Papa Leo I

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Papa Leo Mkuu anaheshimiwa sana na Waorthodoksi kama inavyoonyesha picha hii.

Papa Leo I (Italia ya kati, 400 hivi – Roma, Italia, 10 Novemba 461) alikuwa Papa kwa muda mrefu, kuanzia 29 Septemba 440 hadi kifo chake[1], wakati usalama wa Roma ulikuwa unatishwa na makabila yasiyostaarabika. Jina lake la kuzaliwa pia lilikuwa Leo.

Alimfuata Papa Sixtus III akafuatwa na Papa Hilarius.

Ndiye Papa wa kwanza kuitwa "Mkuu" kutokana na mchango mkubwa alioutoa upande wa dini na wa siasa akiwajibika kuhudumia taifa la Mungu kwa kila namna. Ni kati ya Mapapa bora waliolipatia Kanisa la Roma sifa na kuliimarishia mamlaka yake wakati ile ya serikali ya jiji hilo ilikuwa inafifia zaidi na zaidi.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1754 Papa Benedikto XIV alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 10 Novemba[2].

Asili na ujana[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa na familia ya kisharifu ama Roma ama katika mkoa wa Toscana (Italia ya kati) mwaka 400 hivi.

Kutokana na umaarufu wake, mwaka 431, akiwa shemasi tu, pengine aliandikiwa na Sirili wa Aleksandria ili amuunge mkono dhidi ya Juvenali wa Yerusalemu. Wakati huohuo Yohane Kasiano alimuandikia kitabu dhidi ya Nestori wa Konstantinopoli. Hasa malkia wa Magharibi alimteua kuwapatanisha maofisa wakuu wa Galia (leo Ufaransa).

Akiwa huko, Papa Sixtus III alifariki (11 Agosti 440), na Leo alichaguliwa na umati kwa kauli moja kushika nafasi yake.

Papa[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 29 Septemba alianza kazi yake kama Papa ambayo ilichangia sana kukusanya mamlaka ya Kanisa lote katika jimbo la Roma, aliloliunda upya pamoja na majimbo mengine ya Italia.

Ili kuimarisha nafasi hiyo ya Kanisa pekee la Magharibi lililoanzishwa na mitume, alijitafutia hati maalumu kwa Kaisari Valentiniano II. Hiyo haikupendeza Wakristo wa Mashariki.

Nafasi bora ya kusisitiza kwa busara mamlaka hiyo hata upande wa mashariki ilitolewa na mabishano kuhusu nafsi ya Yesu Kristo yaliyosababishwa na Eutike kukanusha ubinadamu halisi wa Kristo.

Katika waraka maarufu aliomuandikia Patriarki Flavianus wa Konstantinopoli (449) ili kumuangalisha kuhusu uzushi wa mtu huyo, Leo alifafanua wazi namna umungu na utu wa Kristo yanavyounganika katika nafsi yake.

Hata hivyo mwaka huohuo mtaguso unaojulikana kama Wizi wa Efeso ulipuuzia waraka huo usisomwe, ukamtetea Eutike. Hapo Leo akashika uongozi wa mapambano dhidi yake.

Mwaka 451 katika Mtaguso wa Kalsedonia, baada ya barua yake kwa Flavianus kusomwa, maaskofu wote 350 walisimama na kulia: "Ndiyo imani ya mababu... Mtume Petro amesema kwa njia ya Leo..." Hivyo ilithibitishwa imani katika hali mbili za Kristo zisizochanganyikana wala kutenganika.

Hata hivyo mabalozi wa Leo hawakuwekwa kati ya viongozi wa mtaguso, na kanuni ya 28 ilidai Kanisa la Konstantinopoli kuwa muhimu sawa na la Roma. Kwa hiyo Leo aliikataa, akisisitiza nafasi ya kwanza ya Roma ili kudumisha umoja hasa katika kipindi hicho cha fujo.

Vilevile, Leo alipambana kwa nguvu na Wapelaji, Wamani na Waprishila akitetea daima imani kadiri ya mapokeo ya mitume, akiunganisha vizuri ajabu unyenyekevu wake mwenyewe na hakika juu ya ukuu wa cheo chake kama mwandamizi wa Mtume Petro; vilevile alipambana na ushirikina wa Wapagani.

Siasa[hariri | hariri chanzo]

Mchoro wa Raffaello kuhusu Leo Mkuu kukutana na Atila.

Wakati Dola la Roma lilipokuwa likisambaratika, Leo alipata umaarufu pia kwa kutumia mamlaka yake ya kiroho tu ili kuzuia uvamizi wa Roma uliohofiwa kufanywa na Atila, mfalme wa Wauni (452) na ili kupunguza madhara ya ule uliofanywa na Wavandali kwa wiki mbili (455). Tena alistawisha matendo ya huruma mjini kwa waliopatwa na njaa, dhuluma na ufukara, kama vile umati wa wakimbizi.

Umuhimu wa Leo[hariri | hariri chanzo]

Leo aliunganisha vizuri ajabu unyenyekevu wake mwenyewe na hakika ya ukuu wa cheo chake kama mwandamizi wa Mtume Petro, akiingilia kati masuala mbalimbali magharibi na mashariki vilevile kwa njia ya barua na ya mabalozi wake.

Umuhimu wa Upapa wa Leo, ambao ulidumu muda mrefu kuliko Mapapa karibu wote, ni katika kusisitiza hata kwa madondoo ya Biblia mamlaka ya pekee ambayo Kanisa la Roma linayo juu ya makanisa yote duniani kutokana na Mtume Petro kuwekwa na Kristo na kufia Roma walipo waandamizi wake.

Ndilo fundisho linalojitokeza mfululizo katika barua zake 143 na hasa katika hotuba 96 zilizopo hata leo.

Humo unajitokeza utajiri na uwazi wa mafundisho aliyoyatoa kwa lugha sahili na safi. Ndio mkusanyo wa kwanza wa hotuba za Kipapa zilizochangia sana ustawi wa Kanisa baadaye.

Aliunganisha matendo ya ibada na maisha ya kila siku ya Wakristo, k.mf. saumu na matendo ya huruma. Alionyesha kuwa liturujia ya Kikristo si kumbukumbu ya matukio yaliyopita, bali utimiaji wa mambo yasiyoonekana katika maisha ya kila mmoja. Hivyo ni lazima Pasaka iadhimishwe kila wakati wa mwaka, “si kama jambo la zamani, bali kama tukio la leo”. Hata siku hizi Liturujia ya Roma inazidi kutumia matini yake mengi na kufuata mtindo wake bora katika sala.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. https://www.vatican.va/content/vatican/en/holy-father.index.html#holy-father
  2. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

  • Louise Ropes Loomis, The Book of Popes (Liber Pontificalis). Merchantville, NJ: Evolution Publishing. ISBN 1-889758-86-8 (Reprint of the 1916 edition. English translation with scholarly footnotes, and illustrations).
  • T. Jalland, The Life and Times of St. Leo the Great, (London, 1941).

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]