Sacrosanctum Concilium

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Sacrosanctum Concilium (Kilat. Mtaguguso (au: mkutano) mtakatifu) ni jina fupi la hati ya Mtaguso wa pili wa Vatikano inayohusu liturujia au utaratibu wa ibada katika kanisa katoliki.

"Sacrosanctum Concilium" ni maneno mawili ya kwanza ya hati hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kilatini.

Azimio hili lilipitishwa kwenye kikao cha pili cha mtaguso na maaskofu na makasisi 2147 kati ya waliohudhuria wakati 4 tu waliipinga, halafu Papa Paulo VI aliitangaza kama mafundisho ya kanisa tarehe 4 Desemba 1963. Hutazamwa kuwa kati ya hati muhimu zaidi za mtaguso.

Ilileta mabadiliko makuu katika ibada za kanisa katoliki, hasa matumizi ya lugha za kawaida za watu katika ibada badala ya Kilatini kama lugha kwa nchi zote.

Lengo la hati hiyo ni kufanya kwanza mapadri, halafu Wakristo wengine pia waelewe na kutimiza liturujia ili kwa njia yake wamtukuze kweli Mungu na kufaidika Kiroho.

Mabadiliko haya yaliandaliwa kwa muda mrefu na mapapa mbalimbali wakati wa karne ya 20 hasa na kamati iliyopewa wajibu huu na Papa Pius XII kuanzia 1959.

Kikwazo kikuu kilionekana katika matumizi ya lugha ya Kilatini iliyokuwa tayari lugha ya kihistoria bila wasemaji kama lugha ya kwanza. Kwa hiyo walikuwa hasa wasomi pekee walioweza kuelewa masomo na mengineyo ya liturujia. Watu wa kawaida mara nyingi walikuwa watazamaji tu wa matendo ya ibada. Bila ya kupata mafundisho ya kutosha wala sakramenti ya ekaristi, Wakristo wa Magharibi walijitungia ibada zao badala ya kutegemea liturujia ya Kanisa.

Huko Mashariki hali ilikuwa tofauti kabisa: ndiyo sababu hati hiyo inahusu liturujia ya Roma tu, isipokuwa misingi ya liturujia yoyote na mengineyo yanayofaa kokote.

Sura ya kwanza[hariri | hariri chanzo]

Sura hii inahusu kanuni za jumla kwa urekebisho na ustawishaji wa liturujia.

Kwanza inaeleza undani na umuhimu wake, halafu inasisitiza haja ya malezi ya kiliturujia kuanzia seminari na nyumba za kitawa ambapo maisha yote yafuate roho ya liturujia na masomo yote yafundishwe kwa kuonyesha uhusiano wake na liturujia ambayo ihesabiwe kati ya masomo muhimu zaidi na kufundishwa na wataalamu. Hivyo waamini wote watasaidiwa kuchota roho halisi ya Kikristo katika chemchemi hiyo ya kwanza na ya lazima; pia wataweza kushiriki ibada kwa jinsi iliyo haki na wajibu wao.

Baadaye tu yanaagizwa marekebisho ya jumla ya liturujia na vitabu vyake vyote; msingi wake ni kwamba liturujia, mbali ya mambo yaliyoagizwa na Bwana Yesu, ina mengi yaliyopangwa na Kanisa lenyewe katika historia yake kulingana na mahali na nyakati mbalimbali. Kwa hiyo mara kwa mara linaweza na kupaswa kuyapanga upya kwa manufaa ya waamini.

Kwa kuwa liturujia ni kazi ya Kanisa lote, inaratibiwa na uongozi wake tu: wengine wasithubutu kubadilisha lolote wanapofanya ibada zake.

Hata uongozi wa Kanisa usirekebishe vitabu harakaharaka na pasipo lazima, bali uhakikishe kwamba mapya yanalingana na ya zamani.

Kwa namna ya pekee ni lazima neno la Mungu katika liturujia liheshimiwe linavyostahili, tena lionjwe kama ilivyokuwa mwanzoni mwa Kanisa.

Maagizo mengine yanatokana na hali ya kijumuia ya liturujia, yaani kwamba ibada zake si za binafsi, bali ni za Kanisa lote, na kila mmoja anahusika namna yake kama mwamini wa kawaida au kama mwenye daraja au huduma fulani. Hivyo ipendelewe ibada ya pamoja ambapo kila mmoja ashike nafasi yake na kulingana vizuri na wengine wanaoshika nafasi zao.

Maagizo mengine yanazingatia faida ya waamini upande wa imani ikiwa ni pamoja na kujifunza undani wake.

Kwa ajili hiyo mtaguso huo umeamua ibada zieleweke kwa urahisi, mapadri watoe hotuba na mawaidha mbalimbali wakati wa ibada, pia ziruhusiwe lugha hai za watu ingawa Kilatini kinabaki lugha rasmi ya madhehebu ya Kanisa la Magharibi na waamini wake wote wanatarajiwa kujua kuitikia na kuimba kwa Kilatini wakati wa Misa.

Mbali ya lugha, mtaguso umekubali yafanyike marekebisho mengine ili kupokea katika liturujia ya Roma utamaduni wa makabila yoyote mradi usipingane na imani. Utamadunisho huo ufanyike chini ya Baraza la Maaskofu na kukubaliwa na Roma.

Mwisho wa sura hiyo unasisitiza umuhimu wa watu kushiriki liturujia ya askofu katika Kanisa kuu na ile ya parokia ili waamini wajisikie kweli Kanisa moja.

Ili kustawisha liturujia mtaguso umeagiza ziwepo kamati maalumu kitaifa na kijimbo.

Sura ya pili hadi ya tano[hariri | hariri chanzo]

Ili kutekeleza yaliyosemwa hapo juu, sura ya pili inaagiza namna ya kurekebisha madhehebu ya Misa, sura ya tatu inafanya vilevile kuhusu sakramenti nyingine na visakramenti, na sura ya nne kuhusu Sala ya Kanisa.

Kufikia miaka ya 90 vitabu hivyo vyote vilikuwa tayari vimerekebishwa: katika kuvitumia ni muhimu kujisomea utangulizi wake.

Sura ya tano inarekebisha mwaka wa Kanisa kusudi mpango wake ueleweke zaidi bila ya kujaa mno sikukuu za watakatifu: hasa siku ya Bwana na vipindi maalumu vya mwaka vipate nafasi vinavyostahili.

Sura za mwisho[hariri | hariri chanzo]

Sura mbili za mwisho zinahusu muziki na sanaa takatifu ili liturujia ipendeze kwa uzuri wake, iinue roho kwa Mungu na kuwa kielelezo cha ile ya mbinguni. Hivyo vipawa mbalimbali vya binadamu vitumike kumtukuza Mungu.

Hayo yameelezwa baada ya vitabu kwa sababu hivyo vina neno la Mungu na maitikio ya watu kwa neno hilo lenye kuwatakasa.

Vilevile muziki unaelezwa kabla ya sanaa nyingine kwa sababu unaambatana na maneno matakatifu.

Mtaguso umesisitiza umuhimu wa kuimba katika liturujia, ukiagiza malezi kwa ajili hiyo, uundaji wa kwaya, utungaji wa nyimbo ambazo zichote hasa katika vitabu vya Biblia na liturujia.

Kuhusu aina za muziki mtaguso umekubali aina yoyote inayoweza kulingana na utakatifu wa ibada; vilevile umeruhusu ala mbalimbali za kufaa.

Hata hivyo liturujia ya Roma inapendelea muziki wa Kigregori na kinanda cha mabomba.

Sanaa nyingine pia zinaheshimiwa na kutumiwa na Kanisa kwa ujenzi, mapambo, vifaa na picha takatifu. Kadiri ya mahali na nyakati limekubali mitindo mbalimbali mradi ilingane na imani, maadili na ibada ya Kikristo.

Mtaguso umeagiza maaskofu hasa wajitahidi kudumisha msimamo huo na uzuri wa yote yanayohusu liturujia, kwa kuelimisha wanasanaa na makleri.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]