Nenda kwa yaliyomo

Amani ya Augsburg

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wajumbe wa madola ya Ujerumani wakijadili huko Augsburg uwezekano wa amani ya kidini nchini.

Amani ya Augsburg ni mapatano yaliyofikiwa mwaka 1555 ili kumaliza Vita vya Schmalkald (1546-1547), vilivyoendeshwa na Karolo V, Kaisari wa Dola Takatifu la Kiroma dhidi ya maeneo ya Walutheri yaliyokuwa ndani ya dola hilo kubwa la Ujerumani.

Vililenga kuwalazimisha watawala wadogo waliowaunga mkono Walutheri wafute matengenezo yote.

Mwanzoni alishinda (20 Julai 1547); kwenye Bunge la Augsburg (1547-1548) alidai Walutheri wakubali kuwa chini ya maaskofu na Papa wa Kanisa Katoliki. Ingawa aliruhusu ndoa ya mapadri na kupokea ekaristi kwa maumbo yote mawili (mkate na divai), maitikio hayakuwa mazuri hata kidogo: kukawa na vurugu kubwa.

Mwaka 1552, baada ya njama ya watawala hao dhidi ya Karolo V, vilianza tena vita ambavyo vilimlazimisha kukimbia Austria. Hatimaye watawala Walutheri walipatana na mwanae, mfalme Ferdinand III. Hivyo jaribio la kufuta Ulutheri kijeshi lilishindikana kabisa.

Vita vilimalizika mwaka 1555 kwa amani ya Augsburg. Mapatano hayo yalilenga kuwezesha wananchi wenye imani tofauti waishi katika taifa lilelile. Watawala walipewa haki ya kuwachagulia madhehebu ya dini raia wao. Wasiokubali kufuata imani ya mtawala, walipewa tu haki ya kuhamia eneo lingine ambapo mtawala wake alikuwa na imani yao.

Hivyo katika Dola la Kijerumani yalikubalika rasmi maeneo yaliyoshikilia Ungamo la Augsburg na yale yaliyobaki katika Kanisa Katoliki, lakini si wenye imani tofauti na hizo mbili, kama vile Wareformati na Waanabaptisti.

Amani ya Augsburg kwanza ilifaulu kuleta mahusiano imara upande wa siasa, lakini baadaye haikuweza kuzuia mlipuko wa vita vikali vya karne XVII: vita vya miaka 30 (1618-1648).

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Amani ya Augsburg kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.