Nenda kwa yaliyomo

Vulgata

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Toleo la Malmesbury.

Vulgata (kwa Kilatini ya umati yaani ya kawaida) ni tafsiri maarufu zaidi ya Biblia ya Kikristo katika lugha ya Kilatini. Ilitolewa kuanzia mwaka 382 hadi 405 na Hieronimo kwa agizo la Papa Damaso I ili ichukue nafasi ya tafsiri mbalimbali zilizotangulia ambazo hazikuridhisha.

Kuanzia karne ya 8 hadi ya 9 ilikuwa Biblia ya kawaida katika maeneo yaliyokuwa chini ya Kanisa Katoliki ikitazamwa kuwa toleo pekee lililostahili kutumiwa.

Matengenezo ya Kiprotestanti yalichukua jukumu la kusambaza Biblia katika tafsiri ya lugha yoyote yakitegemea nakala za zamani katika lugha zake asili, yaani Kiebrania, Kiaramu na Kigiriki. Lakini nakala zilizojulikana wakati ule hazikuwa za zamani kuliko zile alizozitumia Hieronimo kutengenezea Vulgata; kinyume chake zilikuwa na makosa mengi ambayo yakaja kurekebishwa hasa katika karne ya 20 kutokana na maendeleo ya utaalamu.

Upande wa Kanisa Katoliki Mtaguso wa Trento ulitangaza Vulgata kuwa tafsiri rasmi ya Biblia na kuwa haina makosa upande wa imani na maadili. Tamko hilo halikuwa na maana ya kuwa tafsiri hiyo haiwezi kuboreshwa.

Kwa kuwa mtaguso huo ulisisitiza kuwa "toleo la kale la Vulgata, lililokubaliwa na Kanisa lenyewe kwa kulitumia tangu karne nyingi, linatakiwa kutazamwa toleo rasmi kwa usomaji wa hadhara, mabishano, mahubiri na ufafanuzi" ikawa desturi kwa Wakatoliki kutoa tafsiri rasmi katika lugha mbalimbali kutokana na Vulgata badala ya kutumia lugha asili. Hivyo Wakatoliki walijikuta wanatumia tafsiri zinazolingana na nakala ya kale zaidi kuliko tafsiri za Waprotestanti, ingawa hao wa pili walikuwa na utaalamu mkubwa zaidi.

Mwaka 1943 Papa Pius XII alihimiza Wakatoliki kutoa tafsiri mpya kutoka lugha hizo asili, kama zile zilizofanywa na Wakristo wengine tangu zamani.

Mtaguso wa Pili wa Vatikani uliamua tafsiri hiyo iangaliwe upya na tangu mwaka 1979 "Nova Vulgata" (yaani Vulgata Mpya) imetolewa kama tafsiri rasmi ya Kilatini kwa Kanisa Katoliki lote ambayo iongoze katika kutafsiri katika lugha nyingine kutoka zile asili.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Vulgata kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.