Sifa nne za Kanisa
Sifa nne za Kanisa, kadiri ya imani ya madhehebu mengi ya Ukristo, ni zile ambazo zinalitambulisha Kanisa la kweli kati ya makundi mengi ya Ukristo ni kuwa moja, takatifu, Katoliki, la Mitume.
Sifa hizo zilitajwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) uliporefusha Kanuni ya Imani iliyotungwa na Mtaguso wa kwanza wa Nisea (325).
Ndiyo sababu zinakubaliwa na madhehebu mengi, ingawa zinatafsiriwa nayo kwa namna tofautitofauti.
Teolojia ya Kanisa Katoliki
[hariri | hariri chanzo]Kanisa Katoliki linaona sifa hizo zinalitambulisha kati ya madhehebu mengi kama Kanisa pekee lililoanzishwa na Yesu kumpitia Mtume aliyembadilishia jina aitwe Petro, yaani Mwamba wa Kanisa lake lisilokoma wala kupotoka kamwe: “Wewe u Simoni, mwana wa Yohane; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro)” (Yoh 1:42). Siku ya Pentekoste, “waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu” (Mdo 2:41). Ndiye aliyekaribisha hata wasio Wayahudi: “Tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini” (Mdo 15:7). Baada ya kuongoza Mitume wenzake na Kanisa lote, aliuawa msalabani huko Roma kama alivyotabiriwa: “’Utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka’. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu” (Yoh 21:18-19).
Kanisa kuwa moja maana yake ni “mwili mmoja na Roho mmoja”: lina “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” (Ef 4:4-5). Yesu alisema, “Na kondoo wengine ninao. Ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja” (Yoh 10:16). Hakuna Kanisa lingine, isipokuwa matawi ambayo yamekatika kwa kiasi tofauti, na yana uhai kadiri yanavyounganika bado na shina. Hata leo Kanisa Katoliki peke yake lina waamini wengi kuliko jumla ya madhehebu mengine ya Kikristo.
Kanisa kuwa takatifu maana yake ni kazi ya Mungu mtakatifu inayong’aa katika watakatifu wa mbinguni, hasa Bikira Maria. “Ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu” (1Pet 2:9-10). “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika Neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa” (Ef 5:25-27). Hata hivyo hapa duniani linaundwa na wakosefu pia: “Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila namna. Hata lilipojaa, walilivuta pwani, wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa” (Math 13:47-48).
Kanisa kuwa katoliki maana yake linaweza kuwatolea watu wote wa mahali pote na wa nyakati zote kweli zote za imani na vifaa vyote vya kufikia wokovu wa milele. “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Math 28:18-20).
Kanisa kuwa la Mitume maana yake limejengwa juu ya Mitume 12 wa Yesu na kuongozwa na waandamizi wao. “Ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo” (Ufu 21:14). “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Yesu Kristo mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Ef 2:20-22).
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Four Marks of the Church Archived 26 Februari 2019 at the Wayback Machine. by Kenneth D. Whitehead
- The Four Marks of the Church Archived 3 Juni 2008 at the Wayback Machine. by Fr. William Saunders
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sifa nne za Kanisa kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |