. 
 • Pottier, René (2006). Saint Augustin le Berbère (in French). Fernand Lanore. ISBN 2851572822. 
 • Fitzgerald, Allan D., O.S.A., General Editor (1999). Augustine through the Ages: An Encyclopedia. Grand Rapids: William B. Eerdmans Publishing Co.. ISBN 0-8028-3843-X. 
 • Plumer, Eric Antone, (2003). Augustine's Commentary on Galatians. Oxford University Press. ISBN 0-199-24439-1. 
 • Weiskotten, Herbert T. (2008). The Life of Saint Augustine: A Translation of the Sancti Augustini Vita by Possidius, Bishop of Calama. Merchantville, NJ: Evolution Publishing. ISBN 1-889-75890-6. 
 • Pagels, Elaine Adam, Eve, and the Serpent: Sex and Politics in Early Christianity Vintage Books (Sep 19 1989) ISBN 0-679-72232-7

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]