Utatu
Utatu au Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili.
Jina hilo la kiteolojia linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, sahili kabisa, ni Nafsi tatu zisizotenganika kamwe: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Katika Biblia
[hariri | hariri chanzo]Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo 28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu.
Ufafanuzi wa teolojia
[hariri | hariri chanzo]Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa milele Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao[1].
Kimsingi ni kwamba Mungu pekee (Baba) anajifahamu milele (Mwana) na kwa kujifahamu anajipenda (Roho Mtakatifu).
Katika matamko rasmi ya Kanisa
[hariri | hariri chanzo]Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha umungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli inayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.
Kwa imani hiyo tunapaswa kusadiki hasa Utatu wa Mungu pekee, kwamba ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Milele yote Baba kwa jinsi alivyo ndani mwake anamzaa Mwana na kumvuvia Roho Mtakatifu, kama vile jua linavyotoa mwanga na joto lisitenganike navyo. Mwana, ambaye “ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake” (Eb 1:3), alisema: “Nimekuja kutupa moto duniani” (Lk 12:49). Naye Roho aliwashukia wafuasi wake “kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:3-4).
Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umoja kamili. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk 12:29). Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine. “Mimi na Baba tu umoja” (Yoh 10:30).
Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu. “Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17). Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.
Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu. “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).
Nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo. Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji. “Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).
Katika liturujia
[hariri | hariri chanzo]Fumbo hilo linaadhimishwa katika liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa mashariki (siku ya Pentekoste) na ya Ukristo wa magharibi (Jumapili inayofuata).
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Pontifical Council for Promoting Christian Unity: The Greek and the Latin Traditions regarding the Procession of the Holy Spirit Archived 3 Septemba 2004 at the Wayback Machine. and same document on another site
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Emery, Gilles, O.P.; Levering, Matthew, whr. (2012). The Oxford Handbook of the Trinity. ISBN 978-0199557813.
{{cite book}}
: CS1 maint: multiple names: editors list (link) - Fiddes, Paul, Participating in God : a pastoral doctrine of the Trinity (London: Darton, Longman, & Todd, 2000).
- Harris, B.P. (2006). Understanding the Trinity. An Encouragement to Abide in the Doctrine in Both Faith and Practice (PDF).
- Holmes, Stephen R. (2012). The Quest for the Trinity: The Doctrine of God in Scripture, History and Modernity. ISBN 9780830839865.
- Johnson, Thomas K., "What Difference Does the Trinity Make?" (Bonn: Culture and Science Publ., 2009).
- La Due, William J., The Trinity guide to the Trinity (Continuum International Publishing Group, 2003 ISBN 1-56338-395-0, ISBN 978-1-56338-395-3).
- Letham, Robert (2004). The Holy Trinity : In Scripture, History, Theology, and Worship. ISBN 9780875520001.
- O'Collins, Gerald (1999). The Tripersonal God: Understanding and Interpreting the Trinity. ISBN 9780809138876.
- Olson, Roger E.; Hall, Christopher A. (2002). The Trinity. ISBN 9780802848277.
- Phan, Peter C., mhr. (2011). The Cambridge Companion to the Trinity. ISBN 978-0-521-87739-8.
- So, Damon W. K., Jesus' Revelation of His Father: A Narrative-Conceptual Study of the Trinity with Special Reference to Karl Barth. Ilihifadhiwa 14 Oktoba 2012 kwenye Wayback Machine. (Milton Keynes: Paternoster, 2006). ISBN 1-84227-323-X.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Trinity Entry at the Stanford Encyclopedia of Philosophy
- Doctrine of the Trinity Ilihifadhiwa 23 Julai 2010 kwenye Wayback Machine.
- Trinity Article at Theopedia
- Eastern Orthodox Trinitarian Theology Ilihifadhiwa 26 Juni 2010 kwenye Wayback Machine.
- Doctrine of the Trinity Reading Room Ilihifadhiwa 19 Juni 2013 kwenye Wayback Machine.: Extensive collection of on-line sources on the Trinity (Tyndale Seminary)
- All About Trinity Sunday
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Utatu kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |