Yohane wa Avila

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mtakatifu Yohane wa Avila.
Mtakatifu Yohane wa Avila.

Yohane wa Avila (Almodóvar del Campo, Hispania, 6 Januari 1499 au 1500 - Montilla, Hispania, 10 Mei 1569) alikuwa padri mwanajimbo wa Hispania aliyeathiri sana Kanisa Katoliki la nchi hiyo na urekebisho wa Kikatoliki katika karne ya 16 hasa kwa njia ya mahubiri yake yaliyotegemea Biblia, ya uongozi wa kiroho na ya vyuo alivyovianzisha.

Kwa namna ya pekee mkoa wa Andalusia na watakatifu Teresa wa Yesu, Yohane wa Mungu na Fransisko Borja walifaidika na utume wake.

Papa Leo XIII alimtangaza mwenye heri tarehe 6 Aprili 1894, halafu Papa Paulo VI akamtangaza mtakatifu tarehe 31 Mei 1970.

Hatimaye Papa Benedikto XVI akamtangaza mwalimu wa Kanisa wa 34 tarehe 7 Oktoba 2012.[1]

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 10 Mei[2].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto na wito[hariri | hariri chanzo]

Yohane wa Avila alizaliwa huko Almodóvar del Campo (Ciudad Real, katika Jimbo Kuu la Toledo, Hispania) tarehe 6 Januari 1499 au 1500 katika familia tajiri na yenye imani ya Kikristo[3] ingawa yenye asili ya Kiyahudi.[4]Baba yake aliitwa Alonso Avila na mama Katalina Gijon.

Akiwa mtoto pekee, alipofikia umri wa miaka 14 alitumwa masomoni kwenye chuo kikuu cha Salamanca ili ajifunze sheria, lakini baada ya miaka miwili akarudi nyumbani kutokana na wongofu wa dhati akatumia miaka mitatu kufanya toba kali, kusali na kutafakari.

Utakatifu wake ulimvutia Mfransisko ambaye alipitia Almodóvar, akamshauri aanze masomo ya falsafa na teolojia kwa ajili ya upadri huko Alcalá de Henares, alipofundishwa na Mdominiko maarufu, Domingo de Soto. Chuo hicho kilikuwa wazi kwa mitazamo mbalimbali ya wakati ule na kwa tapo la Renaissance lililojali sana binadamu na mambo yake yote.

Wakati wa masomo hayo alifiwa wazazi; hivyo baaada ya upadrisho wake (1526) aliuza mali ya familia na kuwagawia maskini mapato yake.

Yeye aliona vifo hivyo kuwa ishara ya Mungu kumwita awe mmisionari akajiandaa kwenda Mexico.

Mwaka 1527, akiwa Seville ili kupata nafasi nzuri ya kusafiri baharini, alijitosa kuhubiri mjini na kandokando yake. Namna yake bora ya kuishi, kuadhimisha Misa na kuhubiri ilimshangaza padri Hernando de Contreras, mwalimu wa Alcalà maarufu upande wa katekesi, ambaye alimuarifu Askofu mkuu wa Seville, na pia Hakimu mkuu Alonso Manrique de Lara.

Askofu alitambua kwamba huyo padri kijana anafaa sana kuchochea imani mkoani Andalusia, na baada ya kumshauri sana alimfanya akubali kuacha mpango wa kwenda Amerika.

Basi, akabaki na Hernando, akishiriki naye maisha ya ufukara na sala na kuendelea na masomo yake katika Chuo cha Mtume Thoma. Labda ndipo alipopewa jina “Mwalimu”, lililoendelea kutumika kwa ajili yake hata kisha kufa.

Mtume wa Andalusia[hariri | hariri chanzo]

Alianza kuhubiri tarehe 22 Julai 1529, akapata mara umaarufu.

Katika miaka tisa aliyofanya utume huko Andalusia, mahubiri yake yote yalisikilizwa na umati wa watu waliobanana.

Hata hivyo, nguvu ya maneno yake kwa ajili ya urekebisho na dhidi ya mwenendo wa matabaka ya juu katika jamii ilisababisha mwaka 1531 afikishwe mbele ya Hakimu mkuu wa Seville.

Shtaka lilikuwa kwamba alizidisha hatari ya kiroho inayotokana na utajiri na hivyo kuwafungia matajiri milango ya mbinguni. Lakini aliweza kujitetea vizuri na kuachiliwa mwaka 1533 baada ya kufungwa gerezani zaidi ya mwaka mmoja, akateuliwa kuhubiri tena[5]kwa watu wa kawaida na kwa wale wenye mamlaka.

Akiwa gerezani alianza kuandika kitabu chake bora; pia alijaliwa kuzama katika fumbo la upendo wa Mungu uliofunuliwa kumpitia Yesu Kristo na katika fadhili ambazo binadamu wamepata kutoka kwa Mkombozi huyo.

Tangu hapo hizo mbili zikawa nguzo za maisha yake ya Kiroho na mada kuu za mahubiri yake, pamoja na kutangaza nafasi ya kwanza ya neema, inayohimiza matendo mema, na kuhamasisha tumaini kwa Mungu na itikio kwa upendo wake unaoita wote wawe watakatifu.

Kama wanasala wengine wa Hispania wakati huo, alishukiwa mara kadhaa kuhusika na Alumbrados, waliotazamwa kama wazushi.

Urekebisho wa mapadri nchini Hispania[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na kwamba Yohane aliwahi kuelekeza wote kwenye utakatifu, alichangia sana ustawi wa teolojia ya upadri, akisababisha kati ya wanajimbo juhudi kubwa za Kiroho na kuathiri waandishi waliofuata. Kiini cha mafundisho yake kuhusu jambo hilo ni kwamba “wakati wa Misa sisi (mapadri) tunajiweka juu ya altare katika nafsi ya Kristo ili kutekeleza kazi ya Mkombozi mwenyewe”; hiyo inadai kutimiza kwa unyenyekevu upendo wa kibaba na wa kimama wa Mungu, kwa hiyo kuwa na mtindo wa maisha wa pekee.

Hivyo anakumbukwa hasa kwa kurekebisha Kanisa kwa kuboresha maisha ya mapadri nchini Hispania, ingawa hakuanzisha shirika lolote kwa ajili yao.[5]Wakleri watakatifu ni haja ya msingi kwa urekebisho wa Kanisa, na hilo linadai uchambuzi makini na malezi ya kufaa kwa walioelekea upadri. Hivyo alihimiza uanzishaji wa seminari na wa vyuo maalumu kwa elimu ya Biblia. Mapendekezo hayo yalikuja kuathiri Kanisa lote.

Ni kwamba, kwa kutia maanani sana malezi, alianzisha mwenyewe vyuo kadhaa ambako wanafunzi wake walijitosa kufundisha vijana.[6] Baada ya Mtaguso wa Trento, hivyo vikawa seminari kadiri ya maagizo ya mtaguso huo.

Umuhimu wa pekee kati ya mafanikio yake unacho Chuo kikuu cha Baeza kilichoanzishwa naye mwaka 1538 kwa hati ya Papa Paulo III[7] na ambacho akawa gombera wake wa kwanza[8]hata bila kufundisha mwenyewe, isipokuwa Biblia kwa walei, watawa na wakleri, kwa sababu alitamani sana ijulikane na wote.

Chuo hicho katika karne zilizofuata kikawa kielelezo kwa seminari na kwa shule za Wajesuiti, ambao wanamheshimu kwa pekee kwa kuwasaidia kustawi Hispania hasa kwa kuelekeza kwao wanafunzi wake bora 30 hivi.[5] Mwenyewe alitamani kujiunga nao, asiweze ingawa alikaribishwa na Ignasi wa Loyola aliyemheshimu sana.

Kati ya watakatifu rafiki zake kuna pia padri Mfransisko Petro wa Alcantara na maaskofu Thoma wa Villanova na Yohane wa Ribera.

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Baada ya utume wake wa miaka tisa mkoani Andalusia, alirudi Seville, ambako aliondoka tu kwa kazi kubwa zaidi huko Cordoba, alipojiunga na jimbo moja kwa moja, Granada (1536), alipohitimu masomo ya chuo kikuu, Baeza, Montilla na Zafra.

Miaka kumi na nane ya mwisho aliugua mfululizo, kutokana na ugumu wa maisha na wa kazi alizofanya kwa miaka arubaini. Mwaka 1554 alihamia nyumba ndogo ya Montilla, alipoendeleza utume wake kwa kuandika barua nyingi na vitabu kadhaa.

Askofu mkuu wa Granada alitaka aende naye kama mtaalamu wa teolojia kwenye vikao vya mwisho vya Mtaguso wa Trento, lakini afya haikumruhusu kusafiri. Hata hivyo “Memoriales” (“Kumbukumbu”) alizoziandika kwa ajili hiyo, ziliathiri sana mtaguso huo.

Alifariki tarehe 10 Mei 1569 asubuhi huko Montilla akishika msalaba na kuzungukwa na wafuasi na marafiki.

Kati ya mengineyo, Yohane alipendekeza ianzishwe mahakama ya kimataifa ya usuluhishi ili kuepa vita, pia alibuni na kusajili vifaa kadhaa vya uhandisi.

Akiishi kifukara sana, alijitosa hasa kuhimiza maisha ya Kikristo kati ya wale waliomfuata kila mahali ili kumsikiliza.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

Wale wote walioongozwa naye kiroho walitambua mapema kipaji chake cha pekee cha kupenya fumbo la Kristo, kwamba baraka zote zinatujia kwa njia yake; kwamba tunachuma matunda ya ukombozi kadiri tunavyoungana naye; kwamba muungano huo unaanza na imani na ubatizo na kukamilishwa na ekaristi; na kwamba kujitoa kabisa kwake kunazaa ndani mwetu tumaini na furaha.

“Fungua moyo wako mdogo upokee ile pumzi ya upendo ambao kwao Baba anatupatia Mwanae, na kwa njia yake anajitoa kwetu pamoja na Roho Mtakatifu na vingine vyote”.

Maandishi yake yalikusanywa huko Madrid miaka 1618, 1757, 1792 na 1805; yote yanang’aa kwa kufafanua mada kwa dhati, kwa mbinu rahisi na kwa mifano mingi; kati yake, maarufu zaidi ni: "Audi Filia, et vide" (“Sikiliza, binti, na uone”) kuhusu ukamilifu wa Kikristo, na "Barua za Kiroho" kwa wafuasi wake[9]zilizotafsiriwa mapema katika lugha mbalimbali.

Pia kuna katekisimu kwa watoto na watu wazima inayoitwa “Mafundisho ya Kikristo”, “Insha juu ya Upendo wa Mungu”, inayoshirikisha dhati ya fumbo la Kristo, “Insha juu ya Upadri”, “Maelekezo kuhusu Urekebisho”, “Hotuba”, “Maongezi” na ufafanuzi wa vitabu mbalimbali vya Biblia, kama vile barua kwa Wagalatia na ile ya kwanza ya Yohane.

Katika kusoma Biblia alitumia na kulinganisha tafsiri mbalimbali, alichunguza maneno yenyewe na maana yake ya Kiroho, pamoja na kutegemea sala na kuwa na uzoefu na maelezo ya mababu wa Kanisa.

Pengine hakuandika zaidi kwa kuogopa hukumu kali za Mahakama ya Imani ya wakati ule.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Pope to proclaim St John of Avila Doctor of the Universal Church. News.va. Holy See (20 Agosti 2011). Iliwekwa mnamo 21 Agosti 2011.
  2. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
  3. Wilke 2003, p. 963
  4. Domínguez Ortiz 1992
  5. 5.0 5.1 5.2 Wilke 2003, p. 964
  6. Smith 1913
  7. Introducción Histórica Archived 26 Septemba 2011 at the Wayback Machine., Universidad de Jaén, 2005-09-26. Accessed online 2010-02-05.
  8. José Biedma, Juan de Ávila y la Universidad de Baeza, cibernous.com. Accessed online 2010-02-05.
  9. St. John of Ávila 1904

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

      .

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons