Nenda kwa yaliyomo

Alberto Mkuu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Alberto Mkuu alivyochorwa na Tommaso da Modena mwaka 1352
Alberto Mkuu alivyochorwa na Tommaso da Modena mwaka 1352

Alberto Mkuu (Lauingen, Donau, leo nchini Ujerumani, 1205 hivi - Cologne, Ujerumani, 15 Novemba 1280) ni jina alilopewa kwa heshima askofu Alberto wa Bollstädt (au wa Cologne) kutokana na mchango wake mkubwa upande wa elimu ya kawaida na ile ya dini na vilevile upande wa uchungaji na wa upatanishi wa watu na watawala.

Mtawa huyo wa Shirika la Wahubiri anahesabiwa kuwa mwanafalsafa na mwanateolojia bora wa Ujerumani katika Karne za Kati.

Alijitahidi kulinganisha imani na akili akiingiza falsafa ya Aristotle katika Ukristo, jambo lililoendelezwa na mwanafunzi wake bora, Thoma wa Akwino.

Alitangazwa na Papa Gregori XV kuwa mwenye heri mwaka 1622, na baadaye alitangazwa na Papa Pius XI kuwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa tarehe 16 Desemba 1931.

Mwaka 1941 Papa Pius XII alimtangaza msimamizi wa wanasayansi.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Novemba[1].

De animalibus

Alberto, mtoto mdogo wa mtawala wa Bollstädt, alizaliwa Lauingen (Svevia, Ujerumani) lakini mwaka haujulikani: 1205, 1206 kama si 1193.

Vilevile hakuna hakika kuhusu elimu yake ya msingi, kama aliipata nyumbani au shuleni, lakini ujanani alitumwa kwenye chuo kikuu cha Padova (Italia), maarufu kwa masomo yaliyompendeza zaidi: lugha, hoja, hisabati, falaki na muziki.

Akiwa huko, alikuwa anahudhuria ibada katika kanisa la Wadominiko, ambao utakatifu wa maisha yao ulichangia, pamoja na uhusiano wake wa dhati na Mungu, kumfanya atamani kuwa mmojawao hata akaweza kushinda upinzani wa familia yake.

Mwaka 1223, baada ya kusikia hotuba ya Jordano wa Saksonia, mwalimu mkuu wa pili katika historia ya Shirika la Wahubiri, alijiunga na utawa huo ulioanzishwa na Dominiko Guzman. Jordano mwenyewe alimvika kanzu ya shirika.

Alipomaliza masomo yake, ama Padova ama kwingine, na kupata upadrisho, alitumwa kufundisha katika vituo vya teolojia vilivyounganika na konventi za shirika huko Hildesheim, Freiburg in Brisgau, Regensburg, Strasburg na Cologne mmoja kati ya miji mikuu ya mikoa, ambapo aliishi kwa awamu kadhaa na hatimaye ukawa mji wake.

Akiwa katika konventi ya mji huo, akisoma Liber Sententiarum ya Petro Lombardo mwaka 1245, aliagizwa kwenda Paris (Ufaransa) alipojipatia digrii katika kituo kikuu cha huko, maarufu kuliko vyote upande wa teolojia.

Tangu hapo alianza kazi yake kubwa ya kuandika, mbali ya kutekeleza majukumu makubwa alivyozidi kupewa.

Akiwa safarini alisikilizwa na Thoma wa Akwino, kijana mkimya mwenye kutafakari, ambaye Alberto alitambua ukuu wa akili yake akamtabiri umaarufu wa kimataifa. Kati yao kukawa na heshima na urafiki mkubwa hadi mwisho. Huyo mwanafunzi mpya aliongozana naye hadi Paris halafu (1248) Cologne, ambapo Alberto alikuwa amechaguliwa kuwa gombera wa kwanza, wakati Thoma akawa mwalimu wa pili na Magister Studentium ("mwalimu wa wanafunzi").

Katika mkutano mkuu wa Wadominiko uliofanyika Valenciennes mwaka 1250, pamoja na Thoma na Petro wa Tarentaise, alitunga taratibu za masomo na za stahili shirikani.

Mwaka 1254 alichaguliwa mkuu wa kanda ya Ujerumani, wadhifa mgumu alioshughulikia vizuri sana. Alijitokeza kwa ari yake katika kutembelea jumuia za eneo lake kubwa, lililojumlisha Ulaya Kaskazini na ya Kati, huku akihimiza uaminifu kwa mafundisho na mifano ya Mt. Dominiko.

Mwaka 1256 alikwenda Roma ili kutetea mashirika ya ombaomba dhidi ya mashambulizi ya Wiliamu wa Saint-Amour, ambaye kitabu chake De novissimis temporum periculis hatimaye kililaaniwa na Papa Aleksanda IV tarehe 5 Oktoba 1256.

Akiwa Roma, vipawa vyake viligunduliwa na Papa aliyetaka awe naye ili kufaidika na mashauri yake ya kiteolojia. Hivyo Alberto alishika nafasi ya mwalimu wa nyumba ya Papa na kufafanua Injili ya Yohane.

Mwaka 1257 alijiuzulu kama mkuu wa kanda ili ajitose kusoma na kufundisha.

Mwaka 1260 kwa uamuzi wa Papa huyohuyo, alipewa daraja takatifu ya uaskofu kwa ajili ya Jimbo la Regensburg, ambalo lilikuwa kubwa na maarufu, lakini wakati huo lilipitia matatizo mbalimbali. Basi, aliliongoza kwa bidii isiyokoma, akifaulu kurudisha amani mjini, kupanga upya parokia na nyumba za kitawa pamoja na kuchochea upya huduma za huruma.

Mwaka 1262 alijiuzulu, halafu miaka 1263-1264 alihubiri katika Ujerumani na Ucheki wa leo kwa agizo la Papa Urban IV akarudia kazi ya kufundisha na kuandika huko Cologne.

Kama mtu wa sala, elimu na upendo, aliingilia kwa mafanikio matukio mbalimbali ya Kanisa na jamii: hasa alipatanisha watu wa Cologne na askofu mkuu wao aliyekuwa ameharibu sana.

Mwaka 1270 alimuandikia Thoma, aliyekuwa Paris, ili kumsaidia dhidi ya hoja za Sigieri wa Brabante na wafuasi wa Averroe. Ilikuwa kitabu cha pili dhidi ya huyo mwanafalsafa Mwarabu (cha kwanza kiliandikwa mwaka 1256 kwa jina De Unitate Intellectus Contra Averroem).

Mwaka 1274 aliitwa na Papa Gregori X ashiriki Mtaguso wa pili wa Lyon, ambamo alifanya kazi kubwa ili kurudisha umoja kati ya Kanisa la Kilatini na lile la Kigiriki. Huko alipata taarifa ya kifo cha Thoma akasema, "Mwanga wa Kanisa umezimika".

Alijitokeza tena kwa nguvu mwaka 1277, ilipotangazwa nia ya Etienne Templier, askofu mkuu wa Paris pamoja na wengine ya kulaani maandishi ya Thoma kama yenye uzushi. Ili kumtetea alifunga safari kwenda Paris kuyafafanua.

Mwaka 1278 (alipoandika wasia wake) alianza kusahausahau mambo, na mwili wake uliodhoofishwa na maisha magumu ya kujinyima na ya kazi ulizidi kushindwa na uzee hadi akafa tarehe 15 Novemba 1280 katika chumba chake konventini.

Alizikwa katika kanisa la parokia ya Mt. Andrea ya Cologne.

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vyake vingi vinahusu fani zote za elimu ya wakati ule: mantiki, sayansi mbalimbali, elimunafsia, falsafa, maadili, siasa, teolojia, ufafanuzi wa Biblia n.k. Orodha yake inashangaza kwa upana wa mada alizozikabili kitaalamu. Ndiyo sababu Papa Pius XII alimpangia jina la “Doctor universalis” (yaani Mwalimu wa kila jambo).

Akiwa mtaalamu mkuu wa biolojia wakati wake, aliunganisha vizuri sayansi na ufunuo wa Mungu, falsafa na teolojia. Ulinganifu huo unamfanya awe karibu na watu wa leo katika maswali wanayojiuliza kuhusu asili na maendeleo ya ulimwengu.

Upana wa mawazo yake ulijitokeza hasa katika kuelekeza Kanisa lipokee falsafa ya Aristotle katika ufafanuzi wa ulimwengu, kutokana na hakika ya kwamba kila kinachokubaliwa na akili nyofu kinapatana na imani katika ufunuo wa Mungu. Kwa namna hiyo Alberto aliwezesha falsafa kuwa fani inayojitegemea, ikishirikiana na kuunganika na teolojia katika umoja wa ukweli tu, bila kuchanganyikana.

Yeye alifaulu kushirikisha hata mawazo hayo kwa namna sahili na ya kueleweka, kama alivyofanya katika mahubiri aliyowapa watu wa kila kiwango cha elimu, waliovutiwa na maneno yake na mfano bora wa maisha yake.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • Attwater, Donald and Catherine Rachel John. The Penguin Dictionary of Saints. 3rd edition. New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-14-051312-4.
  • Collins, David J. "Albertus, Magnus or Magus?: Magic, Natural Philosophy, and Religious Reform in the Late Middle Ages." Renaissance Quarterly 63, no. 1 (2010): 1–44.
  • Wallace, William A. (1970). "Albertus Magnus, Saint". In Gillispie, Charles. Dictionary of Scientific Biography. 1. New York: Scribner & American Council of Learned Societies. pp. 99–103. ISBN 9780684101149
      . http://www.u.arizona.edu/~aversa/scholastic/Dictionary%20of%20Scientific%20Biography/Albertus%20Magnus%20(Wallace).pdf. Archived 8 Machi 2021 at the Wayback Machine.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons