Fransisko wa Sales
Fransisko wa Sales (Thorens-Glières, leo nchini Ufaransa, 21 Agosti 1567 - Lyon, Ufaransa, 28 Desemba 1622) alikuwa askofu wa Kanisa Katoliki kwa jimbo la Geneva (Uswisi).
Akijumlisha ndani mwake matunda bora ya karne XVI, ni kati ya watu muhimu zaidi katika Urekebisho wa Kikatoliki na katika teolojia ya maisha ya kiroho.
Mchungaji halisi, alirudisha katika Kanisa Katoliki Waprotestanti wengi, na kuwafundisha kwa maandishi yake Wakristo wamheshimu na kumpenda Mungu. Pamoja na Yoana Fransiska wa Chantal alianzisha shirika la Ziara.
Kwa ajili hiyo anaheshimiwa kama mtakatifu na mwalimu wa Kanisa. Pia kama msimamizi wa waandishi wa habari, watunzi na wanafasihi, magazeti ya Kikatoliki na mabubu-viziwi.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Januari[1].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Utoto na ujana
[hariri | hariri chanzo]Fransisko, mtoto wa kwanza wa mtawala wa Boisy, sharifu wa Savoy, alizaliwa Thorens-Glières, leo nchini Ufaransa, tarehe 21 Agosti 1567..
Alipata mapema elimu bora ambayo aliikamilisha akisoma sheria za Kanisa na za serikali.
Baba yake, akimtaka awe mwanasheria, ndiye aliyemtuma kwenye chuo kikuu cha Padova (Italia) ambako Fransisko alipata digrii, lakini pia wito wa upadri.
Baada ya kurudi kwao, aliteuliwa kuwa wakili wa Seneti ya Chambéry.
Katika ujana wake safi, tafakuri juu ya mafundisho ya Agostino wa Hippo na ya Thoma wa Akwino zilimfanya afadhaikie wokovu wake kuhusiana na suala la [[uteule] lililojadiliwa sana wakati huo. Alisali kwa bidii, lakini wasiwasi kuhusu hali yake mbele ya Mungu ulimfanya ashindwe kwa wiki kadhaa hata kula na kulala, isipokuwa kwa shida.
Katika kilele cha jaribu hilo, aliingia katika kanisa la Wadominiko la Paris akasali moyo wazi: “Ee Bwana, unayeshika yote mkononi mwako na ambaye njia zako ni haki na ukweli, lolote litakalotokea, lolote ulilonipangia… nitakupenda ee Bwana uliye daima hakimu mwenye haki na Baba mwenye huruma. Nitakupenda hapa, Mungu wangu, nami nitatumainia daima huruma yako na nitarudia daima sifa zako… Ee Bwana Yesu, utakuwa daima tumaini langu na wokovu wangu katika nchi ya walio hai”.
Hivyo akiwa na umri wa miaka 20 alipata amani moyoni kwa kujiachia katika upendo wa Mungu, bila kudai chochote zaidi wala kumuuliza atamfanyia nini: ndiyo siri ya maisha yake yote.
Upadri wake
[hariri | hariri chanzo]Kisha kushinda upinzani wa baba yake, alisoma teolojia huko Paris, akapewa upadrisho tarehe 18 Desemba 1593, akatumwa kwenye eneo la Chablais, lililotawaliwa na madhehebu ya Yohane Calvin.
Huko alijitosa hasa kuhubiri, akitumia mbinu ya majadiliano. Alipoona itikio hafifu, alitambua umuhimu wa uchapaji akabuni uandishi wa «matangazo» yaliyomwezesha kuwafikia hata watu wa mbali. Alikuwa anayabandika kutani na kuyasambaza nyumbani kwa watu kupitia chini ya milango. Hata hivyo matunda hayakuwa mengi.
Akiwa na nia ya kuzuia uenezi wa Uprotestanti kati ya Wakatoliki, na kurudisha wengi iwezekanavyo katika ushirika wa Kanisa, aliongea na askofu wa Geneva ili kumuomba amtume akahubiri katika mji huo, makao makuu ya Wakalvini.
Kisha kufika alijadiliana na Waprotestanti ili kuwarudisha kwenye umoja kamili na Kanisa la Roma.
Wazo lake lilielekea daima walei, ili kuwapa mafundisho na miongozo ya maisha ya Kikristo.
Juhudi zake na mafanikio aliyopata kwa ubora wa mahubiri yake vilifanya ateuliwe kuwa askofu mwandamizi wa Geneva mwaka 1599, akiwa na umri wa miaka 32 tu.
Uaskofu
[hariri | hariri chanzo]Baada ya miaka mitatu akawa askofu wa jimbo hilo ambapo alijitahidi kutekeleza maagizo ya Mtaguso wa Trento.
Lakini mji kwa jumla ulibaki mikononi mwa Wakalvini, hivyo ilimpasa aishi Annecy, katika utawala wa Savoy.
Kama mchungaji wa jimbo fukara lenye matatizo katika mazingira ya milimamilima, aliandika: “Nimemkuta Mungu mtamu na mpole katika milima yetu mirefu mizuri, ambapo watu wengi sahili wanampenda na kumuabudu kwa ukweli na unyofu”. Hata hivyo athari ya maisha na mafundisho yake ilienea sana wakati huo na baadaye kutokana na utimilifu na utamu wake.
«Kama ni kukosea, napenda kukosea kwa kuzidisha wema kuliko ukali»: kauli yake hiyo inaeleza alivyoweza kujivutia watu wengi. Kuliko hoja za kupinga uzushi, ni ufafanuzi wake wa upendo wa Mungu uliowafanya Wakalvini wengi wajiunge na Kanisa Katoliki na hatimaye kurudisha Chablais nzima.
Walisema juu yake, “Jinsi gani Mungu ni mwema, ikiwa Fransisko ni mwema hivyo!”
Katika nafasi mbalimbali alitumiwa pia kama balozi na mpatanishi wa jamii.
Mstaarabu na mwenye elimu kubwa, alipata umaarufu hasa kwa kuongoza kiroho watu wengi (zimetubakia barua zake 2000 hivi!); kati yao watakatifu Vinsenti wa Paulo na Yoana Fransiska wa Chantal, aliyemsaidia kuanzisha Shirika la Maonano. Katika mpango wake, uliozuiwa kwa kuwa nyakati hazikuwa tayari, masista hao hawakutakiwa kubanwa na ugo bali kutembelea na kusaidia mafukara na wagonjwa. Aliwaelekeza waishi kweli kwa Mungu tu katika usahili na unyenyekevu, wakitenda vizuri kabisa mambo ya kawaida: “Nataka mabinti wangu wasiwe na kipeo kingine isipokuwa kumtukuza Bwana kwa unyenyekevu wao”.
Huko Thonon, ili kueneza utakatifu kati ya Wakristo wote,, alianzisha pia tawi la Oratorio ya mtakatifu Filipo Neri na “chuo kikuu” cha kazi.
Heshima baada ya kifo
[hariri | hariri chanzo]Alitangazwa na Papa Alexander VII kuwa mwenye heri tarehe 8 Januari 1662, na mtakatifu tarehe 19 Aprili 1665. Halafu Papa Leo XIII mwaka 1887 alimtangaza kuwa mwalimu wa Kanisa.
Sala zake
[hariri | hariri chanzo]Ee Mungu wangu, nakutolea siku hii.
Nakutolea sasa mema yote nitakayotenda na ninakuahidi nitapokea kwa upendo wako magumu yote yanayonikabili.
Unisaidie kuenenda siku hii namna inayokupendeza.
Ee Bwana, mimi ni wako, tena natakiwa kuwa wako tu,
si wa mwingine yeyote.
Roho yangu ni wako, nayo inatakiwa iishi kwa njia yako tu.
Utashi wangu ni wako, nao unatakiwa kupenda kwa ajili yako tu.
Napaswa kukupenda kama asili yangu kuu, kwa kuwa natoka kwako.
Napaswa kukupenda kama lengo na pumziko langu, kwa kuwa nipo kwa ajili yako.
Napaswa kukupenda kuliko nafsi yangu, kwa kuwa nafsi yangu inatoka kwako.
Napaswa kukupenda kuliko mimi mwenyewe, kwa kuwa mimi mzima ni wako na ndani yako. Amina.
Maandishi yake bora
[hariri | hariri chanzo]Kati ya vitabu alivyotunga, muhimu zaidi ni "Kuingia maisha ya juhudi" na "Kitabu cha upendo wa Mungu", ambavyo ni kati ya vitabu bora vya kidini vya nyakati zote na vinaelekeza walei pia kufuata njia ya utakatifu, yaani ya upendo wa Mungu, ambaye alimtambulisha kama “Mungu wa moyo wa binadamu”.
Katika kitabu “Kuingia Maisha ya Juhudi” Fransisko alitoa wito ulioonekana wa kimapinduzi kwa wakati ule: kila mtu kuwa kabisa mali ya Mungu huku akiishi ulimwenguni na kutimiza kitakatifu majukumu maalumu ya hali yake. “Nia yangu ni kufundisha wanaoishi mijini, katika ndoa na ikuluni” kwa sababu moyo wa ibada unatakiwa kung’aa kila mahali: juu ya viti vya enzi vya wafalme, katika mahema ya majemadari, katika mahakama na ofisi za ushuru, viwandani na machungani.
Kipeo cha binadamu mwenye umoja wa dhati kilionyeshwa katika ulinganifu wa sala na utendaji ulimwenguni, katika kulenga ukamilifu bila kuacha maisha ya kawaida, kwa msaada wa neema ya Mungu ambayo inampenya mtu bila kuangamiza umbile lake, bali kwa kulitakasa na kuliinua hadi vilele vya Kimungu.
Miaka baadaye, “Kitabu cha Upendo wa Mungu” kilimpa Mkristo aliyekomaa Kiroho fundisho kamili zaidi, kikianzia mtazamo sahihi kuhusu binadamu: akili yake, yaani roho kadiri inavyoweza kufikiri, inaonekana humo kama jengo zuri kabisa, kama hekalu lenye nyua mbalimbali kandokando ya kiini ambacho ni “kilele cha roho yetu” na ambamo akili, kisha kupanda ngazi zote, “inafumba macho yake” na ujuzi unakuwa mamoja na upendo.
Mtazamo huo mpana hauna mpasuko: “Binadamu ndiye ukamilifu wa ulimwengu; roho ndiyo ukamilifu wa binadamu; mapendo ndiyo ukamilifu wa roho, na upendo ndio ukamilifu wa mapendo”. Hivyo safari ya kumuendea Mungu inaanza kwa kutambua “elekeo la kimaumbile” lililomo moyoni mwa mtu - hata kama ni mkosefu - la kumpenda Mungu kuliko yote.
Akifuata Biblia, Fransisko anazungumzia muungano wa Mungu na mtu kwa mifano mbalimbali ya mahusiano: Baba, Bwana, mume na rafiki, ambaye ana sifa za mama na nesi mwenye hisani na ni jua linalotambulishwa na usiku pia.
Mungu huyo anamvuta binadamu kwake kwa vifungo vya upendo, si kwa shuruti: “Upendo hauna wafungwa wala watumwa, bali unaleta yote chini yake kwa nguvu ya kupendeza hivi, hata hakuna chenye nguvu kuliko upendo, lakini pia hakuna kitamu kuliko nguvu yake”.
Kwa sababu hiyo alimuandikia Yoana Fransiska wa Chantal: “Hii ndiyo kanuni ya utiifu wetu, ninayokuandikia kwa herufi kubwa: FANYA YOTE KWA UPENDO, HATA MOJA KWA SHURUTI; UPENDE UTIIFU KULIKO KUOGOPA UKAIDI. Nakuachia roho ya uhuru, si ile inayokataa utiifu, ambayo ndiyo uhuru wa kidunia, bali uhuru ule unaokataa matumizi ya nguvu, mahangaiko na mafadhaiko”.
Ni roho hiyo iliyoathiri malezi na maisha ya Kiroho ya wengi katika karne zilizofuata: bila hiyo tusingepata “malezi kinga” ya Yohane Bosco wala “njia ndogo” ya Teresa wa Mtoto Yesu.
Kwa ajili hiyo anahesabiwa kama baba wa maisha ya kiroho ya nyakati zetu, yaliyofuatwa na watakatifu wengi, hasa Yohane Bosco, mwanzilishi wa shirika linaloitwa la Wasalesiani kwa heshima yake.
Alifariki Lyon, Ufaransa, tarehe 28 Desemba 1622.
Orodha ya maandishi yake
[hariri | hariri chanzo]- Introduction a la vie devote par S. François de Sales eveque et prince de Geneve, Derniere edition, revue, corrigee, & augmentee, A Lyon: chez Louis Servant, 1608;
- Traicte de l'amour de Dieu par François de Sales euesque de Geneue, A Lyon, Chez Pierre Rigaud, rue Merciere, au coing de rue Ferrandiere, a l'enseigne de la fortune, 1620;
- Les epistres spirituelles du bien-heureux François de Sales euesque & prince de Geneue, ... Diuisees en sept liures. Le 1. Contenant celles qu'il a escrit aux papes, cardinaux, euesques, roys, princes. Le 2. Plusieur beaux enseignemens... Recuillies par messire Loys de Sales, preuost de l'eglise de Geneue, A Lyon, pour Vincent de Coeursilly en rue Tupin a la fleur de Lis, 1628;
- Lauro Aime Colliard, Une lettre inedite de Saint François de Sales concernant la bastonnade d'un jeune homme fort eveille, Roma, LAS, 2002, estratto da "Salesianum", a. 64. (2002), pp. 525–543.
Kwa Kiswahili
[hariri | hariri chanzo]- MT. FRANSISKO WA SALES, Mwanzo wa Maisha ya Kumcha Mungu – tafsiri ya Fr. Severin L. Njako na Cornelius D. Nsalanga – ed. Vincentians – Mbinga 1996 – ISBN 9976-67-091-5
Maandishi yake katika mtandao
[hariri | hariri chanzo]- Better Translation of the book, "Introduction to the Devout Life".
- Christian Classics Ethereal Library Introduction to the devout life.
- Set Your Heart Free Ilihifadhiwa 5 Desemba 2010 kwenye Wayback Machine., 30 days with a great spiritual teacher, edited by John Kirvan.
- Spiritual Conferences Ilihifadhiwa 22 Januari 2010 kwenye Wayback Machine..
- The Catholic Controversy Ilihifadhiwa 27 Septemba 2007 kwenye Wayback Machine..
- Treatise on the Love of God.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Catholic Encyclopedia: St. Francis de Sales
- International Commission on Salesian Studies All about St. Francis de Sales worldwide
- Founder Statue in St Peter's Basilica
- Francis de Sales bio at Catholic.org