Nenda kwa yaliyomo

Shaka Zulu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Shaka)
Picha ya Shaka Zulu mnamo mwaka 1824

Shaka (pia: Tshaka, Tchaka au Chaka; halafu: Shaka Zulu, Shaka ka Senzangakhona) (* takriban 1781 - 1828 BK) alikuwa kiongozi wa Wazulu aliyebadilisha ukoo mdogo wa Kinguni kuwa kabila au taifa kubwa lililotawala maeneo mapana ya Afrika Kusini hasa Natal ya leo.

Sifa zake zimetokana na uwezo wa kupanusha utawala wake kutoka eneo ndogo la 260 km² kuwa 28.500 km², kuvunja nguvu ya makabila mengine na kuyaunganisha na taifa lake. Katika historia ya kijeshi ya Afrika alianzisha mbinu mpya zilizopanusha uwezo na enzi yake. Sifa hizi, jinsi ilivyo mara nyingi na viongozi wanaotegemea nguvu ya kijeshi, zimeenda pamoja na vita na uharibufu mwingi. Miaka ya Shaka ilianzisha kipindi cha mfecane yaani "uharibifu" kinachokumbukwa na mataifa mengi ya Afrika Kusini.

Maisha yake

[hariri | hariri chanzo]

Shaka alikuwa mtoto wa chifu Senzangakhona ka Jama na Nandi binti wa chifu wa Langeni. Jina lake ni kutokana na neno la kizulu "iShaka" linalomtaja mdudu ambaye katika imani ya utamaduni wa Kizulu anasemekana kuvuruga hedhi ya wakinamama. Jina hili ni dalili ya kuzaliwa nje ya utaratibu. Hivyo miaka ya kwanza ya Shaka ilikuwa miaka migumu bila baba anayejulikana rasmi akisikia kudharauliwa na watu wengine. Utoto huu ulisababisha hasira ndani yake akalipiza kisasi baadaye.

Alipo kuwa kijana Shaka alikaa kwenye kabila kubwa zaidi la Mthethwa alikoingia pamoja na hirima yake katika jeshi. Wakati ule ukoo wa Wazulu walikubali Wamthehtwa kuwa mabwana wao. Chifu wa Mthethwa alikuwa Dingiswayo aliyeanzisha utaratibu mpya wa impi yaani kupanga watu wake vitani katika vikundi na kuwa na ngazi mbalimbali za mamlaka. Shaka alihudumia miaka sita katika vita za Dingiswayo akawa hodari sana na kujifunza uongozi aliouboresha baadaye.

Kurudi kwa Wazulu

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kifo cha baba yake, Shaka alirudi kwa Wazulu kwa msaada wa Dingiswayo akachukua uongozi mnamo mwaka 1812. Baada ya kuwa kiongozi akalipiza kisasi kwa maadui zake wa utotoni na kuwaua kwa njia mbalimbali.

Shaka aliendelea kukubali ubwana wa Mthethwa na Dingiswayo alipouawa vitani na kabila la Ndwandwe mwaka 1817. Lakini pamoja na hayo alipigana vita na koo au makabila madogo jirani. Mbinu yake ilikuwa kuwashambulia waliompinga au kuwa hatari kwake; wanawake na watoto waliingizwa katika ukoo wake, pamoja na wanajeshi wa kiadui walio salimika kufa vitani lakini waliokubali kumfuata baada ya kushindwa. Kwa njia hiyo ukoo mdogo wa Wazulu uliendelea kukua.

Eneo la milki ya Shaka

Kupanusha utawala na mfecane

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kifo cha Dingiswayo mw. 1817 Shaka alishambulia kabila kubwa la Ndwandwe akawashinda kwenye mapigano ya kilima cha Gqokli kwa sababu ya mbinu zake za kijeshi ingawa idadi ya watu wake ilikuwa nusu tu ya adui.

Katika miaka iliyofuata Shaka aliendelea kushambulia vikundi vya jirani na kuwaingiza katika utawala wake. Makabila mengine walimfuata bila vita wakikubali uongozi wake na kuingiza vijana wao katika impi au vikosi vya kijeshi vya Shaka. Alituma viongozi au majenerali zake pamoja na impi pande mbalimbali hadi Msumbiji na Zimbabwe. Vikundi kama Ndebele huko Zimbabwe au hata Wangoni katika Tanzania ni matokeo ya matembezi ya impi za kizulu zilizoenda mbali na kupoteza mawasiliano na nyumbani.

Vita hizi zilisababisha makabila mengine kukimbia na kuhamahama wakishambulia majirani zao iliyopelekea kupanua eneo la vita katika nchi mbali na Wazulu wenyewe. Kipindi hiki kinakumbukwa kwa majina kama "mfecane" (Kizulu) au "difaqane" (Kisotho) kuwa miaka 30 ya vita na kifo.

Katika mawazo ya wataalamu Shaka aliandaa upanuzi wa Makaburu kwa uharibifu wa vita zake. Makaburu walipoanza kuenea ndani ya Afrika Kusini walikuta maeneo mazuri bila watu lakini maghofu ya kuonyesha watu waliwahi kuishi hapa. Pamoja na hayo makabila mengine kama Wasotho, Waswazi, Wandebele au Wagaza walioshambuliwa walijifunza mbinu za kijeshi, wakaweza kujitetea na kuanzisha mataifa makubwa yaliyounganisha koo na makabila madogo zaidi.

Utawala wa Shaka ulikuwa na tabia za kinyama zilizosababisha chuki nyingi dhidi yake. Baada ya kifo cha mamake Nandi alikuwa na hasira kiasi cha kuua watu 7000 kati ya wanajeshi wake kwa kosa la kutoonyesha huzuni ya kutosha na kuamuru kipindi cha kufunga miezi mitatu. Aliamuru mashamba yasilimwe kwa mwaka mmoja na kila mwanamke aliyeonekana kuwa na mimba katika kipindi hiki aliuawa pamoja na mumewe. Wataalamu wengine huona ya kwamba wakati ule Shaka alionekana kuwa na kichaa. Maadui walifanya mipango dhidi yake mwishowe aliuawa na ndugu zake. Mwaka 1828 impi nyingi zilikuwa mbali vitani ikulu ikawa bila ulinzi wa kutosha. Kaka zake Dingane na Mhlangana walimwua na kutupa maiti shimoni.

Dingane alimfuata Shaka akaua vingozi wengi waliokuwa waaminifu kwa Shaka.


Mafanikio ya kijeshi ya Shaka

[hariri | hariri chanzo]

Shaka aliboresha utaratibu alioukuta katika utumishi wa Dingiswayo. Wataalamu hutofautiana ni kwa kiasi gani ya kwamba Shaka alianzisha mbinu kadhaa au kiasi gani ndiye Shaka aliyeunganisha mbinu mbalimbali zilizowahi kujulikana lakini yeye alifuata utaratibu kuzitumia kushinda viongozi wote wengine. Kati ya mbinu alizotumia ni zifuatazo:

Silaha mpya

[hariri | hariri chanzo]

Utamaduni wa Wanguni ulikuwa mikuki ya assegai na kila mtu alibeba tatu. Shaka aliona silaha za kutupwa ni hasara. Aliongea mwenyewe na wahunzi akawapa wanajeshi silaha katikati ya mkuki na upanga - "Iklwa". Haikufaa kutupwa bali kushikwa hivyo kuwalazimisha watu wake kushambulia na kuwa karibu na adui. Aliwapatia pia vigao vizito vya ngozi ya ng'ombe.

Kutembea bila viatu

[hariri | hariri chanzo]

Alilazimisha watu wake kuacha kuvaa viatu au kukinga miguu yao na kutembea pekupeku. Hii iliongeza kasi ya impi zake na uwezo wao wa kushambulia haraka. Inasemekana ya kwamba Shaka aliua wote waliolalamika walipoamriwa kuacha viatu vyao.

Kujenga nidhamu

[hariri | hariri chanzo]

Shaka alijenga nidhamu ya watu wake kwa kuwa na utaratibu wa mamlaka kati yake mwenyewe na vikosi vidogo zaidi. Sehemu nyingine ilikuwa adhabu kali: askari asiyeweza kuonyesha damu kwenye silaha yake aliweza kuuawa baada ya kurudi vitani. Impi ambao walipata sifa machoni pa Shaka waliruhusiwa kuoa baada ya ushindi.

Kuwa na vikosi vya kusaidia mizigo

[hariri | hariri chanzo]

Shaka alitumia wavulana wadogo kuanzia umri wa miaka sita waliongozana na impi wakibeba mizigo au kuwafuata wanajeshi kwa ng'ombe kama chakula cha baadae. Hata hii iliharakisha mwendo wa impi zake.

Impi wa hirima

[hariri | hariri chanzo]

Hirima au vikundi vya kujumuisha watu wa umri mmoja ni tabia ya utamaduni kwa Wabantu wengi. Shaka alipoanzisha impi zake -badala ya kushambulia na watu wake wote mara moja jinsi ilivyokuwa kawaida awali- alitumia vikundi vilivyokuwepo tayari kiutamaduni kama msingi wa impi zake.

Muundo wa Kichwa cha Mbogo

[hariri | hariri chanzo]

Shaka alitumia mpangilio wa impi zake vitani kwa umbo la "Kichwa cha Mbogo": 1. vikosi viwili upande wa kushoto na kulia vilikuwa kama "pembe za mbogo" 2. kikosi kikubwa cha katikati kilikuwa kama "uso" au "kifua" 3. vikosi vya ziada au vya wazee vilikuwa "viuno" vilivyotumika ama kuongeza uzito wa mashambulio panapohitajika au kuimarisha utetezi pale ambako adui alisogea mbele.