Fasihi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Fasihi (kutoka neno la Kiarabu فصاحة, fasaha kwa maana ya ulimbi au "literacy" kwa Kiingereza) ni utanzu (tawi) wa sanaa ambao hutumia lugha ya mazungumzo au maandishi ili kufikisha (kuwasilisha) ujumbe kwa hadhira husika. Ni ufundi wa kuwasilisha mawazo au ujumbe ulio katika fikra za binadamu.Fasihi ni sanaa inayotumia lugha kwa ubunifu kuwasilisha masuala kuhusu maisha ya binadamu na mazingira

Vipengele vinavyounda fani ya fasihi ni kama ifuatavyo: fani ni umbo la nje la kazi ya fasihi; maudhui ni umbo lake la ndani.

Fani

Katika kazi yoyote ya fasihi ni lazima pawepo na ustadi wenye kuleta mvuto fulani kwa hadhira (wasikilizaji au wasomaji) husika. Ustadi (ufundi) huo unaovutia hadhira huitwa fani, ambayo hujumuisha mambo kama vile:

  • Muundo - ni mtitiriko/msuko/mpangilio wa matukio / visa
  • Mtindo - ni mbinu inayotumiwa na fanani ili atofautiane na fanani mwingine
  • Wahusika - ni watu au vitu vyenye uhai au la ambavyo hutumiwa na fanani katika kazi yake
  • Mandhari - ni eneo ambalo fanani hulitumia kujenga matukio na au mtiriko katika kuumba kazi yake au maeneo anayoyatumia fanani kuakisi jamii anayoilenga
  • Matumizi ya lugha - ni lugha anayotumia fanani katika kujenga wasifu wa wahusika kihaiba kazi yake

Maudhui

Pamoja na fani, kazi yoyote ya fasihi huwa na ujumbe na malengo mbalimbali ambayo hukusudiwa yaifikie jamii husika. Yale yote ambayo msanii wa kazi ya fasihi anakusudia yaifikie jamii husika huitwa maudhui. Maudhui ya kazi ya fasihi hujumuisha:

  • Dhamira
  • Ujumbe/Mafunzo
  • Mgogoro
  • Falsafa/msimamo na
  • Mtazamo

Sifa za fasihi

  • Fasihi ni utanzu wa sanaa. Kuna aina tatu za sanaa: sanaa za ghibu, sanaa za maonyesho na sanaa za vitendo.
  • Kazi ya fasihi ni kujaribu kusawiri vipengele vya maisha, mahusiano, na hisia za watu katika jamii husika.
  • Fasihi ni maelezo ya fani na maudhui.
  • Fasihi ni ufundi unaotumia lugha ili kulete mguso au hisia fulani za watu katika muktadha fulani.

Dhima za fasihi katika jamii

Fasihi hufanya kazi mbalimbali katika maisha:

  • Kuelimisha jamii - Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mbalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.
  • Kukuza utamaduni - Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.
  • Kustawisha lugha- Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.
  • Kuburudisha jamii - Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.
  • Kukomboa jamii.
  • Kuonya jamii - Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
  • Kukuza uwezo wa kufikiri-Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.
  • Kuhifadhi historia ya jamii.

Aina za fasihi

Fasihi ndiyo aina pekee ya sanaa inayotumia lugha kujitambulisha au kujitofautisha na aina nyingine za sanaa. Kuna aina kuu mbili za fasihi nazo ni:

Fasihi hizi zina dhima sawa katika jamii ingawa ni tofauti. Utofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi hujitokeza katika uwasilishwa wake katika jamii husika.

    • Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya lugha ya mazungumzo au masimulizi ya mdomo
    • Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya lugha ya maandishi

Fasihi simulizi

Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mazungumzo ya mdomo ili kufikisha ujumbe kwa hadhira. Aina hii ya fasihi ndiyo iliyokuwapo tangu zamani kabisa mwanadamu alipoanza kuishi yaani ilianza pale mwanadamu alipochangamana na wenzake katika kufanya mambo mbalimbali mfano,shughuli za biashara,kilimo,na nyinginezo.

kuna tanzu nne za fasihi simulizi .ie;

  • 1.utanzu wa hadithi
  • 2.utanzu wa semi
  • 3.utanzu wa ushairi simulizi
  • 4.utanzu wa maigizo
  • 5.utanzu wa mazungumzo

Sifa za fasihi simulizi

  • Hutolewa kwa njia ya mdomo.
  • Haitumii gharama
  • Huonyesha uhalisia wa hisia za mzungumzaji
  • Ni mali ya jamii. Hakuna mtu anayeimiliki.

Dhima za fasihi simulizi

  • kuburudisha
  • kuelimisha jamii
  • kunasihi
  • kukuza lugha
  • kuunganisha watu

Kufanana kwa fasihi simulizi na fasihi andishi

Kimsingi fasihi ni moja ingawa imegawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani, fasihi simulizi na fasihi andishi. Mbali na mgawanyiko huo kuna mambo ambayo yanafanana katika fasihi zote mbili. Mambo hayo ni pamoja na:

  • Zote hutumia ufundi wa lugha ili kuwasilisha ujumbe kwa hadhira husika
  • Zote zina dhima inayofanana katika jamii, yaani, kuelimisha na kuburudisha jamii
  • Zote zina wahusika ambao ni Fanani na Hadhira
  • Zote zina vipengele vya Fani na Maudhui
  • zote zinaweza kukashifiwa na wasanii mbalimbali ikiwa hawajaridhishwa na mbinu za lugha zilizotumika

Tofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi

Na. Kipengele Fasihi simulizi Fasihi andishi
1 Uwasilishwaji Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo pamoja na vitendo Fasihi andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi bila vitendo
2 Umri Fasihi simulizi ni kongwe kuliko fasihi andishi Fasihi andishi ni changa kuliko fasihi simulizi
3 Umilikaji Fasihi simulizi humilikiwa na jamii nzima, ni mali ya jamii Fasihi andishi humilikiwa na mwandishi, ni mali ya mwandishi
4 Tanzu Fasihi simulizi ina tanzu nyingi kuliko fasihi andishi Fasihi andishi ina tanzu chache kuliko fasihi simulizi
5 Hadhira hadhira ina uhusiano wa moja kwa moja na fanani yaani kuna hadhira hai hadhira inayoshirika haina uhusiano wa moja kwa moja na fanani
6 Mabadiliko Fasihi simulizi hubadilika haraka kutegemeana na mahitaji ya hadhira na wakati Fasihi andishi haibadiliki haraka kutegemeana na mahitaji ya hadhira na wakati
7 Utunzi Fasihi simulizi hutungwa kwa muda mfupi Fasihi andishi hutungwa kwa muda mrefu
8 Mazingira ya uwasilishaji wake (mandhari) Huambatana na tukio maalumu la jamii Kusoma au kusomewa ni ya kufikirika au mahali popote
9 Marekebisho Mtunzi/msimulizi anaweza kurekebisha kazi yake wakati wa kuwasilisha au baadaye kidogo Kitabu kikishaandikwa ni vigumu kukifanyia marekebisho mpaka toleo jipya litakapoandikwa
10 Uhifadhi Huhidhiwa kwa njia ya kichwa (kichwani) kwa sehemu kubwa na sehemu ndogo sana huhifadhiwa kwenye maandishi, vinasa sauti au kanda mbalimbali za kurekodi Huhifadhiwa kwa njia ya maandishi (vitabu)
11 Gharama Fasihi simulizi ina gharama ndogo ukilinganisha na fasihi andishi Fasihi andishi ina gharama kubwa ukilinganisha na fasihi simulizi
12 Wahusika Fasihi simulizi mara nyingi hutumia wahusika wa kubuni wasio binadamu Fasihi andishi hutumia wahusika wa kubuni ambao mara nyingi ni binadamu
13 Uhai Fasihi simulizi ni hai kuliko fasihi andishi Fasihi andishi si hai kuliko fasihi simulizi

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Fasihi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.