Mfecane

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mfecane (Kizulu: kutawanyika au kumegeka; kwa Kisotho "Difaqane") ni kipindi katika historia ya Afrika ya Kusini kati ya 1815 na 1840.

Kipindi cha vita na uhamisho wa makabila[hariri | hariri chanzo]

Kipindi hiki kilikuwa na mvurugo mkubwa kutokana na vita nyingi zilizosababisha uhamisho wa makabila yaliyolazimishwa kuondoka kwao au kutafuta mahali mapya yakiendelea kuhamahama hadi Tanzania, Malawi na Zambia.

Kikosi cha Wazulu mwisho wa karne ya 19

Mafanikio ya Shaka Zulu[hariri | hariri chanzo]

Harakati hii ilianzishwa na mafanikio ya ufalme wa Wazulu walioongozwa na Shaka Zulu. Shaka kama kiongozi wa kijeshi katika kundi dogo la Wanguni alibadilisha mtindo wa vita akaweza kushinda viongozi majirani na kuunganisha Wanguni katika himaya yake ya Kizulu. Mtindo huu mpya ulikuwa na mpangalio wa askari katika vikundi vyenye nidhamu kali vilivyoitwa impi na silaha mpya zilizolazimisha askari kukaribia maadui na kupigana nao ana kwa ana.

Uhamisho mfululizo[hariri | hariri chanzo]

Mafanikio ya kijeshi ya Shaka yalisababisha makabila mengine kukimbia yakiingia katika maeneo ya majirani ya kusababisha uhamisho wao. Wangoni wa eneo la Songea katika Tanzania ni kundi mojawapo lililoendelea kukimbia hasira ya Wazulu hadi kufika mbali.

Maeneo makubwa hasa katika tambarare za Afrika Kusini yalibaki bila watu kwa sababu vikundi vingi vilihamia mbali au kukimbilia maeneo ya milima penye usalama zaidi.

Mitindo ya kivita ya Kizulu ilinakiliwa haraka na makabila mengine na kipindi cha mfecane kiliona pia kutokea kwa madola mapya yenye nguvu ya kijeshi kama vile Sotho, Swazi na Ndebele.

Kuwapa nafasi makaburu[hariri | hariri chanzo]

Uharibifu uliosababishwa na mfecane uliorahisisha upanuzi wa makaburu aina ya voortrekker waliondoka katika koloni ya Rasi kuanzia 1835. Hata kama walikuwa wachache waliweza kuingia mbali katika maeneo yaliyowahi kukaliwa na makabila ya Kiafrika lakini kwa kipindi hiki kubaki bila watu.

Chanzo cha madola ya Kiafrika yenye uwezo wa kijeshi[hariri | hariri chanzo]

Vilevile mashindano ya kijeshi yalijenga madola ya Waafrika yaliyokuwa na nguvu kujitetea dhidi ya upanuzi wa jamhuri za Makaburu na baadaye ukoloni wa Uingereza. Waingereza walilazimishwa kutambua madola kama Lesotho au Uswazi kwa sababu waliogopa gharama kubwa za kuwashinda.

Athari ya vita za mfecane nje ya Afrika Kusini[hariri | hariri chanzo]

Vikundi vya Wazulu na vikundi vilivyoondolewa nao katika maeneo yao viliendelea kuhamahama wakaelekea kaskazini na kufika hadi sehemu za nchi za kisasa za Zambia, Malawi na Tanzania. Hapo ni pia asili ya Wangoni katika Mkoa wa Ruvuma (Songea) wa Tanzania.

Walileta mtindo wa kupigania vita katika vikosi vya impi ulioigwa na majirani yao kama Wasangu na Wahehe.