Isidori wa Sevilia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Isidori wa Sevilia alivyochorwa na Bartolomé Esteban Murillo.
Sanamu ya Isidori huko Madrid (1892), iliyochongwa na J. Alcoverro.

Isidori (Cartagena, leo nchini Hispania, 560 - Sevilia, Hispania, 4 Aprili 636) alikuwa askofu mkuu wa Sevilia, maarufu kwa elimu yake kubwa aliyowarithisha hasa watu wa Ulaya magharibi wa Karne za Kati.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1722 Papa Inosenti XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Ni msimamizi wa mtandao na wa wanafunzi.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Aprili.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa na Severianus na Turtura huko Cartagena (Hispania), akiwa wa nne kati ya watoto watano, ambao wanne kati yao wanaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama watakatifu: Leandro wa Sevilia, Fulgensi, Fiorentina wa Cartagena naye mwenyewe. Kati yao, watatu walikuwa maaskofu, na wa kike alikuwa mtawa.

Kaka yake, Leandro, ndiye aliyemlea baada ya kifo cha baba yao.

Kisha kuwa mkleri huko Sevilia, Isidori alimrithi kaka yake Leandro kama askofu wa jimbo kuu hilo, akaliongoza kwa miaka 40, akijitahidi pande zote: katika teolojia, liturujia, sheria za Kanisa n.k.

Alishika nafasi ya maana katika matukio ya nchi yake wakati huo ilipotawaliwa na kabila la Kijerumani la Wavisigoti, ambao aliwavuta kutoka uzushi wa Ario kwenye imani ya Mtaguso wa kwanza wa Nisea na ya Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli.

Alishiriki Mtaguso IV wa Toledo (633) uliolenga kuunganisha liturujia maalumu ya Kihispania. Ndiye mwakilishi bora wa liturujia hiyo, aliyoirekebisha na kuistawisha.

Alipokaribia kufa, aliamua kupokea kitubio cha hadharani kadiri ya ibada aliyoitunga mwenyewe.

Pia alistawisha elimu yoyote na fasihi kuliko wote wa wakati wake.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Aliandika sana juu ya mambo mbalimbali: sayansi, historia, teolojia, maadili, sheria za Kanisa na ufafanuzi wa Biblia.

Vitabu muhimu zaidi ni vile 20 vya Etymologiae, ambavyo aliviandika hasa kwa ajili ya malezi ya wakleri na vilikusanya ujuzi wote wa wakati ule vikatumika sana katika Karne za Kati.

Hivyo alipata kuwa kiungo kati ya mababu wa Kanisa, ambaye ni wa mwisho wao upande wa magharibi, na hatua iliyofuata.

Tafsiri[hariri | hariri chanzo]

Tafsiri yake ya kwanza kwa Kiingereza ni: Barney, Stephen A., Lewis, W. J., Beach, J. A. and Berghof, Oliver (translators). The Etymologies of Isidore of Seville. Cambridge: Cambridge University Press, 2006. ISBN 0521837499, ISBN 9780521837491.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]