Nenda kwa yaliyomo

Ekaristi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Meza ya Bwana)
Vipaji vya mkate na divai vilivyoandaliwa kwa adhimisho la ekaristi.


Ekaristi (pia Chakula cha Bwana) ni ibada iliyowekwa na Yesu Kristo wakati wa karamu ya mwisho, usiku wa kuamkia Ijumaa Kuu, siku ya mateso na kifo chake msalabani. Kwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ekaristi ni sakramenti, tena moja ya sakramenti kuu.

"Chakula cha Bwana" ni jina ambalo lilitumika na Mtume Paulo alipotaja ibada hiyo katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho[1]

Jina "ekaristi" ambalo ni kawaida katika Kanisa Katoliki linatokana na neno la lugha ya Kigiriki εὐχαρίστω (eukharisto: "nashukuru") lililotumiwa na Mtume Paulo na Wainjili katika kusimulia hiyo karamu ya mwisho ya Yesu na Mitume wake, na muujiza uliotangulia ambao Yesu alidokeza nia yake ya kushibisha watu wote, yaani ule wa kuzidisha mkate na samaki kwa ajili ya umati wa watu waliokusanyika

Jina linaonyesha mazingira ya sala katika matukio hayo, ambapo Yesu alimuelekea Mungu akimshukuru kwa vyakula na vinywaji alivyoshika mikononi mwake kabla hajawagawia wanafunzi wake.

Shukrani ilikuwa msimamo wa msingi wa Yesu kwa Baba maisha yake yote, hasa alipofikia wakati wa kutolewa awe kafara ya wokovu wa watu. “Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, ‘Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, ‘Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mlapo na mnywapo, kwa ukumbusho wangu’” (1Kor 11:23-25). Ndiyo maandishi ya kale zaidi tuliyonayo juu ya tukio hilo.

Mkate na divai

[hariri | hariri chanzo]

Yesu alitumia mkate na divai kwa sababu vilikuwa vya maana sana katika utamaduni wa taifa lake na katika Agano la Kale. Vilikuwa chakula cha kawaida na kinywaji cha karamu. “Divai imfurahishe mtu moyo wake... na mkate umburudishe mtu moyo wake” (Zab 104:15). Vilitokana na chembe za ngano na matunda ya mzabibu ambavyo Yesu alijifananisha navyo. “Amin, amin, nawaambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yoh 12:24). “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5). Baada ya kulimwa, vilihitaji kusagwa au kushinikizwa, matendo yanayodokeza tena mateso yake pamoja na kazi ya binadamu. Pia wingi wa chembe na wa zabibu zinazoungana ziwe mkate na divai unamaanisha umoja wa waamini ndani ya Kristo. Kwa hiyo ni lazima vitumike daima mkate na divai, si vitu vingine.

Mara nyingine Wakatoliki wanapokea umbo la mkate tu kwa lengo la kukwepa umwagaji wa Damu ya Kristo na kurahisisha ibada, hasa kama washiriki ni umati (hata milioni 6 katika misa moja ilivyotokea Manila, Ufilipino, wakati wa ziara ya Papa Fransisko). Yesu mwenyewe alizungumzia mkate kuliko divai, kwa sababu chakula ni muhimu kuliko kileo. “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” (Yoh 6:51). “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:17). Kwa Wakatoliki anayekula umbo la mkate hapokei sehemu tu ya Yesu, bali anampokea mzima, Mwili, Damu, Roho na Umungu. Pamoja na hayo, daima ni lazima walau padri anywe umbo la divai.

“Melkizedeki mfalme wa Salemu alileta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana” (Mwa 14:18), “amefananishwa na Mwana wa Mungu” (Eb 3:7). “Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana” (Isa 25:6). “Njoo, ule mkate wangu, ukanywe divai niliyoichanganya” (Mith 9:5-6). Yesu alishiriki karamu nyingi na katika mojawapo ndipo alipoanza miujiza yake kwa kugeuza mapipa ya maji kuwa divai bora. “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa” (Yoh 2:10). “Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa, nanyi mwasema, ‘Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi” (Lk 7:34).

Hatimaye Yesu alitumia divai kuachia ishara ya damu yake ili wafuasi wake waweze kushiriki mateso yake. “Je, mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?” (Math 20:22). Kisha kushiriki kila mwaka karamu ya Pasaka, ambapo wote walikunywa divai mara nne, safari ya mwisho alikamilisha miujiza yake kwa kuigeuza iwe damu yake. “‘Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu’. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, ‘Twaeni hiki, mgawanywe ninyi kwa ninyi; maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja’. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, ‘Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula, akisema, ‘Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu’” (Lk 22:15-20). “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je, si ushirika wa damu ya Kristo?” (1Kor 10:16).

Ushuhuda wa Biblia

[hariri | hariri chanzo]

Agano Jipya linasimulia mara nne matendo na maneno ya Yesu ambayo alianzisha ibada hiyo na kuwakabidhi Mitume wake.

Simulizi la zamani zaidi ni lile la 1Kor 11:23-25. Likafuata lile la Mk 14:22-24; halafu yale ya Math 26:26-28 na Lk 22:19-20.

Kadiri ya ushuhuda huo, Yesu, katika karamu ya mwisho aliwagawia mitume wake mkate na divai akisema ndio mwili wake na damu yake vitakavyotolewa kama kafara kwa ondoleo la dhambi za umati, akawaagiza wafanye vilevile kwa ukumbusho wake.

Hivyo Kanisa tangu hapo, linaendeleza ibada hiyo maalumu na ya msingi katika mazingira mbalimbali.

Simulizi la Paulo linafanana na lile la Mwinjili Luka na kufuata jinsi ekaristi ilivyoadhimishwa kati ya Wakristo wa mataifa; kumbe Mwinjili Marko na Mwinjili Mathayo waliripoti adhimisho lilivyokuwa kati ya Wakristo wa Kiyahudi.

Maendeleo

[hariri | hariri chanzo]
Papa Benedikto XVI akiadhimisha ekaristi.

Karne zilizofuata ibada ilizidi kubadilika, hasa ilipotenganishwa na mlo wa kawaida ulioendana nayo awali. Badala ya mlo huo, ibada iliunganishwa na masomo ya Neno la Mungu.

Ekaristi inaadhimishwa kwa mpangilio wa kupanda: waamini wanalishwa Neno la Mungu katika mimbari, halafu Mwili na Damu ya Kristo katika altare. Vilevile sehemu ya kwanza (liturujia ya Neno) inaleta masomo yakiwa na kilele katika Injili. Halafu katika sehemu ya pili (liturujia ya ekaristi) padri anafuata alichofanya Yesu katika karamu ya mwisho: anatwaa mkate na divai (kuandaa dhabihu), anashukuru juu yake (sala kuu ya ekaristi inayogeuza dhabihu) na kuwapa waamini (komunyo, kilele cha yote, inayowageuza ndani ya Kristo). Yesu mfufuka “aliwaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe... Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua” (Lk 24:27,30-31). “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali” (Mdo 2:42). “Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu... akamega mkate, akala” (Mdo 20:7,11). Usipofuata vizuri hatua za awali, hutafaidika kweli na sakramenti: ndiyo sababu ni muhimu uwahi ibada.

Kati ya namna mbalimbali za kuiadhimishwa, yalijitokeza mapokeo ya mashariki na ya magharibi. Kwa jumla mapokeo ya mashariki yanahusisha milango ya fahamu na ni ya fahari kuliko yale ya magharibi.

Teolojia

[hariri | hariri chanzo]

Kwa Wakristo ekaristi inahusiana sana na Pasaka, yaani kifo na ufufuko wa Yesu vilivyotokea kwenye sikukuu hiyo ya Wayahudi.

Kadiri ya Injili Yesu Kristo aliweka ekaristi wakati wa kuadhimisha karamu ya Pasaka ya Kiyahudi, akaipatia maana mpya kuhusiana na kifo na ufufuko wake.

Madhehebu mengi ya Kikristo yamekubali hati ya kiekumeni ya Lima (1982) inayosema "Ekaristi ni ukumbusho wa Yesu msulubiwa na mfufuka, yaani ishara hai na ya nguvu ya sadaka yake, ambayo ilitolewa mara moja tu msalabani na inaendelea kutenda kwa faida ya binadamu wote".

Wakatoliki na Waorthodoksi wanaamini kwamba katika karamu ya Bwana wanakula na kunywa Mwili wa Damu ya Kristo. Katika sala kuu ya ekaristi padri anaporudia maneno ya Yesu juu ya mkate na divai na kumuomba Roho Mtakatifu, huyo anavigeuza kwa dhati: mkate si tena mkate, wala divai si tena divai, ingawa maumbo yanabaki yaleyale kwa hisi zetu. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli” (Yoh 6:54-55). “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana” (1Kor 11:27).

Baada ya mageuzo Yesu anabaki katika ekaristi moja kwa moja. Maumbo ya mkate na divai yanazidi kudokeza uwepo wake kama chakula na kinywaji cha watu, hata kwa faida ya wagonjwa na wengineo wasiohudhuria. Ndiyo sababu Wakristo hao wanazidi kumuabudu katika ekaristi, ingawa hawamuoni. “Tomaso alijibu, akamwambia, ‘Bwana wangu na Mungu wangu!’ Yesu akamwambia, ‘Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yoh 20:28-29).

Vilevile Wakatoliki na Waorthodoksi wanaamini ekaristi ni kafara ambayo Yesu alimtolea Baba msalabani na anaendelea kumtolea kwa wokovu wa watu. “Yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee... Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa” (Eb 7:24-25; 8:3). Katika ekaristi tunajiunga naye kwa kufanya ukumbusho wa kifo na ufufuko wake, tukimtolea tena Baba sadaka ya Mwili na Damu yake iliyolinganishwa na zile za Waisraeli na za Wapagani: “Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je, hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani” (1Kor 10:18-21).

Ekaristi inaitwa sakramenti ya upendo kwa sababu kila unapofanyika ukumbusho wa sadaka hiyo pekee waamini wanazidi kujifunza na kupokea upendo ambao siku hiyo Yesu “ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo” (Yoh 13:1). Hivyo wanawezeshwa kutekeleza amri mpya aliyowaachia pamoja na ekaristi. “Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (Yoh 13:34). Ni sharti wajitoe kama Yesu, wakijiunga na sadaka yake katika ibada na katika maisha. “Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma yake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yoh 3:16-18).

Katika mpangilio wa sakramenti saba

[hariri | hariri chanzo]
Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi

Katika imani ya Kanisa Katoliki na Waorthodoksi sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai. Walioshiriki kifumbo kifo na ufufuko wake wakapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, wanaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapowalisha na kuwanywesha Mwili na Damu yake ili washiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57). Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani ya mtu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.

Katika maisha ya Kiroho

[hariri | hariri chanzo]

Anayelenga ukamilifu wa Kikristo anatakiwa kuishi zaidi na zaidi kwa ekaristi, si tu kwa kuhudhuria misa, bali hasa kwa kuipokea mara nyingi, hata kila siku. Kwa ajili hiyo tuseme juu ya mkate wa uzima na juu ya masharti ya kuupokea vema, halafu motomoto.

Ekaristi ndiyo mkate hai kutoka mbinguni

[hariri | hariri chanzo]

Bwana hakuweza kujitoa kwa wokovu wa wote jumla kuliko alivyojitoa msalabani, na sasa hawezi kujitoa kwa kila mmojawetu kuliko anavyojitoa katika ekaristi. Akijua mahitaji yetu, alituahidia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe… Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu… Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake” (Yoh 6:35,51,55-56).

Ekaristi ndiyo sakramenti kuu, kwa sababu ndani mwake haimo neema tu, bali yumo aliyetustahilia neema. Ndiyo sakramenti ya upendo, kwa sababu ni tunda la upendo unaojitoa, na tokeo lake kuu ni kustawisha ndani mwetu upendo wa Mungu na wa watu. Kuipokea kunaitwa “komunyo” (= ushirika kwa Kilatini) yaani muungano wa dhati na Mungu na watu unaolisha roho iishi Kimungu zaidi na zaidi; kwa namna fulani unaifanya iwe ya Kimungu kwa kustawisha neema inayotia utakatifu.

Kila kiumbe hai kinahitaji lishe: mimea inajilisha rutuba ya ardhi; wanyama wanajilisha mimea au viumbe vingine; binadamu analisha mwili wake kwa vyakula vya kufaa, na anatakiwa kulisha akili yake kwa ukweli, hasa wa Kimungu, tena utashi wake kwa matakwa ya Mungu anayopaswa kuyatekeleza kila siku ili kufikia uzima wa milele. Kwa maneno mengine, anatakiwa kujilisha imani, tumaini na upendo; matendo ya maadili hayo yanamstahilisha ustawi wa uzima upitao maumbile. Lakini Mwokozi anamtolea chakula kingine, cha Kimungu zaidi: anajitoa kuliwa alivyomuambia Augustino, “ndimi chakula cha wenye nguvu; kua unile. Lakini hutanigeuza ndani mwako unavyogeuza chakula cha mwili wako; kinyume chake wewe utageuzwa ndani mwangu”. Katika ushirika huo Mwokozi hapati faida yoyote, ila mwamini anahuishwa Kimungu. Maadili ya Yesu yanamuingia awe kiungo hai zaidi cha mwili wake wa fumbo. Hasa Yesu aliyemo katika ekaristi anamfanya ampende Mungu kwa usafi na nguvu zaidi.

“Matokeo yale ambayo mateso ya Kristo yalisababisha ulimwenguni, sakramenti hii inayasababisha ndani ya kila mmojawetu… Kama vile chakula cha kawaida kinavyotegemeza uhai wa mwili na kuuongeza na kuuburudisha na kupendeza kwa ladha, ekaristi inasababisha rohoni matokeo ya namna hiyo” (Thoma wa Akwino). Kwanza inategemeza: mtu ambaye upande wa mwili hajilishi au anajilisha vibaya anadhoofika; inatokea vilevile upande wa roho asipokula mkate upitao maumbile anaopewa na Bwana kama chakula bora cha kila siku. Kama vile chakula cha kawaida kinavyoburudisha mwili kwa kufidia ulichopoteza kwa ugumu wa kazi, ekaristi inafidia nguvu zilizopungua kutokana na uzembe wetu: inatuondolea dhambi nyepesi na kuturudishia ari iliyopotea kwa dhambi hizo, pia inatukinga na dhambi ya mauti. Chakula cha kawaida kinakuza uhai wa mtoto anayetakiwa kuwa mtu mzima. Upande wa roho, tunapaswa kukua daima katika upendo hadi kufa kwetu: hivyo tu tunazidi kuelekea uzima wa milele. Mkate wa ekaristi unatuletea neema mpya daima kwa ajili ya ustawi huo; ndani ya watakatifu, kila siku zaidi imani inakuwa angavu na hai, tumaini linakuwa imara na upendo safi na motomoto. Polepole, badala ya kuvumilia tu mateso wanakuja kuthamini na kupenda msalaba. Kwa komunyo maadili yanakua pamoja hata kufikia ushujaa, na vipaji vya Roho Mtakatifu vinastawi pamoja nayo. Hatimaye, kama vile chakula cha kawaida kinavyonoga, mkate wa ekaristi ni mtamu kwa mtu mwaminifu anayechota humo faraja na hisi ya kuwa na afya.

“Kwa kutegemea wema wako na huruma yako kubwa, Ee Bwana wangu, nathubutu kukujongea; mimi mgonjwa nakujia wewe Mwokozi wangu, mimi mwenye njaa na kiu nakutafuta asili ya uzima… mimi niliye kiumbe nakujia Muumba, katika majonzi nakujia wewe mtuliza wangu mwema… Ukijitolea kwangu imenitosha; kama hupo sipati kutulia. Siwezi kukaa mbali nawe; sina uhai nisipokuona” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,2:1; IV,3:2). “Jambo la ajabu! Mtu maskini, mtumishi na mnyonge anamla Bwana!” (Thoma wa Akwino). Kumbe mara nyingi mazoea yanatuzuia tusizingatie uangavu wa Kimungu wa zawadi hiyo isiyo na kifani!

Masharti ya kupokea vema

[hariri | hariri chanzo]

Masharti hayo yanatajwa na hati ambayo Papa Pius X aliwahimiza waamini wote kupokea ekaristi mara nyingi: “Tunapaswa kujitahidi tutangulize maandalizi mema kabla hatujapokea, halafu kutoa shukrani kwa namna ya kufaa, kulingana na uwezo na hali ya kila mmoja”. Sharti la kwanza ni nia nyofu: “anayeikaribia meza takatifu asiende kwa mazoea tu, kwa majivuno au kwa sababu nyingine ya kibinadamu, bali atake kumtimizia Mungu hamu yake, kuungana naye kwa dhati kwa njia ya upendo, na kuponya maradhi yake na kasoro zake kwa dawa hiyo ya Kimungu”. Mtu akiwa na nia nyingine (k.mf. hamu ya kusifiwa) pamoja na hiyo ya kwanza, komunyo itabaki njema, lakini matunda yatapungua. Komunyo moja motomoto ina faida kuliko nyingi vuguvugu.

Masharti ya kupokea motomoto

[hariri | hariri chanzo]

Katerina wa Siena alitoa mfano wa watu wanaotafuta mwanga kwa mishumaa yenye ukubwa tofauti, ambayo mkubwa unaangaza kuliko mdogo. Inatokea vilevile kwa sakramenti hii, ambayo matunda yake yanalingana na hamu takatifu ya kila anayeikaribia. Hamu hiyo inajitokeza hasa kwa kukomesha mshikamano wowote na dhambi nyepesi. Mshikamano huo unastahili lawama ndogo kwa Wakristo wenye ujuzi mdogo kuliko kwa wale waliopokea zaidi. Huo uzembe na utovu wa shukrani ukiongezeka, utafanya komunyo ilete faida ndogo zaidi na zaidi. Ili hiyo iwe motomoto tusishikamane na matendo mapungufu, yaani kutenda mema kiasi, kutopambana kwa nguvu na kasoro zetu, na kujitafutia maburudiko halali yasiyo ya lazima (k.mf. kinywaji). Kujinyima kunampendeza Mungu, naye Mkristo akiwa mkarimu zaidi atazidishiwa neema katika komunyo. Kielelezo chetu ni Mwokozi aliyejitoa sadaka hadi msalabani, nasi tunapaswa kuufanyia kazi wokovu wetu na wa wenzetu kwa njia zilezile za Yesu.

Kujitenga na dhambi nyepesi na matendo mapungufu ni msimamo wa kutotenda; misimamo ya kutenda ni: unyenyekevu (Bwana, sistahili), heshima kwa ekaristi, imani hai, hamu ya kumpokea Bwana, ambayo yote inajumlishwa katika neno moja: kuwa na njaa ya ekaristi. Tukiwa na njaa, kila chakula ni kitamu; tukiwa na njaa ya ekaristi kwa kuamini ndiyo chakula cha lazima kwa roho yetu, komunyo italeta matunda mengi. Ikiwa hamu ya chakula imetuishia, tunapaswa “kufanya mazoezi” ili kuipata tena; upande wa roho mazoezi ni kumtolea Mungu sadaka fulani, hasa kujikana badala ya kujipendea katika yote. Polepole umimi utatoweka, na upendo utatawala bila pingamizi; tutaacha kuhangaikia mambo madogo yanayotuhusu ili tuzingatie zaidi utukufu wa Mungu na wokovu wa watu. Hapo njaa ya ekaristi itaturudia.

Kwa walio dhaifu tunatafuta chakula cha kufaa kuwarudishia nguvu. Basi, tutafute pia kinachofaa zaidi kutengeneza upya nguvu za roho. Hisi zetu zinazoelekea tamaa na uvivu zinahitaji kuhuishwa kwa kugusa mwili safi wa Kristo uliostahimili mateso makali kwa upendo. Roho yetu, inayoelekea kiburi, upumbavu, kutojali na kusahau kweli kuu, inahitaji kuangazwa na mguso wa akili angavu ya Mwokozi. Utashi wetu unakosa nguvu, ni baridi kwa kupungukiwa upendo; nani anaweza kuurudishia moto unaohitajika kama si mguso wa moyo wa Yesu ulio tanuri ya upendo, ambao utashi wake mwadilifu daima ni chemchemi ya stahili zisizopimika? “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema” (Yoh 1:16). Tunahitaji huo muungano na Mwokozi ulio tokeo kuu la komunyo.

Matunda ya komunyo yanalingana na ubora wa misimamo yetu. “Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele” (Math 13:12). Mfano wa matokeo ya komunyo motomoto ni Eliya alipoishiwa nguvu katika kukimbia dhuluma; malaika akamuonyesha “mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, ‘Inuka, ule, maana safari hii ni kubwa mno kwako’. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku, hata akafika Horebu, mlima wa Mungu” (1Fal 19:6-8). Tukumbuke kila komunyo inatakiwa kuwa bora kuliko iliyotangulia, kwa kuwa kila moja inakusudiwa kustawisha upendo na hivyo kutuandaa kumpokea Bwana kwa upendo mkubwa zaidi. Ndiyo sheria ya kuongeza kasi inayotakiwa kutimia hasa kwa komunyo ya kila siku, tunavyoona katika watakatifu, ambao miaka yao ya mwisho ilikuwa na maendeleo ya kasi kuliko ile ya nyuma; ilitimia hasa kwa Maria, kielelezo cha ibada kwa ekaristi. Mungu atujalie tufanane nao.

“Nani anaweza kuikaribia kwa unyenyekevu chemchemi ya utamu, asionje utamu walau kidogo? Nani ajongee moto unaowaka mno, asisikie joto hata kidogo? Basi, ndiwe chemchemi iliyojaa utamu siku zote kabisa; ndiwe moto unaowaka daima, bila kufifia” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,4:3). Hiyo chemchemi ya neema ni bora hata istahili kupatiwa pamoja sifa za maji yanayoburudisha na za moto uwakao. Yaliyotenganika upande wa viumbe yameunganika katika ekaristi. Tukienda kumpokea Yesu tumfikirie mtume Yohane aliyeegemea moyoni pake, na Katerina wa Siena aliyejaliwa kunywa kwa wingi katika donda la moyo huo ulio wazi daima ili kutuonyesha upendo wake. Tumuombe pia bikira Maria atushirikishe upendo aliokuwa nao katika kuipokea ekaristi kwa mikono ya Yohane.[2]

Katika maendeleo ya Kiroho

[hariri | hariri chanzo]

Kila Komunyo inatakiwa kustawisha upendo na hivyo kutuandaa tumpokee Bwana vizuri zaidi kesho yake. Komunyo ya kwanza ni neema kubwa, lakini zile zinazofuata zinatakiwa kuzaa matunda makubwa zaidi na zaidi. Katika safari yetu ya kumuendea Mungu ongezeko la kasi linatakiwa kupatikana katika wale wanaoendelea kuliko kwa wanaoanza. Ili tuelewe Komunyo ya wanaoendelea inavyotakiwa kuwa, tukumbuke kwamba tokeo lake kuu ni kustawisha upendo, ambao ndio adili linalotakiwa kukua zaidi ndani yao, na kwamba upendo wa kidugu ndio dalili kuu ya upendo kwa Mungu. Tutaelewa zaidi kwa kuzingatia Komunyo inavyohakikisha, kwa njia ya muungano na Bwana, umoja na ustawi wa mwili wake wa fumbo.

Karamu takatifu na umoja wa Mwili wa Fumbo

[hariri | hariri chanzo]

“Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:17). Mabishano yoyote yakome kwenye meza ya waamini wote. Ushirika wao katika mwili wa Kristo ndio “ishara ya umoja, kiungo cha upendo!… Bwana ametupa mwili wake na damu yake katika maumbo ya mkate na divai. Kama vile mkate unavyotokana na chembe nyingi za ngano, na divai inavyotokana na zabibu nyingi, vivyo hivyo Kanisa la Kristo linatakiwa kutokana na wingi wa waamini waliounganishwa na upendo” (Augustino). Papa Pius X alipowaalika tena waamini kupokea ekaristi mara nyingi na hata kila siku, alikumbusha kuwa “karamu takatifu ndiyo ishara, mzizi na chanzo cha umoja wa Kikatoliki”.

Kwa msingi huo kabla hatujapokea tufikirie vizuio tunavyoweka pengine kwa muungano wa upendo na Yesu na viungo vyake. Tumuombe tuone vizuio hivyo vinavyotokana nasi, na tuwe na juhudi za kuviondoa; tena, tukiwa wazembe katika kuviondoa, tuombe aviondoe hata kwa kututia uchungu. Katika maandalizi ya Komunyo tuseme, “Nakutolea yaliyo mema ndani mwangu, ijapo ni machache na hafifu, kusudi uyatakase zaidi na kuyakamilisha… Nakutolea pia tamaa takatifu zote za watu wema… Nawaombea wote waliotaka niwakumbuke katika sala… Nakutolea pia sala zangu na sadaka ya kitubio kuwaombea hasa watu ambao walinidhuru, walinichukiza, walinidharau au kunikosea kwa namna yoyote. Vilevile nawaombea wale ambao siku moja niliwatia uchungu, niliwaudhi, niliwalemea na kuwakwaza kwa maneno au kwa matendo, kwa kujua au la, kusudi utuondolee dhambi zetu na makosa tuliyokosa. Ee Bwana, ondoa moyoni mwetu dhana zote za kudhaniana, chuki yote, hasira, ugomvi na lolote ambalo linavunja mapendano au kupunguza mapatano ya kidugu” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,9:4-6). Komunyo iliyopokewa hivyo inahakikisha maishani umoja na Mwokozi na wote aliowahuisha, ili atawale na amani yake.

Komunyo na ustawi wa Mwili wa Fumbo

[hariri | hariri chanzo]

Komunyo inatakiwa kuchangia na kuhakikisha pia ustawi wa mwili wa fumbo wa Mwokozi: “Tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa... huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo” (Ef 4:15-16). Mwokozi anajenga hivyo viungo vyake hasa katika ekaristi; kwa kupokea mkate wa uzima hao wanaufikia ukamilifu waliopangiwa na Mungu. “Kama vile ubatizo, mlango wa sakramenti, unavyosababisha ndani mwetu chanzo cha uzima wa Kiroho, ekaristi inasababisha utimilifu wake; yenyewe ni kama lengo la sakramenti nyingine ambazo zinatuandaa kuipokea… Kwa hiyo tokeo la ubatizo rohoni… linalenga lile la ekaristi” (Thoma wa Akwino), kama utoto unavyolenga ukomavu wa utu uzima. Kwa maana hiyo hamu fulani ya tokeo la ekaristi ni ya lazima kwa wokovu.

Hatuwezi kuufikia ukamilifu wa Kikristo tusipojiandaa kupokea ekaristi vizuri na kwa manufaa zaidi na zaidi. Tena si kila Mkristo tu, bali kila parokia, kila jimbo na Kanisa lote katika kila kizazi ndivyo wanavyofikia ukomavu na kuzaa kwa kueneza imani kama mbegu takatifu. Kila wakati una matatizo yake, na Mkristo anatakiwa kujipatia nguvu katika ekaristi leo kama wakati wa dhuluma. Anapaswa kuwa na njaa ya ekaristi, yaani kutamani kuunganika na Kristo kwa undani wa utashi hata ashinde vishawishi vyote akiendelea kutimiza maadili katika nafasi ngumu.

Tumuambie, “Kweli ndiwe mpenzi wangu kabisa; nimekuchagua kati ya maelfu. Roho yangu inapenda kukaa nawe siku zote za maisha yangu. Kweli ndiwe unayenituliza, kwako napata amani kuu na raha kamili; mbali nawe pana masumbuko na uchungu na tabu isiyo na mwisho… Siwezi kueleza uzuri wa tabia yako. Kusudi uwaonyeshe wadogo wema wako, umependa kuwalisha mkate mtamu mno unaotoka mbinguni” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,13:1-2).

Kwa kuupokea motomoto yanatimia maneno ya Zaburi (31:19): “Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako ulizowawekea wakuchao!” “Ndio wanaomtambua Bwana wao kwa namna anavyomega mkate, ambao moyo wao unawaka sana wakiwa njiani pamoja na Yesu. Mara nyingi sina ibada ya nguvu namna hii, sina upendo kama huo, wala sisikii moyo kuwaka. Ee Yesu mwema, mpole, mpendevu! Nipe mimi, maskini wako, nisikie mara moja tu mwako wa moyo walau kidogo wakati ninapopokea Komunyo, ili nizidi kukusadiki kwa imara, kuutumainia wema wako, kukupenda kwa upendo kamili usiopoa, kama chakula hiki cha mbinguni kimewasha moto moyo wangu. Huruma yako ina uwezo wa kunipa neema hii ninayopupia mno. Unaweza kunijia kwa upole wako siku yoyote utakayotaka na kunitia moto moyoni” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,14:2-3).

Njaa ya ekaristi inaelezwa hivi, “Napenda kukupokea wewe, Bwana, kwa ibada kubwa sana, kwa upendo unaowaka, kwa hamu yote ya moyo wangu na kwa shauku ya nguvu, vile walivyokutamani watakatifu na watu wema wengi wakati wa kutaka Komunyo. Walikupendeza kabisa kwa usafi wa mwenendo wao na kwa bidii yao iliyokuwa kama moto usiozimika… Napenda kukutolea nafsi yangu na yote niliyo nayo kwa hiari yangu na kwa moyo mkuu. Ee Bwana Mungu wangu, uliyeniumba, uliyenikomboa, leo napenda kukupokea kwa heshima ile na ibada, na sifa na adabu, na shukrani na utaratibu na mapenzi, kwa imani na tumaini na usafi, alivyokuwa navyo Mama yako mtukufu bikira Maria alipokuchukua mimba… Nakutolea furaha za watakatifu wote, mapenzi yao makubwa, shangwe za roho zao, miangaza waliyopewa nawe… pamoja na sifa zote na fadhila zote unazosifiwa… Nataka makabila yote ya kila nchi na ya kila lugha wakusifu, watukuze jina lako takatifu na tamu kama asali, kwa shangwe kuu na kwa ibada ya upendo” (Kumfuasa Yesu Kristo IV,17:1-5). Mkristo anayepokea kwa msimamo huo anamuelekea Mungu kasi zaidi na zaidi na kuvuta wengi nyuma yake: ndivyo unavyohakikishwa ustawi wa mwili wa fumbo wa Kristo. Lakini ni lazima tupige hatua nyingine upande wa ukarimu.

Komunyo ya kujitoa

[hariri | hariri chanzo]

Bwana ametuambia, “Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (Yoh 13:34). Mwenyewe ametupenda hata kutufilia msalabani na kujifanya chakula chetu. Basi Mkristo anapaswa kujifunza katika ekaristi ajitoe kama Bwana alivyofanya. Yesu anayetupatia kila siku ekaristi ndiye kielelezo bora cha kujitoa kikamilifu, naye anatukumbusha kuwa “ni heri kutoa kuliko kupokea!” (Mdo 20:35), kupenda kuliko kupendwa. Anayezidi kuunganika naye kwa njia ya ekaristi, anatakiwa kuwa chakula cha wanaomzunguka, akijitoa pasipo kipimo, hata akipatwa na uchungu wa kudhaniwa vibaya, ubaridi, uovu na uonevu. “Kwa mfano wa Bwana wetu, padri anapaswa kufia mwili wake, roho yake, matakwa yake, heshima yake, familia yake na ulimwengu; anapaswa kujitoa mhanga kwa kimya, sala, kazi, malipizi, mateso na kifo. Kadiri tulivyokufa tuna uhai na kuushirikisha” (Antoni Chevrier). Yaliyosemwa hapa kuhusu padri yanamfaa kila Mkristo aliyekomaa, ambaye ajitoe mhanga mfululizo ili kuwavuta wanaomzunguka kwenye lengo la safari wanalolisahau mara nyingi. Ari hiyo ya utukufu wa Mungu na ya wokovu wa watu ndiyo itikio ambalo wote walitoe kwa amri kuu ya Mwokozi. Katika Komunyo motomoto tutachota ukarimu huo ambao unang’ariza kwa wengine zawadi tuliyoipokea na unadhihirisha matunda yake. Kazi yetu ni kuupokea tu upendo wa Mungu na kumrudishia kwa kumpenda jirani.

  1. ona (1 Kor 11,20, "Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, 21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine."
  2. Waamini wengi wanatoka kanisani mara baada ya misa walipopokea sakramenti. Mara nyingi lilitolewa kwa faida fundisho la Filipo Neri aliyetuma watumishi wawili wenye mishumaa kumsindikiza mama aliyetaka kufanya hivyo. Lakini ni rahisi kuzoea vibaya, hivyo kuna komunyo nyingi, lakini washiriki halisi wachache. Kama hakutakuwa na watu wenye ari ya kwenda kinyume cha mkondo huo, utaangamiza roho yote ya ibada. Je, shukrani si wajibu kwa mtu aliyepokea fadhili? Je, haitakiwi kulingana na fadhili yenyewe? Basi, tuseme nini kuhusu utovu wa shukrani kwa Bwana ambaye fadhili zake zina thamani isiyopimika? Yesu alimshukuru Baba mara nyingi kwa fadhili zake, hasa kwa umwilisho, kwa kuwafumbulia watu wadogo mafumbo yake, naye hakomi kumshukuru katika misa na huko mbinguni. Kisha kuwaponya wakoma kumi, alipoona mmoja tu amerudi kushukuru, aliuliza, “Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?” (Lk 17:17). Katika ekaristi tunajaliwa fadhili kubwa kuliko muujiza wa kuponywa mwili: tunampokea aliyetustahilia wokovu, pamoja na ustawi wa uzima wa Kimungu na wa upendo. Basi, kama kuna kitu kinachodai shukrani za pekee ndicho ekaristi, ambayo Yesu amependa kubaki kweli kati yetu ili kuendelea kisakramenti kujitoa sadaka na kulisha roho zetu kuliko chakula bora chochote. Hatulishwi mafundisho ya mtakatifu fulani, bali ubinadamu wa Yesu Kristo uliojaa ukamilifu wa neema kwa kuungana na Neno katika Nafsi ya Kimungu. Fadhili isiyo na kipimo inadai shukrani inayolingana nayo. Kwa kuwa hatuwezi kumtolea Mungu shukrani ya namna hiyo, tumuombe bikira Maria atusaidie tushiriki shukrani aliyomtolea Mungu chini ya msalaba, baada ya neno “Yametimia”. Yesu anabaki kweli ndani mwetu mpaka maumbo ya sakramenti yanapodumu, yaani kama robo saa baada ya kupokea. Tunawezaje kushindwa kuongea naye muda huo mfupi? Tunashindwaje kuona kosa la kutoshukuru? Hatusemi juu ya watu wenye roho ya ibada wanaolazimika kutoka ili kutimiza wajibu halisi fulani. “Kisha kukomunika, siwezi kabisa kutoka kanisani. Muda uliopangwa na jumuia kwa kushukuru nauona mfupi hivi hata napaswa kujilazimisha kuifuata mezani” (Teresa Couderc). Bwana anatuita, anajitoa kwetu kwa upendo mkuu, nasi tusiwe na neno la kumuambia bali tuone vigumu kumsikiliza kidogo! Shukrani baada ya komunyo ndiyo fursa bora ya maisha ya Kiroho. Kiini cha misa ni mageuzo, lakini sisi tunaishiriki kwa njia ya komunyo, ambapo uwepo muungano wa roho takatifu ya Yesu na roho yetu; muungano wa akili yake iliyoangazwa na utukufu na akili yetu ambayo mara nyingi imejaa giza; muungano wa utashi wake wenye kusimama daima upande wa uadilifu na utashi wetu geugeu usioaminika; hatimaye muungano wa hisi zake safi na hisi zetu zinazovurugika mara nyingi. Yesu anasema na wale wanaomsikiliza, wasiotawanya mawazo kwa hiari, yaani si tu kwa makusudi mazima, bali pia kwa ulegevu katika kuzingatia, kutaka na kutenda yanayowapasa. Uzembe huo unasababisha dhambi nyingi za kutotimiza wajibu zisizozingatiwa katika kutafiti dhamiri. Wengi wanaoshindwa kuona dhambi yoyote ndani mwao, kwa sababu hawajatenda ya mauti, wamejaa dhambi za kutotimiza wajibu na za uzembe ambao kwa kiasi fulani ni wa hiari. Tusipuuzie wajibu wa kushukuru: komunyo zisizo makini zinaweza kuzaa matunda gani? Mapadri wengi baada ya misa hawatoi shukrani, au badala yake wanatimiza vipindi vya Sala ya Kanisa, hivi kwamba ndani mwao haibaki roho ya ibada ambayo ihuishe liturujia wanazotakiwa kuziongoza. Padri asiyeishi vya kutosha kwa uzima wa Kimungu, atawezaje kuwashirikisha wengine? Atawezaje kuwatimizia mahitaji makubwa ya Kiroho watu ambao wakimuomba msaada wanarudi mikono mitupu na kwa masikitiko? Pengine waamini wenye njaa na kiu ya Mungu, ambao wamejaliwa mengi na kujitoa kati ya matatizo makubwa, wanajibiwa, “Usihangaike! Unafanya kuliko unavyopaswa!” Iko wapi ari ya upendo ya Mwokozi: “Nimekuja kutupa moto duniani, na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?” (Lk 12:49). “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh 10:10). Mtu fulani aliyekuwa akijilaumu kwa kutofikiria vya kutosha mchana juu ya komunyo ya asubuhi, akajibiwa, “Mbona hatufikirii hata mlo tuliopata saa chache zilizopita?” Ndilo jibu la fikra za kidunia zisizoona umbali mkubwa uliopo kati ya mkate wa ekaristi na ule wa kawaida. Jibu hilo linatokeza hali iliyo kinyume cha kuzamia fumbo hilo na inayotokana na uzembe katika kupokea fadhili bora za Mungu. Hayo yanaweza kufikisha mbali, na kusahaulisha kuwa kila Mkristo anatakiwa kulenga upendo kamili; padri na mtawa wanaweza wakasahau wajibu wao wa pekee wa kulenga ukamilifu, ili kutimiza kila siku kitakatifu zaidi huduma yao na kuungana na Bwana zaidi na zaidi. Tukiona muungano na Mungu si jambo la kwanza, hatuelekei tena ukamilifu, hatupimi mambo kwa busara na hekima, bali tunateleza kwa uzembe kwenye mteremko wa upumbavu wa roho. Uzembe katika kushukuru unakuwa uzembe katika kuabudu, kuombea na kufidia. Hivyo tunasahau malengo ya sadaka, na tunafuatilia mambo yasiyo na thamani yasipohuishwa na muungano na Mungu. Uzembe katika kushukuru baada ya komunyo unatokana na kutojua vya kutosha ukuu wa zawadi ya Mungu: “Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, ‘Nipe maji ninywe’…” (Yoh 4:10). Tumuombe kwa unyenyekevu na ari atujalie imani kubwa ambayo tuzamie fumbo hilo kwa vipaji vya akili na hekima: ndio chanzo cha shukrani iliyo motomoto kadiri tunavyojua ukuu wa zawadi tuliyojaliwa.
Bouyer, Louis. Eucharist: Theology and Spirituality of the Eucharistic Prayer, trans. by Charles Underhill Quinn. Notre Dame, Ind.: University of Notre Dame Press, 1968. N.B.: Despite what the subtitle may suggest, the book discusses the Christian Eucharist in further aspects than alone the "Canon of the Mass". ISBN|0-268-00498-6
Chemnitz, Martin. The Lord's Supper. J. A. O. Preus, trans. St. Louis: Concordia, 1979. ISBN|0-570-03275-X
Church, Catholic. "The Canons and Decrees of the Council of Trent" Translated by Rev. H.J. Schroeder, O.P., published by Tan Books and Publishers, Inc., P. O. Box 424, Rockford, IL 61105
Dix, Dom Gregory. The Shape of the Liturgy. London: Continuum International, 2005. ISBN|0-8264-7942-1
Cabrera de Armida, Concepcion. I Am: Eucharistic Meditations on the Gospel, Alba House Publishing 2001 ISBN|0-8189-0890-4
Elert, Werner. Eucharist and Church Fellowship in the First Four Centuries. N. E. Nagel, trans. St. Louis: Concordia Publishing House, 1966. ISBN|0-570-04270-4
Felton, Gayle. This Holy Mystery. Nashville: Discipleship Resources, 2005. ISBN|0-88177-457-X
Father Gabriel. Divine Intimacy. London, UK: Baronius Press Ltd, 2013 reprint ed. ISBN|9781905574438
Grime, J. H. Close Communion and Baptists
Hahn, Scott. The Lamb's Supper: Mass as Heaven on Earth. Darton, Longman, Todd. 1999. ISBN|0-232-52500-5
Henke, Frederick Goodrich A Study in the Psychology of Ritualism. University of Chicago Press 1910
Jurgens, William A. The Faith of the Early Fathers. Collegeville, MN: The Liturgical Press, 1970. ISBN|0-8146-0432-3
Kolb, Robert and Timothy J. Wengert, eds. The Book of Concord: The Confessions of the Evangelical Lutheran Church. Minneapolis: Fortress Press, 2000. (ISBN|0-8006-2740-7)
Lefebvre, Gaspar. The Saint Andrew Daily Missal. Reprint. Great Falls, MT: St. Bonaventure Publications, Inc., 1999
Löhr, Hermut, ed., Abendmahl (Themen der Theologie 3), Tübingen: UTB / Mohr Siebeck 2012. ISBN|978-3-8252-3499-7
Macy, Gary. The Banquet's Wisdom: A Short History of the Theologies of the Lord's Supper. (2005, ISBN|1-878009-50-8)
Magni, JA The Ethnological Background of the Eucharist Archived 26 Septemba 2007 at the Wayback Machine.. Clark University. American Journal of Religious Psychology and Education, IV (No. 1–2), March, 1910.
McBride, Alfred, O. Praem. Celebrating the Mass. Our Sunday Visitor, 1999.
Neal, Gregory. Grace Upon Grace 2000. ISBN|0-9679074-0-3
Nevin, John Williamson. The Mystical Presence: A Vindication of the Reformed or Calvinistic Doctrine of the Holy Eucharist. 1846; Wipf & Stock reprint, 2000. ISBN|1-57910-348-0
Oden, Thomas C. Corrective Love: The Power of Communion Discipline. St. Louis: Concordia Publishing House, 1995. ISBN|0-570-04803-6
Piolanti, Antonio, ed. Eucharistia: il mistero dell'altare nel pensiero e nella vita della Chiesa. Roma: Desclée, 1957.
Rasperger (Raspergero), Christopher (Christophorus, Christoph, Christophoro, Christophe) Two hundred interpretations of the words: This is my Body, Ingolstadt, 1577 Latin text Archived 19 Septemba 2008 at the Wayback Machine.. (Latin title: Ducentae paucorum istorum et quidem clarissimorum Christi verborum: Hoc est Corpus meum; interpretationes,; German title: Zweihundert Auslegungen der Worte das ist mein Leib.)
Sasse, Hermann. This Is My Body: Luther's Contention for the Real Presence in the Sacrament of the Altar. Eugene, OR: Wipf & Stock, 2001. ISBN|1-57910-766-4
Schmemann, Alexander. The Eucharist. St Vladimir's Seminary Press, 1997. ISBN|0-88141-018-7
Scotland, N. A. D. Eucharistic Consecration in the First Four Centuries and Its Implications for Liturgical Reform, in series, Latimer Studies, 31. Oxford, Eng.: Latimer House, 1989. ISBN|0-946307-30-X
Stoffer, Dale R. The Lord's Supper: Believers Church Perspectives
Stookey, L.H. Eucharist: Christ's Feast with the Church. Nashville: Abingdon, 1993. ISBN|0-687-12017-9
Tissot, Very Rev. J. The Interior Life. 1916, pp. 347–9.
Wright, N. T. The Meal Jesus Gave Us
Yarnold, G.D. The Bread Which We Break. London: Oxford University Press, 1960. 119 p.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ekaristi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.