Filipo Neri
Filipo Neri (Firenze 22 Julai 1515 - Roma 27 Mei 1595), alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi wa shirika la Waoratori.
Ni maarufu kama "mtume wa Roma" kutokana na kazi yake bora aliyoifanya katika mji huo katika karne ya 16. Akijitahidi kuepusha vijana na dhambi, alianzisha oratori, vilipofanyika masomo ya kiroho, nyimbo na matendo ya huruma. Aling'aa kwa upendo wake kwa jirani, kwa unyofu wa Kiinjili, kwa furaha ya kudumu, kwa bidii ya pekee na kwa ari katika kumtumikia Mungu[1].
Alitangazwa na Papa Paulo V kuwa mwenye heri tarehe 11 Mei 1615, halafu tarehe 12 Machi 1622 Papa Gregori XV alimtangaza mtakatifu.
Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 26 Mei[2].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Alikuwa mtoto wa mwisho wa Francesco, mwanasheria, na mke wake Lucrezia wa Mosciano.
Filipo alilelewa kwa makini, akapokea mafunzo yake ya kwanza kwa Wadominiko wa konventi maarufu ya San Marco. Baadaye alizoea kusema maendeleo yake yalitegemea hasa wawili kati yao, Zenobio de' Medici na Servanzio Mini.
Akiwa na umri wa miaka 18,[3] alitumwa kwa ndugu wa mzazi wake, Romolo, mfanyabiashara tajiri huko San Germano, karibu na Monte Cassino. Lengo lilikuwa kumsaidia na baadaye kumrithi.
Kweli alijipatia imani yake, lakini muda mfupi baadaye alipata wongofu akaacha mipango ya kidunia akahamia Roma mwaka 1533.[4]
Utume wake mjini Roma ulivyoanza
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kuwa kwa miaka miwili mlezi nyumbani mwa Galeotto Caccia, aliendelea na masomo yake mwenyewe kwa miaka mitatu chini ya Waagustino.[5]
Halafu alianza utume wake kati ya wagonjwa, mafukara na hata makahaba.
Mwaka 1538 alianza utume wa nyumba kwa nyumba uliomfanya kuwa maarufu. Akitembelea watu mjini kote ili kuongea nao kirafiki ili kuwaleta kwenye mazungumzo ya kidini.
Chama cha Utatu Mtakatifu
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1548 alianzisha pamoja na muungamishi wake, padri Persiano Rossa, chama cha Utatu Mtakatifu [6], ambacho lengo lake kuu lilikuwa kuhudumia maelfu ya watu waliohiji Roma hasa wakati wa Jubilei, pamoja na walioruhusiwa na hospitali kabla hawajapona vizuri.
Wanachama walikutana kusali katika kanisa la San Salvatore in Campo, ambapo lilikuwa la kwanza kufuata ibada ya Saa arubaini kwa sakramenti ya Ekaristi.
Shirika la Oratorio
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1551 alipewa daraja ndogo zote, akapata ushemasi mdogo na ushemasi, na hatimaye tarehe 23 Mei alipadrishwa.
Alitarajia kwenda India kama mmisionari, lakini marafiki wake walimshauri aendelee na utume mjini.
Basi, alihamia pamoja na wenzake kadhaa katika hospitali ya San Girolamo della Carità, ambapo alianza kujaribu, mwaka 1556, uanzishaji wa shirika la Oratorio.
Mpango wa awali ulikuwa tu mikutano ya jioni katika ukumbi ulioitwa kwa Kiitalia Oratorio, yaani chumba cha sala, ili kusali, kuimba, kusoma Biblia, pamoja na maandishi ya maBabu wa Kanisa na habari za wafiadini, halafu kupata fundisho la kidini au kujadiliana juu ya mada ya namna hiyo.
Tamasha za kimuziki (kutokana na historia ya wokovu) ziliitwa oratorio kwa sababu hiyo.
Mpango huo ulifaulu na kuenea mjini kote kwa mahubiri katika makanisa yote saa za jioni, jambo jipya kabisa.
Pamoja na hayo, Filipo alitumia muda mwingi kuadhimisha sakramenti ya kitubio na kufanya wengi waongoke.[7]
Mwaka 1564 Wafirenze wenzake waliomuomba ahame kanisa hilo la kwanza ili kusimamia lile jipya la kwao, San Giovanni dei Fiorentini[8]. Kwanza alisita, lakini kwa kibali cha Papa Pius IV alikubali bila kuacha San Girolamo, ambapo mazoezi ya Oratorio yaliendelea.
Wakati huo shirika lilikuwa na watu maarufu kama Caesar Baronius, Francesco Maria Tarugi, na Ottavio Paravicini, ambao wote baadaye wakawa makardinali.
Mwaka 1574, Wafirenze walijenga oratorio kubwa ili iwe makao makuu mapya na kupunguza safari.
Shirika lilipozidi kukua, lilipokea parokia ndogo katikati ya Roma, Santa Maria in Vallicella.
Baada ya makao makuu kuhamia huko, Filipo, kwa hati ya Papa ya tarehe 15 Julai 1575, alianzisha rasmi shirika la mapadri wanajimbo lililoitwa Shirika la Oratorio.
Jengo la awali lilibomolewa ili kujenga lingine kubwa na la fahari lililowekwa wakfu mwaka mapema mwaka 1577.
Hata hivyo Filipo hakuhama San Girolamo hadi mwaka 1583, tena kwa amri ya Papa tu, aliyedai kama mkuu wa shirika aishi kwenye makao makuu.
Baada ya kuchaguliwa kwa miaka mitatu, mwaka 1587 alifanywa mkuu hadi kifo, ingawa hiyo haikuwa hamu yake.
Vilevile hakupenda kuwa na madaraka juu ya nyumba nyingine za namna hiyo zilizoanzishwa huko na huko, akaamua zijitegemee, jambo lililopitishwa na Papa Gregori XV mwaka 1622.
Shughuli za kisiasa
[hariri | hariri chanzo]Ingawa Filipo hakupenda kujiingiza katika siasa, mwaka 1593 alimfanya Papa Klementi VIII kufuta uamuzi wa kumtenga na Kanisa mfalme Henri IV wa Ufaransa[9] na wa kumpokea balozi aliyetumwa naye baada ya Henri kuachana na madhehebu ya Yohane Calvin.
Kifo na heshima
[hariri | hariri chanzo]Filipo alifariki tarehe 25 Mei 1595, baada ya kuungamisha na kupokea wageni wengi.[10]
Karibu na usiku kati alianza kutoka damu akaombewa sala za mwisho na Baronius ambaye alimuomba awabariki wafuasi wake; halafu akawa mwandamizi wake.
Maiti yake ipo katika kanisa la Santa Maria in Vallicella mjini Roma.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://www.santiebeati.it/dettaglio/23150
- ↑ Martyrologium Romanum
- ↑ Walsh, p.156
- ↑ Walsh, p.156
- ↑ Walsh, p.156
- ↑ Walsh, p.157
- ↑ Walsh, p.157
- ↑ Ritchie, Charles Sebastian. "St. Philip Romolo Neri." The Catholic Encyclopedia. Vol. 12. New York: Robert Appleton Company, 1911. 20 Dec. 2012
- ↑ "St. Philip Neri, Confessor, Lives of Saints, John J. Crowley & Co., Inc". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-06-02. Iliwekwa mnamo 2013-11-10.
- ↑ Walsh, p.157-158
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Alfonso Capecelatro, The life of Saint Philip Neri, Apostle of Rome v.1 (1894)
- The life of Saint Philip Neri, Apostle of Rome v.2 (1894)
- Bacci, Pietro Giacomo. The life of Saint Philip Neri, Apostle of Rome, and founder of the congregation of the oratory(1902)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Maxims of St. Philip Neri
- Catholic Encyclopedia article
- As described by Goethe
- Filippo Neri's memo to Pope Clement VIII
- Founder Statue in St Peter's Basilica
- St. Philip Neri Church, Kalamulla, Sri Lanka Ilihifadhiwa 9 Desemba 2015 kwenye Wayback Machine.
- Oratorio de San Felipe Neri de Getafe, España
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |