Uchoraji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Uchoraji kwenye mwamba kwenye mapango karibu na Kondoa (Tanzania)

Uchoraji ni sanaa ya kupaka rangi kwenye uso wa karatasi, kitambaa, ubao, metali, mwamba au penginepo. Tokeo la uchoraji huitwa picha.

Ni sanaa wakilishi inayotumika kuwakilisha ujumbe kwa jamii, kuna aina tofauti za uchoraji.

Hii inategemea na mchoraji mwenyewe anapenda aina gani ya uchoraji, pia wakati mwingine sanaa hii ya uchoraji si kuwakilisha ujumbe tu pia kumvutia mtamzamaji kwa rangi za kupendeza bila kujali ujumbe uliobebwa na picha hiyo, au wakati mwingine inawezekana picha isiwe na ujumbe kabisa lakini ikawa imechorwa kwa ustadi mkubwa na kupakwa rangi za kuvutia sana.

Uchoraji wa Misri ya Kale (Kaburi la Nakht)

Historia[hariri | hariri chanzo]

Picha za kale kabisa zinaonyesha uchoraji kwenye miamba katika mapango. Katika Afrika ni Wasan au watu waliokuwa karibu nao waliochora wanyama kwenye kuta za mipango walipopumzika. Picha zao zinapatikana kote katika Afrika ya Kusini hadi Tanzania ambako kuna mifano mbalimbali karibu na Kondoa. Mifano ya uchoraji wa aina hii imepatikana pia Ulaya, Asia na Australia.

Hatujui mengi kuhusu namna nyingine za uchoraji wa kale kwa sababu vifaa vingine vilivyotumiwa havikudumu.

Kutoka tamaduni ya juu kama Misri, bonde la Indus au China tunajua mifano mingine ya uchoraji inayoonyesha hali ya juu zaidi. Katika ustaarabu wa madola ya kwanza wachoraji walikuwa tayari watu waliokuwa na nafasi ya kufuata sanaa yao bila haja ya kuwinda au kulima wenyewe kwa sababu mtu mkubwa kama mfalme au kuhani aliwapa ridhiki ya maisha.

Katika makaburi ya Nubia,Ufalume wa Kush kuna picha zilizohifadhiwa ukutani. Makaburi ya Wamisri yalijengwa mara nyingi kwenye jangwa kando la bonde la Naili. Ukavu wa mazingira pamoja na giza ulitunza rangi vema. Wamisri wa Kale walichora watu bila kutofautisha mandharimbele au mandharinyuma. Wati muhimu waliochorwa wakubwa kuliko wale waliokuwa na cheo kidogo. Mwili ulionyeshwa mara nyingi kwa mbele lakini kichwa na uso kwa kando.

Katika Ugiriki ya Kale uchoraji na wasanii wake uliheshimiwa sana. Philostrates aliandika mnamo mwaka 300 KK ya kwamba uchoraji ulibuniwa na miungu. Kuna taarifa juu ya picha lakini ni machache tu yaliyohifadhiwa kwa sababu ya hali ya hewa na kwa sababu picha nyingi zilichorwa juu ya ubao au matofali.

Waroma wa Kale walituachia mifano mingi ya uchoraji wa ukutani; nje ya makaburi ni hasa nyumba za miji Pompei na Herkulaneo zilizofunikwa na majivu ya volkeno Vesuvio ambako picha nzuri zimehifadhiwa tangu mwaka 79 BK. Wakati ule wasanii walitofautisha tayari kati ya mandharimbele na mandharinyuma.

Uchoraji wa China uliendelea sana kufuatana na utamaduni wake; mnamo mwaka 600 kuna picha za mandhari zinazoonyesha nchi na milima; msanii wa kwanza anayejulikana alitumia mbinu huu alikuwa Zhan Ziqian.

Blank template.svg Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uchoraji kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.