Nasaba ya Song
Nasaba ya Song ilikuwa nasaba ya kifalme ya China iliyotawala kutoka mwaka 960 hadi 1279. Nasaba hiyo ilianzishwa na kaizari Taizu wa Song, ambaye alinyakua utawala wa WaZhou wa Baadaye na kuendelea kushinda Falme Kumi. Hivyo alimaliza kipindi cha Nasaba tano na milki kumi (907 – 960).
Wasong walishindana na nasaba za Liao, Xia wa Magharibi na Jin walioshika maeneo ya kaskazini mwa China wakati huohuo. Baada ya kuhamia kusini mwa China, Wasong hao hatimaye walishindwa na Wamongolia walioanzisha Nasaba ya Yuan.
Kipindi cha nasaba hiyo hugawanywa katika sehemu mbili : Wasong wa Kaskazini na Wasong wa Kusini.
Wakati wa Wasong wa Kaskazini (960–1127), mji mkuu ulikuwa Bianjing (leo Kaifeng) na nasaba hiyo ilidhibiti sehemu kubwa ya eneo ambalo leo ni China ya Mashariki.
Wasong wa Kusini (1127–1279) inarejelea kipindi baada ya Song kupoteza udhibiti wa nusu yake ya kaskazini kwa nasaba ya Jin iliyoongozwa na Wajurchen kutoka Manchuria. Wakati huo, Wasong walipeleka mji mkuu huko Lin'an (leo Hangzhou) upande wa kusini wa Mto Yangtze. Hata baada ya kupoteza sehemu za kaskazini, Wasong wa Kusini waliendelea kutawala juu ya watu wengi na ardhi yeye rutuba. Uchumi, jeshi na utamaduni wao vilikuwa na nguvu.
Mnamo 1234, nasaba ya Jin ilishindwa na Wamongolia, ambao walichukua udhibiti wa kaskazini mwa China. Wasong walishirikiana na Wamongolia katika vita dhidi Jin lakini baadaye walifarakana kuhusu ugawaji wa maeneo ya kaskazini.
Hivyo Wamongolia walishambulia Wasong wa Kusini walioweza kujitetea kwa miongo kadhaa. Baada ya kutwaa maeneo mengi ya kusini ya China, mtawala wa Wamongolia Kublai Khan alijitangaza kama kaizari wa China akianzisha nasaba ya Yuan mnamo 1271.[1] Hatimaye majeshi ya Kublai Khan yalishinda mabaki ya maeneo ya Song kwenye mwaka wa 1279. China iliunganishwa tena chini ya nasaba ya Yuan.
Sayansi, teknolojia, falsafa, hisabati na uhandisi zilistawi katika enzi ya Song. Nasaba hiyo ilikuwa ya kwanza katika historia ya Dunia kutoa noti za benki (pesa halisi za karatasi). Ilikuwa serikali ya kwanza ya China kuanzisha jeshi la kudumu la wanamaji. Fomula ya kikemia ya baruti inashuhudiwa mara ya kwanza katika muswada ya kipindi hicho. Wakati huo silaha za kwanza za baruti zilibuniwa kama vile mishale ya moto, mabomu na mikuki ya moto. Kaskazini halisi iliweza kuonyeshwa kwa kutumia dira. Katika kipindi cha Song tunaona pia taarifa za kwanza kuhusu mlango wa mashua, na miundo iliyoboreshwa ya saa za nyota.
Uchumi wa milki ya Song ulikuwa mara tatu kuliko ule wa Ulaya yote katika karne ya 12[2]. Idadi ya wakazi wa China iliongezeka maradufu kati ya karne ya 10 na 11. Ukuaji huo uliwezekana kwa upanuzi wa kilimo cha mpunga, matumizi ya mpunga kutoka Kusini-mashariki na Kusini mwa Asia unaoiva mapema. Uzalishaji wa chakula cha ziada ulienea.[3] Sensa ya Song wa Kaskazini ilirekodi milioni 20 za kaya, mara mbili ya zile za nasaba za Han na Tang. Ongezeko kubwa la idadi ya watu lilichochea mapinduzi ya kiuchumi katika China ya siku zile.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Rossabi, Morris (1988), Khubilai Khan: His Life and Times, Berkeley: University of California Press, ISBN 978-0-520-05913-9
- ↑ Chaffee, John W. (2015), The Cambridge History of China Volume 5 Part Two Sung China, 960-1279, Cambridge University Press
- ↑ Ebrey, Patricia Buckley; Walthall, Anne; Palais, James B. (2006), East Asia: A Cultural, Social, and Political History, Boston: Houghton Mifflin, ISBN 978-0-618-13384-0, uk 156