Volkeno

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Volkeno

Volkeno (pia: volkano) ni mahali ambako zaha inatoka nje kwa uso wa ardhi. Mara nyingi -lakini si kila mahali- volkeno ni mlima. Volkeno huwa na kasoko yaani shimo ambako zaha na gesi inatoka nje.

Asili ya jina[hariri | hariri chanzo]

Asili ya jina ni mungu wa imani ya Roma ya Kale aliyeitwa "Vulcanus". Kati ya miungu ya Kiroma alihusika na moto, radi na uhunzi; kwa hiyo aliheshimiwa hasa na wote waliotumia moto kwa kuyeyusha metali kama chuma au shaba.

Volkeno na ganda la dunia[hariri | hariri chanzo]

Volkeno ni dalili ya kwamba mahali pake ganda la dunia si nene sana hivyo joto la ndani linapata njia ya kutoka nje. Volkeno huanza katika tambarare. Zaha hutoka katika hali ya kiowevu ikipoa haraka inaganda kuwa mwamba na hujenga mlima wa kuzunguka shimo la kasoko yake. Milima ya aina hii inaweza kukua sana. Mfano wa volkeno kubwa ni Kilimanjaro. Miamba yake yote ilijengwa na zaha iliyotoka ndani ya dunia.

Volkeno nyingi hutokea pale ambako mabamba ya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Hivyo volkeno hutokea hasa kwenye mistari ya kukutana kwa mabamba haya.

Sababu nyingine ya kutokea kwa volkeno ni kuwepo kwa chumba cha magma ndani ya ganda la dunia.

Volkeno hai na volkeno bwete[hariri | hariri chanzo]

Volkeno inaweza kupatikana kama volkeno hai inayoendelea kutema moto, gesi na majivu. Inaweza pia kuonekana kama volkeno bwete inayokaa kama milima mingine bila kuonyesha dalili za moto. Lakini kutokana na umbo na tabia za miamba yake inaonekana mlima huu ulijengwa kwa njia ya kivolkeno.

Volkeno bwete inaweza kuamka tena. Mara nyingi kuwepo kwa chemchemi za maji ya moto au kutokea kwa gesi kwenye sehemu fulani ni dalili ya kwamba bado kuna njia kati ya mlima na magma ya chini. Kipindi kati ya milipuko kinaweza kuwa miaka mingi.

Mlipuko wa volkeno[hariri | hariri chanzo]

Mlipuko wa volkeno ni hatari sana kwa ajili ya wanadamu na mazingira. Hii hatari ni kubwa zaidi pale ambako volkeno ililala kama olkeno bwete kwa miaka mingi labda maelfu. Hapa mara nyingi watu wamevutwa na udongo mwenye rutba kutokana na majivu ya volkeno wajenge makazi na kulima. Kama hapa volkeni inageuka kuwa hai tena hatri ni kubwa. Kuna mifano ya vifo vingi vilivyosababishwa na volkeno. Hasara inategema kama miji iko karibu na volkeno au la, na kama serikali zina huduma za kutazama volkeno na kuonya watu watoke mapema wakati dalili za kwanza zinatokea.

Kati ya mifano ya milipuko makali inayojulikana zaidi ni:

  • mlipuko wa volkeno ya Vesuvio, Italia. Iliharibu miji ya Pompei na Herkulaneo mwaka 79 BK.
  • mlipuko wa volkeno ya Krakatau, Indonesia mwaka 1883. Ilirusha vumbi nyingi angani kiasi kilichoonekana kote duniani
  • mlipuko wa volkeno Nevado del Ruiz, Kolumbia mwaka 1985 uliua watu 25.000 kutokana na kuyeyusha theluji na barafu mlimani na kusababisha mafuriko ya ghafla

Ol Doinyo Lengai ni volkeno ndogo iliyolipuka Tanzania kaskazini mwaka 2006.


Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Volkeno kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Sciences de la terre.svg Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Volkeno kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.