Mtaguso wa Trento

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mtaguso ukifanyika katika kanisa kuu la Trento.

Mtaguso wa Trento (uliofanyika kwa kwikwi kuanzia mwaka 1545 hadi 1563), unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa mtaguso mkuu wa 19.

Mtaguso huo, uliochukua muda mrefu kuliko yote ya historia, ulieneza urekebisho wa Kanisa na kuchukua msimamo kuhusu mafundisho ya Waprotestanti waliojitokeza katika hiyo karne ya 16.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Mtu wa kwanza kulilia mtaguso ambao uamue kati yake na papa alikuwa Martin Luther (1517): huko Ujerumani ombi lake liliungwa mkono na wengi, pamoja na kaisari Karolo V aliyeuona kuwa njia ya kurekebisha Kanisa lakini pia ya kujiimarisha kimamlaka. Ndiyo sababu kuu iliyomfanya Papa Klementi VII (1523-1534), aliyesimama upande wa Ufaransa, kukataa kabisa kuuitisha.

Mchoro wa Sebastiano Ricci, Papa Paulo III ana ono la Mtaguso wa Trento. 1687-1688, Piacenza, Museo Civico.

Wazo hilo lilipata nguvu tena chini ya mwandamizi wake, Papa Paulo III (1534-1549), ambaye mwaka 1536 aliitia kwanza Mantova halafu Vicenza maaskofu na maabati wote, pamoja na wafalme wadogo wengi wa Dola takatifu la Kijerumani.

Baada ya juhudi mbalimbali kushindikana, mwaka 1542 uamuzi ulifikiwa wa kuitisha mtaguso huko Trento kwa sababu ni mji wa Italia lakini ulikuwa ndani ya mipaka ya dola hilo. Hatimaye (Novemba 1544) papa aliweza kutoa hati ya kuitisha mtaguso inayoitwa Laetare Jerusalem.

Mtaguso ulifunguliwa rasmi tarehe 13 Desemba 1545 katika kanisa kuu la Mt. Vigilio.

Mtaguso wa Trento katika kanisa la Santa Maria Maggiore (Museo Diocesano Tridentino).

Mwanzoni mtaguso ulikuwa na maaskofu wachache, karibu wote kutoka Italia, ukatawaliwa na wajumbe wa Papa. Kati ya makardinali wapya (Contarini, Sadoleto, Carafa, Fisher na huyo Pole) wengi walipenda urekebisho.

Zilijadiliwa na kupitishwa hasa dogma dhidi ya mafundisho ya Waprotestanti, kama vile kuhusu utakaso na wokovu. Pamoja na kupitisha tafsiri rasmi ya Biblia katika Kilatini iliyo maarufu kwa jina la Vulgata, kati ya maamuzi muhimu zaidi upo ule wa kudai maaskofu waishi katika majimbo yao ili kufanya uchungaji uliowapasa.

Baada ya mtaguso kuhamishiwa Bologna, Papa Paulo III aliusimamisha mnamo Septemba 1549.

Papa Julius III (1550-1555) aliuitisha tena kuanzia tarehe 1 Mei 1551 na zikatolewa hati juu ya sakramenti za Ekaristi, Kitubio na Mpako wa wagonjwa.

Polepole waliohudhuria waliongozeka, wakiwemo Waprotestanti wengi pia, wakidai wanateolojia wao wawe na haki ya kupiga kura na hati zilizokwishatolewa zifutwe. Ndipo ilipoonekana wazi kwamba tofauti katika imani ni kubwa mno.

Majeshi ya Kiprotestanti yalipokaribia Trento, Papa alikubali kusimamisha tena mtaguso tarehe 28 Aprili 1552.

Sehemu ya mwisho ya mtaguso baada ya kuitishwa ilichelewa kuanza hadi tarehe 18 Januari 1562, tena ilikabili matatizo mengi, lakini iliokolewa na kutawaliwana askofu wa Milano Karolo Borromeo, mpwa wa Papa Pius IV (1559-1565) aliyemalizia haraka mtaguso wakiwemo wajumbe 255.

Katika sehemu hiyo yalitolewa mafundisho rasmi kuhusu Misa, Daraja takatifu na Ndoa, Toharani, sala kwa watakatifu, heshima kwa masalia na rehema.

Pia Kanisa la Roma lilikubaliwa kama mama na mwalimu wa makanisa yote. Maaskofu wote walitakiwa kuahidi utiifu kwa Papa, ambaye peke yake ana haki ya kuitisha mtaguso mkuu. Kwa msingi huo, mtaguso ulimuachia Papa kuthibitisha maamuzi yote, naye alifanya hivyo bila ya kujali upinzani wa maofisa wake huko Roma.

Hivyo, mwishoni, maamuzi mbalimbali yaliachwa mikononi mwa Papa na ofisi zake, yakachukuliwa miaka iliyofuata; kati yake, urekebisho wa Breviari na Misale, kwa kusawazisha liturujia za majimbo ya magharibi (isipokuwa chache, kama ile ya Jimbo la Milano na ya Jimbo la Lyon) kulingana na mapokeo ya Roma. Halafu ikatolewa Katekisimu ya Trento na Orodha ya vitabu vilivyokatazwa (Index librorum prohibitorum).

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]