Askofu mwandamizi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Askofu mwandamizi au kwa maneno mengine "askofu mrithi"(kwa Kiingereza "coadjutor bishop") ni askofu aliyeteuliwa kurithi madaraka kamili ya kuongoza na kusimamia jimbo endapo askofu aliyeko madarakani ataacha kusimamia jimbo hilo kufuatia sababu yoyote ile, kama vile kujiuzulu, kustaafu au kufariki.

Katika Kanisa Katoliki askofu mwandamizi huteuliwa na Papa kama wanavyoteuliwa maaskofu wengine na anatarajiwa kumsaidia askofu wa jimbo katika shughuli za usimamizi wa jimbo kulingana na mwongozo wa Kanisa Katoliki chini ya usimamizi wa askofu kiongozi.

Kipindi hiki askofu mwandamizi anakuwa hana madaraka kamili ya kuongoza au kusimamia jimbo ila humsaidia askofu aliyepo madarakani, lakini huyo wa mwisho katika kuchukua uamuzi wake ni lazima amsikilize mwandamizi wake, kwa kuwa ndiye atakayepaswa kuendesha jimbo baadaye, hivyo maamuzi hayo yanaweza yakamsumbua.

Pengine askofu mwandamizi anapewa na Papa mamlaka ya pekee, hasa kutokana na hali ya askofu wa jimbo au ya jimbo lenyewe.

Upande wa sakramenti askofu mwandamizi ni askofu kamili kama walivyo maaskofu wengine na huweza kutoa sakramenti zote zikiwa ni pamoja na daraja takatifu ila atahitaji ruhusa ya askofu wa jimbo ili kufanya hivyo.

Tofauti na "askofu msaidizi" (kwa Kiingereza "auxiliary bishop"), askofu mwandamizi hurithi mara moja kiti cha askofu kiongozi endapo askofu wa jimbo ataondoka madarakani kwa namna yoyote ile, hivyo hahitaji kuteuliwa tena bali kusimikwa tu.