Waanabaptisti

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Uenezi wa tapo hili katika Ulaya ya Kati miaka 1525-1550.


Waanabaptisti (kwa Kilatini anabaptista,[1] kutoka Kigiriki ἀναβαπτισμός ambapo ἀνά, ana inamaanisha "tena" na βαπτισμός, baptismos, "ubatizo"[2]) ni Wakristo ambao hasa kuanzia karne ya 16 walikataa ubatizo jinsi ulivyotolewa na Kanisa Katoliki na madhehebu mbalimbali ya Uprotestanti.[3][4]

Kwa sababu hiyo, wenyewe hawapendi kuitwa hivyo: kwa mtazamo wao, hawarudii ubatizo, ila wanautoa kwa usahihi kwa mara ya kwanza.[5]

Msimamo wao ulisababisha kuanzia mwaka 1527 dhuluma kali kutoka kwa viongozi wa madhehebu hayo mbalimbali.

Kwa sasa Waanabaptisti wote hawafikii milioni 2 duniani.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Martin Luther yalianza pia madhehebu ambayo zamani hizo yalikataliwa na makanisa mengine yote: Waanabaptisti. Ni kwamba wakati ule wa mabadiliko walijitokeza Wakristo waliopenda kuwa karibu zaidi na mfano wa Ukristo wa kwanza. Walitaka Kanisa liwe jumuiya ya watakatifu, yaani Wakristo wa kweli tu. Waliona wengi kuwa Wakristo wa jina tu.

Walivyojisomea Biblia walishindwa kuelewa desturi ya kubatiza watoto. Jinsi walivyoona, mwanzoni watoto wadogo hawakubatizwa ila watu wazima walioamini. Kwa jumla wakaona desturi ya kubatiza watoto wasiofahamu imani ni msingi wa kuwa na wanafiki na Wakristo wa uongo ndani ya kanisa.

Mwaka 1525 huko Uswisi ulitokea ubatizo wa mtu mzima. Aliwahi kubatizwa utotoni lakini alianza kuelewa imani na kuongoka katika umri mkubwa tu. Akajisikia apokee "ubatizo wa imani".

Habari hii na mafundisho yaliyolingana nayo vilienea haraka sana Uswisi na Ujerumani. Katika miji mbalimbali Wakristo walivutiwa kukutana katika vikundi vidogo nje ya makanisa, wakisali pamoja na kuwa na Chakula cha Bwana nyumbani mwao. Walioamini kwa njia hiyo mpya walitafuta "ubatizo wa imani".

Viongozi Wakatoliki na pia Waprotestanti wakapinga mafundisho yao. Wakaona ni kudharau sakramenti ya ubatizo, maana wale wote wameshawahi kubatizwa kama watoto wadogo. Tena walikuwa na shaka juu ya kanisa kuwa jumuiya ya "Wakristo wa kweli tu". Nani aamue juu ya ukweli wa rohoni kama si Mungu mwenyewe?

Jinsi Waanabaptisti walivyojaribu kulinda utakatifu wa kanisa lao kwa kuweka masharti mbalimbali juu ya maadili, wengine waliona wameunda taratibu za kibinadamu. Luther, aliyetoka katika jitihada za umonaki alipojaribu kujenga utakatifu wake kwa kutimiza masharti mengi, aliona kosa lilelile katika "watakatifu" wale.

Tatizo lingine lilikuwa uhusiano wao na serikali na dola. Walisoma katika Biblia kwamba Mkristo asiape wala kutumia silaha, wala kushiriki katika mambo ya serikali. Kumbe wakaonekana ni maadui wa kila serikali.

Jambo la kusikitisha sana ni kwamba madhehebu makubwa yaliyoendelea chini ya ulinzi wa serikali za maeneo yao yalikuwa tayari kuwagandamiza kinyama Waanabaptisti. Waliobatiza watu wazima na kuhubiri imani hiyo wakatafutwa na kukamatwa, kufungwa gerezani na hata kuuawa. Katika matendo ya namna hiyo zilishirikiana serikali zote za Ulaya, kama ni za Kikatoliki, za Kilutheri au za Kikalvini.

Baada ya wengi wao kuuawa, Waanabaptisti wengine walianza kujificha au kuhamia mahali walipopata ustahimilivu. Kikundi kimoja kiliweza kuishi Uholanzi na Ujerumani Kaskazini. Kiongozi wao alikuwa Menno Simoni. Wafuasi wake wakaitwa "Wamenno".

Baadaye wakahamia mpaka Urusi kutafuta mahali penye uhuru wa dini wasipolazimishwa kuwa wanajeshi wala kuapa mahakamani.

Walienea hasa Marekani walipokimbilia wafuasi wake kutoka sehemu mbalimbali za Ulaya.

Katika karne zilizofuata wamisionari wao walirudi tena Ulaya na kuenea sehemu nyingine za dunia.

Waanabaptisti wanaangalia zaidi uhuru wa ushirika pale wanaposali kuliko umoja wa Kanisa, hivyo wako duniani katika vikundi mbalimbali.

Jumuiya zao zilipokua baadaye, sehemu kubwa ya Waanabaptisti waliacha tena masharti ya kutotumia silaha au kukataa kiapo mahakamani, kama tumeshaona katika vikundi vingine.

Nchini Tanzania Wamenno wako hasa kaskazini, lakini kitovu cha Kanisa la Kibatisti lililoundwa na wamisionari Wamarekani ni katika Nyanda za Juu za Kusini. Kanisa la "African Inland Church - AIC" linafuata pia mapokeo ya Kibatisti katika mengi ila linatumia cheo cha Askofu.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "Anabaptist, n.", Oxford English Dictionary (Oxford University Press), December 2012, retrieved 21 January 2013 
  2. "Anabaptism, n.", Oxford English Dictionary (Oxford University Press), December 2012, retrieved 21 January 2013 
  3. McGrath, William, "Neither Catholic nor Protestant", CBC 4 me (PDF), archived from the original on 2016-12-27, retrieved 2014-08-30 
  4. Gilbert, William, "CHAPTER 15 THE RADICALS OF THE REFORMATION", THE ANABAPTISTS AND THE REFORMATION, archived from the original on 2018-12-25, retrieved 2014-08-30 .
  5. Vedder, Henry Clay (1905). Balthasar Hübmaier, the Leader of the Anabaptists. New York: GP Putnam's Sons. 

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Waanabaptisti kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.