Maudhui

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.

  1. Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
  2. Migogoro; hii ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
  3. Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
  4. Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
  5. Falsafa ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.
  6. Mtazamo ni hisia au uelewa wa mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au kisayansi.
  7. Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]