Sanaa ya Kikristo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bikira Maria na Mtoto Yesu walivyochorwa na Wakristo wa karne ya 4 katika mahandaki ya Roma, walipokutana kusali. Mapema sana walianza kupamba makaburi ya humo kwa michoro ya Kristo, ya watakatifu, ya matukio ya Biblia n.k. Hivyo mahandaki ndiyo vitovu vya sanaa ya Kikristo.


Sanaa ya Kikristo ni sanaa iliyokusudiwa kutokeza imani ya Ukristo katika uzuri wake. Mara nyingi hiyo inafanyika kuhusiana na ibada na majengo yanayotumika kwa ajili hiyo.

Kwa ajili hiyo inatumia mada na mifano ya Injili au vitabu vitakatifu vingine, lakini pia habari za maisha ya watakatifu.

Madhehebu karibu yote yanatumia sanaa za aina fulani kwa namna hiyo, ingawa mengine yanakataa uchoraji n.k.

Picha za Yesu ndiyo michoro ya kawaida zaidi, zikifuatwa na zile za Bikira Maria katika Kanisa Katoliki na yale ya Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki.

Karibu kila mtu ana dhana fulani kuhusu muonekano wa Yesu Kristo. Ndiye mtu aliyechorwa zaidi katika sanaa ya Magharibi. Picha zake hutambuliwa kwa urahisi, ambapo huoneshwa akiwa na nywele ndefu na ndevu, akiwa amevalia vazi refu lenye mikono mirefu linalofanana na kanzu (hasa la rangi nyeupe), na pia akiwa amejifunga joho (hasa la rangi ya samawati).

Muonekano wa Yesu umefahamika sana na wengi kiasi kwamba unaweza kutambuliwa ukiwa hata kwenye mikate au biskuti.

Picha za sasa za Yesu zinatokana na enzi ya Byzanti, himaya iliyokuwa na mji mkuu wake Constantinople. Ni picha iliyoanza kutumika karne ya 4 hivi. Michoro ya Yesu ya wakati wa utawala wa Byzanti ilikuwa ya ishara, na si muonekano halisi. Wasanii waliangazia zaidi maana na si kumfananisha na Yesu mwenyewe.

Picha zao ziliongozwa na dhana ya Yesu kama mtawala, kwenye kiti cha enzi, kama anavyoonyeshwa kwenye mchoro ulio kwenye altari ya kanisa la Santa Pudenziana jijini Roma.

Duara ya nuru kichwani inatokana na sanaa ya zama zile - zamani ilitumiwa katika michoro ya mungu wa jua (Apollo, au Sol Invictus) lakini iliongezwa kwenye kichwa cha Yesu kuonesha utakatifu na utukufu wake

Yesu anaoneshwa akiwa amevalia mgolole wa rangi ya dhahabu.

Kutokana na kujali na kustawisha aina zote za sanaa, Wakatoliki wameshika nafasi ya kwanza katika idadi ya vituo vilivyoorodheshwa na UNESCO kama Urithi wa Dunia. Kwa mfano, nchi nzima ya Vatikani imo katika orodha hiyo.

Wakatoliki katika Mtaguso II wa Vatikano (hati Sacrosanctum Concilium) walikiri kwamba muziki wa Kikristo ndio sanaa bora kuliko zote kwa sababu unahusiana zaidi na Neno la Mungu ambalo unalipamba kwa noti ili lieleweke na kugusa mioyo zaidi.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Sanaa ya Kikristo kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.