Bonaventura wa Bagnoregio

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Bonaventura alivyochorwa na Francisco de Zurbarán

Mtakatifu Bonaventura (Bagnoregio, Italia, 1221 hivi – Lyon, Ufaransa, 15 Julai 1274) alikuwa mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo, halafu padri, askofu na kardinali.

Kisha kufa alitangazwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa na Kanisa Katoliki kila mwaka tarehe 15 Julai.

Maisha yake kabla ya kuwa mtumishi mkuu wa shirika[hariri | hariri chanzo]

Mwaka aliozaliwa haujulikani kwa hakika, bali ni kati ya 1217 na 1221. Mahali ni Civita di Bagnoregio, karibu na Viterbo.

Wazazi wake walikuwa mganga Yohane Fidanza na Maria wa Ritello; kwanza aliitwa kwa jina la baba yake, lakini alipoingia utawani aliitwa Bonaventura (yaani Bahati njema). Inasemekana jina hilo lilikuwa shangilio la Fransisko wa Asizi akimuona bado mtoto kabla hajamponya kimuujiza ulemavu wake.

Alisoma (1235-1253) akafundisha (1253-1257) katika chuo kikuu cha Paris (Ufaransa), akifuata falsafa ya Plato na teolojia ya Agostino wa Hippo.

Mtumishi mkuu wa shirika lake, Yohane wa Parma (1247-1257), alipoamua kujiuzulu, ingawa Mkutano mkuu ulitaka aendelee, hakurudi nyuma. Hatimaye walimuomba walau amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Bonaventura, mtu wa Mungu na wa watu, mwema kwa wote na mwenye kipawa cha uongozi.

Akiwa mtumishi mkuu wa shirika[hariri | hariri chanzo]

Kwa miaka 17 (1257-1274) alikuwa Mtumishi mkuu wa shirika, akijitahidi kulinganisha misimamo tofauti ya watawa walioelekea zaidi sala na ufukara na ya wale walioelekea zaidi elimu na utume. Chini yake mkutano mkuu wa Narbone ulitunga katiba maarufu (1260).

Kufuatana na tabia yake chanya, alikubali hali ya shirika ilivyo na kujitahidi kuliepusha na hatari za nje na za ndani alizoziona mapema kabla hajachaguliwa.

Upinzani wa Maaskofu na maparoko dhidi ya Ndugu Wadogo ulikuwa umeungwa mkono na chuo kikuu cha Paris: hapo hazikupingwa tu ruhusa kadhaa walizopewa, bali msingi wenyewe wa mtindo wa maisha wao na wa Wadominiko. Baada ya Bonaventura na Thoma wa Akwino kuutetea, Papa alilaani upinzani na kusifu sana mtindo huo wa Kiinjili. Mwalimu huyo kuchaguliwa kuwa Mtumishi mkuu kukawa ushindi mwingine mkubwa chuoni.

Mashambulizi ya kutisha zaidi yalitokea ndani, upande wa ndugu “wa Kiroho”. Bonaventura alijipangia kulinganisha uaminifu kwa kanuni na mabadiliko shirikani, akionyesha hayo hayaendi kinyume cha nia ya mwanzilishi. Kwa ajili hiyo ilimpasa kuziondolea lawama za ndugu hao msingi wowote kwa kupigania uaminifu kwa wito wa shirika. Mwenyewe alikubali kwa moyo matamko ya Mapapa juu ya kanuni kama ufafanuzi rasmi wa wachungaji wakuu wa Kanisa na wa shirika pia.

Kielelezo cha Fransisko wa Asizi kilitakiwa kuzingatiwa na wote kwa umoja, bila kupishana kuhusu namna ya kukitazama. Kwa ajili hiyo alitunga kitabu rasmi cha maisha yake kilichopitishwa na mkutano mkuu hata ukaagiza maandishi yote yaliyotangulia juu ya Fransisko yateketezwe. Ndivyo shirika lilivyopotewa kwa muda mrefu na habari nyingi muhimu juu ya mwanzilishi. Bila kusema uongo, kitabu alichokiandika kinaleta baadhi tu ya matendo na mafundisho ya Fransisko yaliyochaguliwa kwa makini ili kumchora kama mfano kamili wa Yesu msulubiwa na kusisitiza mang’amuzi yake bora ya kiroho, lakini kwa kuficha mambo fulanifulani kuhusu kipeo cha udogo.

Aliheshimu ufukara kama sifa kuu na utukufu wa shirika, ingawa alikubali mabadiliko yaliyotokea, yaani konventi kubwa mijini n.k. Kwake elimu pamoja na utume ni sehemu ya lazima ya utendaji wa Kifransisko. Kwa ajili hiyo alikubali ruhusa lilizopewa shirika, ingawa kwa udogo alipenda kupatana na Maaskofu na maparoko.

Basi, chini ya uongozi wake shirika likatulia, kwa jinsi alivyoweza kulinganisha upendo kwa Fransisko na furaha kwa mabadiliko, hamu ya kuishi upwekeni muda mrefu pamoja na ndugu “wa Kiroho” na utetezi wa konventi za mijini.

Akiwa kardinali askofu[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuteuliwa kardinali mnamo Mei 1273, akiwa askofu wa Albano Laziale, aliandaa Mtaguso wa pili wa Lyon ulioanza mwaka 1254 hasa kwa lengo la kurudisha umoja kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi, lakini katikati yake akafa na muungano uliofikiwa ukaja kuvunjika tena.

Kutukuzwa kwake baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1434 walipohamisha masalia yake, walikuta kichwa hakijaoza. Jambo hilo liliharakisha hatua ya kumtangaza mtakatifu iliyochukuliwa na Papa Sixtus IV tarehe 14 Aprili 1482.

Halafu tarehe 14 Mei 1588 akatangazwa na Papa Sixtus V kuwa mwalimu wa Kanisa kwa jina la Doctor Seraphicus, yaani Mwalimu wa Kiserafi. Hilo lilitokana na umotomoto wa upendo uliokuwa tunda la maisha yake ya sala ya dhati na unaojitokeza katika maandishi yake mengi.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Lo, uzuri usiosemeka wa Mungu mkuu, lo, mng’ao safi kabisa wa nuru ya milele!

Wewe ni uhai unaohuisha kila uhai, mwanga unaoangaza kila mwanga!


Bwana Yesu Kristo, unichome mpaka kiini cha moyo wangu kwa donda lile tamu la kuletea wokovu la upendo wako.

Unijaze kwa ule upendo motomoto, mnyofu na mtulivu uliomfanya mtume wako mtakatifu Paulo atamani kutengwa na mwili wake awe nawe.

Roho yangu ikuonee shauku, ikijaa daima hamu ya makao yako ya milele.

Vitabu alivyoandika[hariri | hariri chanzo]

 • Breviloquium
 • Collationes de decem praeceptis
 • Collationes de septem donis Spiritus Sanctis
 • Collationes in Hexaemeron
 • Commentaria in quattuor libros sententiarum Magistri Petri Lombardi
 • De mysterio Trinitatis
 • De perfectione vitae ad sorores
 • De reductione artium ad theologiam
 • De Regno Dei descripto in parabolis evangelicis
 • De scientia Christi et mysterio Trinitatis
 • De sex alis Seraphin
 • De triplici via
 • Itineriarium mentis in Deum
 • Legenda Sancti Francisci
 • Lignum vitae
 • Officium de passione Domini
 • Quaestiones de perfectione evangelica
 • Soliloquium
 • Summa theologiae
 • Vitis mystica

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]