Peter Damian

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Petro Damiani amechorwa chini kulia.

Petro Damiani (Ravenna, Italia, 1007Faenza, Italia, 21 Februari 1072) alikuwa mmonaki wa urekebisho wa Wabenedikto wa Camaldoli nchini Italia.

Kutokana na juhudi zake kwa urekebisho, alifanywa kardinali askofu wa Kanisa Katoliki.

Tangu zamani ametambuliwa kuwa mtakatifu.

Mwaka 1828 Papa Leo XII alimuongezea sifa Ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka ni tarehe 21 Februari.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto na ujana (1007-1022)[hariri | hariri chanzo]

Petro Damiani alizaliwa mwaka 1007 mjini Ravenna nchini Italia katika familia ambayo iliwahi kuwa maarufu, lakini baadaye ikawa na hali duni kidogo.

Alikuwa wa mwisho kati ya ndugu 7: mkubwa wao aliiitwa Damian, ambaye baadaye akawa padri na mmonaki.

Alibaki yatima mapema, akalelewa na wakubwa wake, hasa Damian. Kama shukrani kwake akajiongezea jina la Damiani.

Masomo (1022-1032)[hariri | hariri chanzo]

Damian alijitahidi kumsomesha mdogo wake huko Ravenna, halafu Faenza, alipobaki tangu mwaka 1022 hadi 1025. Baadaye Petro alihamia Parma ili kusoma lugha na sayansi za jamii (1026-1032).

Ualimu (1032-1035)[hariri | hariri chanzo]

Kisha kuhitimu masomo yake alirudi Ravenna akafundisha kwa miaka mitatu, iliyotosha kumpatia umaarufu, wanafunzi wengi na pesa. Inawezekana kwamba kwa wakati huo amekwishaingia ukleri kwa daraja ndogo au hata ushemasi. Upadrisho alipewa na askofu mkuu Gebeardo wa Eichstätt (1027-1044).

Wito wa kimonaki (1035)[hariri | hariri chanzo]

Wakati alipoendelea na ualimu, alizidi kuvutiwa na umonaki akaanza kutimiza desturi kadhaa za kitawa (kukesha, kufunga n.k.).

Uamuzi wa kubadili maisha ulifikiwa alipotambua anajipendea bado kwa sababu akiwa mezani na kipofu alimpa mkate wa kifukara kuliko ule aliojipatia.

Basi, baada ya kukutana na wakaapweke wawili wa Fonte Avellana, palipokuwepo monasteri iliyoanzishwa na mtakatifu Romwald, akawafuata aishi upwekeni huko, kulipokuwa na hali ngumu kabisa, lakini baadaye alipaswa kwenda kuhubiria watu na kurekebisha monasteri mbalimbali. Ili aweze kurekebisha wengine, hakuacha kujirekebisha kwa maisha ya uadilifu.

Mmonaki huko Fonte Avellana (1035-1043)[hariri | hariri chanzo]

Monasteri ya Fonte Avellana.

Huko Fonte Avellana, aliombwa awafundishe na kuwalea Wakamaldoli wenzake, kazi aliyoendelea nayo hata katika Abasia ya Pomposa (1040 - 1042).

Mwaka 1042 priori wa Fonte Avellana alimtuma kurekebisha monasteri ya Mt. Vinsenti huko Furlo (karibu na Urbino), ambako aliandika maisha ya mtakatifu Romwald.

Priori wa Fonte Avellana (1043-1057)[hariri | hariri chanzo]

Mwishoni mwa mwaka 1043 alirudi Fonte Avellana, akachaguliwa kuwa priori wa jumuiya hiyo yenye wamonaki 20 hivi, kazi aliyoifanya kwa miaka 14, akihimiza uzingatifu wa upweke hapo na katika sehemu nyingine za Italia.

Wakati huo mgumu aliwasaidia mapapa wa Roma kwa maandishi yake, na pia alisaidia katika kulirekebisha Kanisa pamoja na mmonaki mwingine, Ildebrando wa Soana (ambaye baadaye akawa Papa Gregori VII).

Kwa ajili hiyo alitembelea majimbo mbalimbali ya Italia akionya maaskofu na hata kumfanya Papa awaondoe madarakani baadhi yao.

Alikwenda pia Ujerumani mara kadhaa kama mgeni wa kaisari.

Alihudhuria sinodi za Roma za miaka 1047, 1049, 1050, 1051 na 1053 kuhusu dhambi ya usimoni, akafaulu hasa kwa kupitisha sheria ya kuwa Papa achaguliwe na makardinali tu, bila kuingiliwa na viongozi wa siasa wala watu wengine.

Mwaka 1049 aliandika Liber gomorrhianus kuhusu aina za uasherati dhidi ya maumbile.

Chini ya Papa Leo IX (1049-1054) na waandamizi wake Papa Stefano IX, Papa Nikolasi II na Papa Aleksanda II upana wa juhudi zake uliongezeka tena, akafanywa pia priori wa Ocri.

Askofu wa Ostia na mshauri wa Papa (kuanzia 1057)[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1057 au 1058 alifanywa na Papa Stefano IX kuwa kardinali askofu wa Ostia awe mshauri wake wa karibu kabisa (alipewa uaskofu mwaka 1058).

Petro Damiani hakufurahia uteuzi huo, kwa jinsi alivyojisikia wito wa kuishi upwekeni, lakini akatii na kuhamia Roma.

Mrekebishaji[hariri | hariri chanzo]

Akitumwa na Papa sehemu mbalimbali za Italia na Ufaransa, Petro Damiani alistawisha urekebisho hasa kwa:

 • kupambana na serikali zilizojiingiza katika uteuzi wa viongozi wa Kanisa hasa kwa njia ya rushwa;
 • kusisitiza mamlaka ya juu ya Papa, kiini cha miundo ya Kanisa;
 • kurudisha elimu na maadili katika maisha ya mapadri, akiwaelekeza kufuata mifano ya wamonaki.

Kurudia monasterini na miaka ya mwisho[hariri | hariri chanzo]

Petro Damiani alimuomba mara kadhaa Papa amruhusu kurudi upwekeni.

Baada ya miaka 10 alikubaliwa arudi Fonte Avellana 1067 na kuacha vyeo vyake vyote.

Kumbe miaka miwili baadaye akatumwa tena Ujerumani (1069)

Mwaka 1071 alikwenda Montecassino ili kutabaruku kanisa la abasia hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka uliofuata alianza kurudi Ravenna ili kuleta amani ndani ya Kanisa. Akiwa njiani alifariki usiku kati ya tarehe 21 na 22 Februari 1072 karibu na Faenza.

Mara baada ya kifo chake alianza kuheshimiwa kama mtakatifu.

Mafundisho[hariri | hariri chanzo]

Aliandika vitabu muhimu kuhusu liturujia, teolojia na maadilidini, vilivyoenea sana. Ndiye mwandishi bora wa karne XI. Kwa ajili hiyo na kwa mchango wake katika urekebisho wa Kanisa, Papa Leo XII alimtangaza mwalimu wa Kanisa mwaka 1828.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

 • Vita beati Romualdi
 • Liber Gratissimus
 • Disceptatio Synodalis
 • Liber Gomorrhianus
 • De sancta simplicitate
 • De divina omnipotentia
 • Dominus vobiscum

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

 • Berger, David, "St. Peter Damian. His Attitude Toward the Jews and the Old Testament," The Yavneh Review, 4 (1965) 80-112.
 • Owen J. Blum, "The Monitor of the Popes: St. Peter Damian," in Studi Gregoriani vol. 2 (1947), pp 459–76.
 • John Boswell, Christianity, Social Tolerance, and Homosexuality Chicago (1980).
 • Pierre J. Payer, 1962. Book of Gomorrah : An Eleventh-Century Treatise against Clerical Homosexual Practices, Waterloo, Ontario: Wilfrid Laurier University Press.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]