Daraja takatifu
Daraja takatifu katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo ni jina la vyeo vya askofu, kasisi na shemasi vinavyounda uongozi wa Kanisa.
Katika Kanisa Katoliki na ya Waorthodoksi ngazi hizo tatu zinaunda kwa pamoja mojawapo ya sakramenti saba ambazo Yesu Kristo alizianzisha na kulikabidhi Kanisa lake.
Baadhi ya Waprotestanti wana huduma hizo lakini kwao si sakramenti.
Jina
[hariri | hariri chanzo]Katika Kigiriki daraja zinaitwa taxeis, na katika Kilatini ordines, kwa sababu waliopewa wanaunda kundi moja.
Ibada ilivyo
[hariri | hariri chanzo]Tangu zamani za Mitume wa Yesu mamlaka inashirikishwa kwa tendo la kumwekea mtu mikono kichwani, kufuatana na mfano wa Musa kwa Yoshua katika Agano la Kale.
Tendo hilo linafuatana na sala maalumu ambayo, katika kumuomba Roho Mtakatifu amshukie mhusika, inaweka wazi daraja gani inatolewa.
Anayetoa daraja
[hariri | hariri chanzo]Kwa kawaida mwenye jukumu la kutoa daraja takatifu ni askofu wa jimbo (dayosisi), ingawa historia ya Kanisa inasababisha maswali kadhaa juu ya jambo hilo hasa upande wa daraja za chini.
Anayeweza kupewa
[hariri | hariri chanzo]Ni imani ya Kanisa Katoliki, ya makanisa ya Waorthodoksi na ya madhehebu mengine kadhaa kwamba daraja zinaweza kutolewa kwa wanaume tu, kwa sababu Yesu aliteua watu wa jinsia hiyo tu awape mamlaka yake ambayo inashirikishwa kwa daraja hizo, na kwa sababu ndiyo mapokeo ya Kanisa tangu mwanzo.
Waprotestanti wanazidi kukubali wanawake katika nafasi zote za uongozi, wakisisitiza usawa wa wafuasi wa Yesu.
Katika Kanisa Katoliki na makanisa ya Waorthodoksi wanaopewa daraja wanaweza wakadaiwa pia hali na ahadi ya useja mtakatifu. Ni hivyo walau kuhusu uaskofu, lakini pengine hata kuhusu upadri.
Hali ya kudumu
[hariri | hariri chanzo]Sawa wa sakramenti za Ubatizo na Kipaimara, katika imani ya Wakatoliki daraja takatifu zinamtia mwamini alama isiyofutika ya kikuhani aweze kumtolea Mungu ibada katika liturujia na katika maisha yake yote.
Kwa maana hiyo daraja inadumu ndani ya mtu hata akiacha kutoa huduma au kuasi kabisa.
Misingi ya imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi katika Biblia
[hariri | hariri chanzo]Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi |
---|
|
Kadiri ya imani hiyo, daraja takatifu zinahitajiwa kabisa na Kanisa kwa sababu kazi ya wokovu haimtegemei binadamu, bali Mungu. “Hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu” (Eb 5:4-5), bali alisisitiza alivyopewa na Baba uwezo wa kutuokoa. “Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake” (Yoh 3:35). “Kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele” (Yoh 17:2). Kisha kufufuka alitumia mamlaka hiyo kuwatuma wanafunzi kumi na mmoja waliobaki: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Math 28:18-20). Mpaka mwisho wa dunia uwezo huo wa Kimungu utatolewa tu kwa sakramenti ya daraja, inayounganisha mtu na Mitume kupitia mlolongo usiokatika wa kuwekewa mikono ili kushirikishwa mamlaka. Bila yake, kuna upungufu katika ufundishaji, utoaji wa sakramenti na uongozi.
Wenye daraja wanastahili heshima kwa sababu ya mamlaka ya Kiroho waliyonayo kutoka kwa Kristo. “Amin, amin, nawaambieni: Yeye ampokeaye mtu yeyote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenipeleka” (Yoh 13:20). “Jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu” (Gal 4:14). “Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii” (Tito 3:1). Wenye daraja wanaotimiza kazi zao vizuri wanastahili heshima kwa uaminifu wao pia. “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu, hasa hao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha” (1Tim 5:17).
Wenye daraja wanaweza wakatenda dhambi kwa sababu ni binadamu kama sisi sote. Yesu alionja ukosefu wa Mitume hasa wakati wa mateso. “Je, mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani?” (Yoh 6:70). “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao, na kuniacha mimi peke yangu” (Yoh 16:32). Mtume Paulo alionya mapadri, “Katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao” (Mdo 20:30).
Kadiri ya Injili ili tuwe na wachungaji wengi waaminifu tunapaswa hasa kusali. “Mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake” (Math 9:38). Halafu yanahitajika maandalizi ya muda mrefu, juhudi na ushirikiano wa kidugu. “Asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi... Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia... Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine” (1Tim 3:6; 4:16; 5:22).
Wanawake hawawezi kupewa daraja, kwa sababu kwa karibu miaka elfu mbili mfululizo Kanisa limejiona halina mamlaka ya kufanya tofauti na Yesu. Yeye alichagua wanaume tu kuwa Mitume wake, ingawa walikuwepo wanawake waaminifu kuliko wengi wao, hasa Bikira Maria, mtakatifu kuliko wote. “Petro, na Yohane, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake... Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya... kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja” (Mdo 1:13-14,23,26). “Walimchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao” (Mdo 6:5-6).
Kutoa daraja kwa wanaume tu si kuwakosea haki wanawake, kwa kuwa hizo ni huduma zinazofaidisha wote. “Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye” (Lk 22:27). Mwenye daraja anahudumia Kanisa kwa kumwakilisha Yesu; hivyo anatakiwa kuwa mwanamume kama yeye mbele ya Bibiarusi wake. Kukubali mgawanyo wa majukumu maishani ni kusifu hekima ya Mungu aliyetuumba watu wa jinsia mbili tofauti ili kustawisha familia, jamii na Kanisa. “Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana... Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1Kor 11:11; 12:27).
Mwenye daraja anaweza kuwa na ndoa. “Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?” (1Kor 9:5). Paulo, akiwa mseja, hakudai kila mmojawao aoe, ila asiwe ameoa mara mbili, bali “mume wa mke mmoja” (1Tim 3:2; Tit 1:6), kama alivyoagiza mjane aandikishwe akiwa tu “mke wa mume mmoja” (1Tim 5:9). Polepole mang’amuzi yakaelekeza Kanisa kubana nafasi hiyo kwa Maaskofu, na katika majimbo mengi kwa mapadri pia. Useja mtakatifu unawalinganisha zaidi na Yesu na kuwaachia uhuru wa moyo na wa muda kwa ajili ya huduma. “Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee” (Math 19:12).
Vyeo vingine visivyo sakramenti
[hariri | hariri chanzo]Katika madhehebu mbalimbali kuna vyeo tofauti na daraja takatifu, ambavyo vilianzishwa na Kanisa kulingana na mahitaji ya mahali na nyakati, kama vile vya Patriarki, Kardinali, Askofu mkuu, Korepiskopo, Paroko, Vartan, Mwenyekiti n.k.
Katika Kanisa Katoliki cheo cha kwanza ni kile cha Papa , ambacho kinategemea na kudai sakramenti ya daraja katika ngazi ya uaskofu kwa sababu ni kukabidhiwa jimbo la Roma kama mwandamizi wa Mtume Petro aliyefia huko.
Imani ya Kanisa hilo ni kwamba cheo hicho, ingawa si sakramenti, ni mpango wa Yesu aliyetaka mitume wake wawe kundi moja chini ya Petro, hivyo waandamizi wao wawe kundi moja chini ya mwandamizi wa Petro, yaani maaskofu wote duniani wawe kundi moja chini ya mkuu wao, askofu wa Roma.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Daraja takatifu kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |