Nenda kwa yaliyomo

Noti ya benki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Noti)

Kwa maana nyingine ya neno hili tazama noti (maana)

Karatasi ya pesa ya kwanza kutoka China.

Noti ya benki, kifupi: noti, (kutoka Kiingereza "banknote") kwa kawaida ni kipande cha karatasi (pia: plastiki) kinachochapishwa na kuonyesha namba fulani na jina la pesa ya nchi fulani. Inakubaliwa kama njia ya malipo halali. Pamoja na sarafu ni pesa taslimu ya nchi fulani.

Kwa kawaida vipande vya sarafu au pesa taslimu metalia huwa na viwango vidogo zaidi na noti huwa na viwango vikubwa zaidi.

Usalama wa noti za benki

[hariri | hariri chanzo]

Tangu noti zianze kutolewa, wahalifu wamejaribu kutengeneza noti bandia wakiiga zile zinazotolewa na benki rasmi. Kwa sababu hiyo benki kuu na serikali zinajitahidi kutoa noti ambazo ni vigumu kuziiga. Hapo wanatumia karatasi za pekee zisizopatikana madukani, wanachapisha kwa rangi zisizosomewa na mashine ya fotokopi, wanaingiza nyuzi za metali ndani ya karatasi na kadhalika.

Tangu mwisho wa karne ya 20 nchi kadhaa zimeanza kutoa noti za plastiki badala ya karatasi. Hizi zina gharama kubwa zaidi ya kuzitengeneza lakini hadi sasa usalama ni mkubwa zaidi, ni vigumu sana za kuigwa, pia hazichakai haraka kama vile noti za karatasi.

Historia ya noti za benki

[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha historia ya noti za benki ni barua zinazoahidi kulipa kiasi fulani cha pesa kwa mtu yeyote anayeshika barua ile. Kwa hiyo noti zilikuwa sawa na hundi za leo.

Barua badala ya sarafu nzito

[hariri | hariri chanzo]

Kwa asili vipande vya metali adili kama dhahabu au fedha vilitumiwa kama pesa vikipimwa kuwa na uzito fulani, kwa mfano "pound" ya Uingereza ilikuwa sawa na uzito wa "pauni" au ratili moja ya fedha.

Wakati uchumi ulipoongezeka watu walianza kutumia viasi vikubwa vya pesa na hii ilikuwa kazi ngumu kutokana na uzito wa sarafu nyingi. Hapo wafanyabiashara waliacha sarafu zao kwa mtu aliyeaminiwa na kushika barua kutoka kwake iliyothibitisha ya kwamba alishika kiasi fulani kwa niaba ya mwingine. Pale ambapo watu waliaminiana waliweza kutumia barua hizo kama malipo badala ya sarafu zenyewe.

Serikali ya kwanza ya kutoa pesa ya karatasi ilikuwa nasaba ya Song nchini China mnamo mwaka 960. Noti hizo zilikuwa na maandishi yaliyomwahidia mwenye kuishika ya kwamba atapewa kiasi fulani cha fedha akiipeleka noti za benki kwa idara ya fedha ya serikali. Kimsingi hii ilibaki muundo wa noti hadi karne ya 20 yaani zilikuwa ahadi za serikali au za benki kubwa kumpatia mwenye noti kiasi fulani cha dhahabu au fedha.

Tatizo la pesa ya karatasai tangu mwanzo lilikuwa kwamba serikali yenye matatizo iliweza kuendelea kuchapisha noti mpya kata kama haikuwa na akiba ya dhahabu au fedha ya kutosha. Hili halikuwa tatizo mara moja kwa sababu hali halisi noti zilifanya kazi zake kama thamani ya noti zote ililingana na thamani ya bidhaa zilizopatikana katika nchi fulani. Lakini kama serikali iliendelea kuchapisha pesa hovyo watu walianza kuona ya kwamba pesa haina thamani tena na bei zilianza kupanda haraka sana.

Katika Ulaya pesa ya karatasi ya kwanza iliyotolewa na serikali au kwa niaba ya serikali ilianza kupatikana tangu karne ya 16 katika Uholanzi na Ufaransa. Mara kwa mara majaribio hayo ya kwanza yalivurugika kutokana na kuchapisha noti nyingi mno na kushuka kwa thamani ya pesa hiyo.

Noti za benki zilianza kuwa kawaida hata kwa watu wa kawaida wakati wa karne ya 19. Mwanzoni benki kuu ya kila nchi kisheria ilipaswa kuwa na akiba ya dhahabu au fedha iliyolingana ama na noti zote au angalau na sehemu kubwa zake. Masharti hayo yalifutwa polepole kwa sababu ilionekana ya kwamba kama kiasi cha noti hakizidi thamani ya bidhaa nchini uchumi unaendelea bila mvurugo. Tena baada ya kupatikana kwa mawasiliano ya kisasa kama simu na intaneti kiasi kikubwa cha ahadi za kulipana inazunguka katika uchumi na hizo ahadi zinafanya kazi kama pesa, hata kama si pesa taslim.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Simple English Wiktionary
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:
Picha za benknoti za dunia
Benknoti za plastiki
Vyama vya watu wanaokusanya aina nyingi za benknoti
Wachapishaji
Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Noti ya benki kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.