Katerina wa Siena

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Madonda matakatifu ya Katerina wa Siena yalivyochorwa na Domenico Beccafumi, mwaka 1515 hivi

Katerina Benincasa wa Siena (Siena, Italia, 25 Machi 1347 - Roma, Italia, 29 Aprili 1380) alikuwa mwanamke mwenye vipaji na karama za pekee aliyemfuata tangu ujanani Yesu Kristo ili kulingana naye katika familia ya kiroho iliyoanzishwa na Dominiko Guzman, akijitahidi kumfahamu Mungu ndani yake na kujifahamu ndani ya Mungu.

Ingawa hakusoma, alishika nafasi muhimu katika historia ya Kanisa, akisababisha wongofu na urekebisho, na katika historia ya Italia, akileta amani wakati wa vita na fujo nyingi za siasa.

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu bikira na mwalimu wa Kanisa.

Kutokana na umuhimu wake katika historia ya Kanisa na ya jamii ni msimamizi (pamoja na wengine) wa Italia (kwa uamuzi wa Papa Pius XII mwaka 1939) na wa Ulaya (kwa uamuzi wa Papa Yohane Paulo II mwaka 1999).

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 29 Aprili[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto[hariri | hariri chanzo]

Katerina alizaliwa Siena (Italia) kama mtoto wa 24 kati ya 25 wa Jacopo Benincasa na Lapa Piagenti (au Piacenti). Pacha wake Giovanna (kitindamimba) aliishi miezi tu.

Mwaka uliofuata (1348) Siena na Ulaya kwa jumla zilipatwa na tauni iliyopunguza sana idadi ya watu.

Alisimulia kwamba alipokuwa na miaka sita alianza kupata njozi na akiwa na miaka saba aliweka nadhiri ya ubikira akianza safari ya toba yenye saumu na malipizi mengine.

Kwenye umri wa miaka 12 wazazi, wasiojua nadhiri yake, walianza kufikiria wamuoze. Katerina aliitikia kinyume, hata kwa kunyoa kipara na kujifungia nyumbani. Ili kumshurutisha wazazi walimuagiza kazi nzito nyingi, lakini bure. Siku moja baba alimkuta akisali ana njiwa akielea kichwani pake. Hapo alikubali kumuacha huru ajichagulie maisha.

Kujiunga na Wadominiko[hariri | hariri chanzo]

Alipokuwa na miaka 16, baada ya kutokewa na Dominiko Guzman, alijiunga na Utawa wa Tatu wa Mt. Dominiko, ambao wanachama wanawake walijulikana kama “Mantellate” kwa sababu ya kuvaa joho maalumu. Hapo alirudia nadhiri yake ya ubikira na kushika maisha magumu ya sala, malipizi na huduma za huruma, hasa kwa wagonjwa, bila kuhama nyumbani.

Sifa ya kuwa mtakatifu ilienea hata kandokando yake walikusanyika marafiki wengi kama kundi la wanafunzi wake wa kiroho, wakiwemo watu wa kila aina, hata masharifu, wanasiasa na wasanii, mbali ya watawa wa kiume na wa kike.

Hao walimuita “mama” kwa kuwa aliwalisha kiroho kwa mamlaka iliyotokana na ubora wa maisha yake na iliyothibitishwa na majaliwa ya pekee waliyoyashuhudia, kama vile kutoka kwake nje ya nafsi mara nyingi. Naye aliwaelekea kama watoto, akiwaandikia k.mf. mapadri watawa: “Mpendwa sana na wa thamani kwangu ndugu na mwana katika Kristo Yesu mtamu”. “Kwa vile nilikuzaa kwa sala za kudumu na hamu mbele ya Mungu, kama mama anavyozaa mtoto”..

Alijaribu kusoma vitabu vitakatifu bila kufundishwa, mpaka akajaliwa kipawa cha kusoma. Baadaye tena akajaliwa kuandika, lakini maandishi yake mengi aliyaandikisha tu.

Kati yake, muhimu zaidi ni “Maongezi ya Maongozi ya Mungu”. Humo tunakuta mafundisho ya hali ya juu, iliyojaa matunda ya sala yake ya dhati. Pia tuna mikusanyo ya barua na sala zake.

Katika kipindi hicho cha vurugu tele, alisafiri sana na kutuma mara nyingi ujumbe wake wa amani kwa miji na makundi yaliyogombana, akilenga daima upendo na umoja.

Alisimulia kwamba kabla ya Kwaresima ya mwaka 1367 alitokewa na Yesu akiwa pamoja na Bikira Maria na watakatifu wengine ili kumuoa kiimani, akimvika pete yenye rubi aliyoweza kuiona yeye tu.

“Mimi, Muumba na Mwokozi wako, nakuoa katika imani, uweze kubaki safi hata utakapoadhimisha arusi yako ya milele na mimi mbinguni”.

Kwake Kristo alikuwa bwanaarusi ambaye aishi naye kwa umoja na uaminifu wa dhati, naye alimpenda kweli kuliko yeyote na chochote.

Muungano huo unaangazwa na tukio lingine la pekee ambalo Katerina alimshirikisha muungamishi wake: mabadilishano ya mioyo. Yesu alimtokea “akishika katika mikono yake mitakatifu moyo wa mtu mwekundu sana tena angavu”, akafungua kifua cha Katerina na kumtia moyo huo akisema, “Binti mpenzi kabisa, kama vile majuzi nilikuondolea moyo wako, tazama, nakupa wa kwangu uweze kuendelea kuishi nao milele”.

Karama nyingine ya Katerina ilikuwa kutokwa na machozi, yaliyodhihirisha wema wake uliokuwa tayari kuguswa na kuhurumia kama vile Yesu mbele ya kaburi la Lazaro wa Bethania. Kwa maelezo yake, machozi ya watakatifu yamechanganyikana na damu ya Kristo, ambayo aliizungumzia kwa maneno motomoto na mifano miangavu: “Umkumbuke Kristo msulubiwa, Mungu na mtu pamoja… Umlenge Kristo msulubiwa, fichama katika madonda ya Kristo msulubiwa na zama katika damu ya Kristo msulubiwa”.

Kwa ubunifu wa pekee Katerina alimfananisha Yesu na daraja linalounganisha mbingu na dunia ambalo lina ngazi tatu: miguu, ubavu na kinywa cha Yesu. Kupitia ngazi hizo roho inapiga hatua tatu za kuelekea utakatifu: kubandukana na dhambi, kutekeleza maadili na upendo, muungano mtamu wa upendo na Mungu.

Mwishoni mwa sura hiyo, aliandika: “Kwa huruma umetuosha katika damu hiyo, kwa huruma umetamani kuongea na viumbe. Kichaa kwa upendo! Haikukutosha utwae mwili, bali ulitamani kufa pia! Lo, huruma! Moyo wangu unazama katika kukufikiria: kwa sababu kila ninapogeuka niwaze, naona huruma tu”.

Uhusiano na viongozi wa Kanisa na wa siasa[hariri | hariri chanzo]

Katerina hakuogopa watu wakubwa bali aliwaelekea uso kwa uso bila unyonge. Pamoja na kwamba aliheshimu daima mamlaka ya viongozi vya Kanisa, hasa ya Papa, aliyemuita “Kristo mtamu aliyepo duniani”, mwaka 1372 hivi alimueleza balozi wa Papa huko Italia, Pietro d'Estraing, haja ya kurekebisha maadili ya wakleri, ya kumrudisha Papa toka Avignon (watangulizi wake na yeye walipokaa tangu mwaka 1309) hadi Roma na ya kuendesha vita vya msalaba dhidi ya wasioamini.

Pamoja na hayo, ilimbidi ateseke sana, kwa sababu wengi hawakumuamini.

Viongozi wa juu wa Kanisa, wakichukizwa na ushujaa wa mwanamke huyo asiye na elimu, walimuita mwaka 1374 huko Firenze mbele ya mkutano mkuu wa Wadominiko. Shirika lao lilitambua usahihi wa imani yake na kumkabidhi kwa uongozi wa kiroho wa Raimondo wa Capua (1330-1399) padri msomi na mnyenyekevu ambaye baadaye alikuwa wa kwanza kuandika maisha yake.

Inasemekana kuwa tarehe 1 Aprili 1375 huko Pisa alijaliwa madonda matakatifu yasiyoonekana hadi kifo chake.

Baada ya majaribio mengi, hatimaye alifaulu katika juhudi kuu ya maisha yake: tarehe 17 Januari 1377 Papa Gregori XI alihamia Roma bila kujali upinzani wowote.

Mwanzoni mwa mwaka 1378 aliagizwa kupatanisha Ukulu mtakatifu na mji wa Firenze.

Lakini tarehe 20 Septemba wa mwaka huohuo, huko Fondi, lilianza Farakano la Magharibi ambalo lilimsikitisha sana likadumu miaka 40 kwa madhara makubwa.

Alifariki Roma, Italia, tarehe 29 Aprili 1380, akiwa na miaka 33 tu, baada ya kushindwa muda mrefu kula na kunywa chochote isipokuwa Ekaristi kutokana na njozi ya Yesu Kristo aliyemjalia kufyonza damu ubavuni mwake.

Kabla hajafa alisema, “Katika kuhama mwili wangu, kweli nimemaliza na kutoa maisha yangu ndani ya Kanisa na kwa ajili ya Kanisa takatifu”.

Utukufu[hariri | hariri chanzo]

Katerina alitangazwa na Papa Pius II kuwa mtakatifu mwaka 1461. Papa Paulo VI alimtangaza mwalimu wa Kanisa tarehe 4 Oktoba 1970.

Mfano wake unafundisha kwamba urekebisho wa hali iliyopo unatakiwa kuletwa na upendo, si uasi. Upande wa Kanisa unatakiwa kutokana na juhudi ya kutekeleza ufalme wa Mungu na kuelekea utimilifu wake.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Mungu wa milele, Utatu wa milele, umefanya damu ya Kristo iwe azizi kabisa kwa kushiriki umungu wako.

Wewe ni fumbo la kina kuliko bahari; kadiri ninavyotafuta naona; na kadiri ninavyoona nakutafuta.

Siwezi kamwe kushiba; ninachopokea kitanifanya daima nitamani zaidi.

Unapojaza roho yangu nazidi kuonea njaa na shauku mwanga wako.

Hasa natamani kukuona wewe, mwanga halisi, jinsi ulivyo.

Ndiwe muumba wangu, Utatu wa milele, nami ni kiumbe chako.

Umenifanya kiumbe kipya katika damu ya Mwanao, nami najua unavutwa na uzuri wa kiumbe chako kutokana na upendo.


Bwana wangu, elekeza jicho la huruma yako juu ya taifa lako na juu ya mwili wa fumbo wa Kanisa takatifu.

Wewe utatukuzwa zaidi sana kwa kusamehe na kuwaangazia akili wengi, kuliko kwa kupokea heshima toka kwa kiumbe mmoja duni, kama nilivyo mimi, ambaye nilikukosea sana na kuwa sababu na chombo cha maovu mengi.

Ingenitokea nini kama ningeona mimi ni hai, na watu wako wamekufa?

Ingekuwaje kama ningeliona gizani, kutokana na dhambi zangu na za viumbe wengine, Kanisa lako, Bibiarusi wako mpenzi, lililozaliwa liwe mwanga?

Basi, nakuomba huruma kwa taifa lako kwa ajili ya ya upendo usioumbwa uliokusukuma wewe umuumbe mtu kwa sura na mfano wako.

Sababu gani ilikufanya umweke mtu katika heshima kubwa hivyo?

Bila ya shaka ni upendo ule usiothaminika ambao ulimuangalia kiumbe chako ndani mwako ukachanganyikiwa naye.

Lakini baadaye kwa dhambi aliyoitenda akapoteza ukuu huo uliomuinulia.

Ukisukumwa na moto huohuo ambao ulituumba, ulipenda kuwatolea binadamu njia ya kupatanishwa nawe.

Ndiyo sababu umetupatia Neno, Mwanao pekee.

Amekuwa mshenga kati yako na sisi, amekuwa haki yetu aliyeadhibu ndani mwake maovu yetu.

Alitii agizo ambalo wewe, Baba wa milele, ulimpa ulipomvika utu wetu.

Lo, kilindi cha upendo! Moyo upi hautajaa mhemko kwa kuona ukuu huo kushukia unyonge mkubwa kama huu, yaani ubinadamu wetu?

Sisi ni mfano wako, nawe mfano wetu kutokana na muungano uliouanzisha kati yako na binadamu, ukifunika umungu wa milele kwa wingu maskini la utu ulioharibika wa Adamu.

Kwa sababu gani? Bila ya shaka kwa upendo.

Kwa upendo huo usiosemeka nakuomba na kukuhimiza uwawie huruma viumbe wako.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Libro della divina dottrina, c. 1475
  • Maongezi ya Maongozi ya Mungu yaani Kitabu cha mafundisho ya Mungu
  • Barua 381
  • Sala [26/27]

Picha[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

  • Blessed Raymond of Capua, The Life of St. Catherine of Siena, tr. George Lamb (Rockford, Illinois: TAN Books, 2003)
  • Catherine of Siena, The Dialogue, ed. Suzanne Noffke, (Paulist Press, New York, 1980) isbn 0-8091-2233-2
  • Hollister, Warren C. and Bennett, Judith M. Medieval Europe: A Short History, 9th ed., (McGraw-Hill Companies Inc, Boston, 2002)
  • Skårderud, Finn. Holy anorexia: Catherine of Siena, (Tidsskrift for norsk psykologforening, Oslo, 2008)

Matoleo ya baadaye[hariri | hariri chanzo]

  • The Italian critical edition of the Dialogue is Catherine of Siena, Il Dialogo della divina Provvidenza: ovvero Libro della divina dottrina, 2nd ed., ed. Giuliana Cavallini (Siena: Cantagalli, 1995). [1st edn, 1968] [Cavallini demonstrated that the standard division of the Dialogue in into four treatises entitled the 'Treatise on Discretion', 'On Prayer', 'On Providence', and 'On Obedience', was in fact a result of a misreading of the text in the 1579 edition of the Dialogue. Modern editors, including Noffke (1980), have followed Cavallini in rejecting this fourfold division.]
  • The Italian critical edition of the 26 Prayers is Catherine of Siena, Le Orazioni, ed. Giuliana Cavallini (Rome: Cateriniane, 1978)
  • The most recent Italian critical edition of the Letters is Antonio Volpato, ed, Le lettere di Santa Caterina da Siena: l'edizione di Eugenio Duprè Theseider e i nuovi problemi, (2002)

Tafsiri za Kiingereza za Maongezi:

  • In the early fifteenth century, heavily adapted, by an unknown writer. This edition was printed in 1519. It was published, still in its original Middle English, as Phyllis Hodgson and Gabriel M Leigey, eds, The Orcherd of Syon, (London; New York: Oxford UP, 1966).
  • Catherine of Siena, The Dialogue of the seraphic virgin Catherine of Siena, trans Algar Thorold, (London: Kegan Paul, Trench, Trübner & Co, 1896). [This does not contain chapters 135-153.]

Tafsiri za Kiingereza za barua:

  • Catherine of Siena (1988). Suzanne Noffke, ed. The Letters of St. Catherine of Siena 4. Binghamton: Center for Medieval and Early Renaissance Studies, State University of New York at Binghamton. ISBN 0-86698-036-9.  [Republished as The letters of Catherine of Siena, 4 vols, trans Suzanne Noffke, (Tempe, AZ: Arizona Center for Medieval and Renaissance Studies, 2000-2008))

Tafsiri ya Kiingereza za Sala:

  • The Prayers of Catherine of Siena, trans Suzanne Noffke, 2nd edn 1983, (New York, 2001)

Tafsiri ya Kiingereza ya Maisha yaliyoandikwa na Raymond wa Capua:

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

  • Carolyn Muessig, George Ferzoco, Beverly Mayne Kienzle, eds, A companion to Catherine of Siena, (Leiden: Brill, 2012).
  • Hollister, Warren; Judith Bennett (2001). Medieval Europe: A Short History (9 ed.). Boston: McGraw-Hill Companies Inc. p. 343. ISBN 0-07-234657-4. 
  • McDermott,, Thomas, O.P. (2008). Catherine of Siena: spiritual development in her life and teaching. New York: Paulist Press. ISBN 0-8091-4547-2. 
  • Cross, F. L., ed. (1957) The Oxford Dictionary of the Christian Church. Oxford U. P.; p. 251
  • Girolamo Gigli, ed, L'opere di Santa Caterina da Siena, 4 vols, (Siena e Lucca, 1707-1721)
  • The Dialogue of St. Catherine of Siena, TAN Books, 2009. ISBN 978-0-89555-149-8

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]