Nenda kwa yaliyomo

Gallia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Galia)
Gallia wakati wa Caesar (58KK); ramani inaonyesha Gallia Cisalpina (jimbo la Kiroma katika Italia ya Kaskazini), Gallia Narbonensis ilikuwa jimbo la Kiroma katika Kusini ya Ufaransa; Gallia Celtica, Belgica na Aquitania zilikuwa sehemu za Gallia huru hadi Caesar (leo nchi za Ufaransa, Uswisi na Ubelgiji)

Gallia ni jina la kihistoria kwa ajili ya Ufaransa pamoja na maeneo ya jirani.

Eneo la Gallia[hariri | hariri chanzo]

Gallia ilikuwa jina la kilatini kwa ajili maeneo yaliyokaliwa na "Wagallia". Hili ilikuwa namna jinsi Waroma wa Kale walivyowaita majirani wao Wakelti.

Kijiografia eneo hili lilijumlisha Ufaransa, Uswisi, Ubelgiji na Italia ya Kaskazini ya leo. Wakelti au Wagallia walikalia pia Uingereza ya Kusini (=Britania) na Hispania (=Iberia) lakini maeneo haya hayakuhesabiwa kuwa sehemu ya "Gallia" na Waroma. Wakelti walikuwa pia kati ya wakazi wa kale wa Ujerumani kabla ya uvamizi huko wa Wagermanik wenyewe.

Habari za Gallia[hariri | hariri chanzo]

Karibu habari zote za kimaandishi kuhusu Gallia na Wagalli zimetokana na Waroma wa kale. Sehemu kubwa ya habari zinapatikana katika kitabu cha Caesar "Vita ya Gallia".

Kuna pia mabaki ya kiarkolojia hasa makaburi pamoja na vitu vya maisha ya kila siku vilivyoweka makaburini kwa imani ya kwamba vitawasaidia marehemu katika ahera. Arkiolojia ya makaburi inaonyesha ya kwamba Wakelti (Wagallia) walikuwa sehemu ya biashara ya kimataifa pia walikuwa na mafundi wenye uwezo wa kutengeneza vitambaa na nguo, pia na wahunzi na wafinyanzi.

Wagallia na Waroma[hariri | hariri chanzo]

Mnamo mwaka 390 KK kabila fulani la Wagallia chini ya kiongozi Brennus lilivamia Italia na mji wa Roma lakini walishindwa kuteka boma la mji. Kwa muda mrefu Waroma walihofia majirani ya kaskazini.

Kuanzia mwaka 200 KK Waroma walikuwa waliendelea kisiasa, kiuchumi na kijeshi wakafaulu kuteka "Gallia Cisalpina" (Gallia upande wa kusini wa milima ya Alpi) ambayo leo hii ni Italia ya Kaskazini. Ikawa jimbo la Kiroma.

Kuanzia mwaka 125 KK Waroma walianza kuvamia sehemu za pwani la Gallia pamoja na bonde la mto wa Rhone. Ikawa jimbo la Gallia Narbonensis. Mji mkuu ulikuwa mji wa Narbo (leo: Narbonne).

Sehemu nyingine ya Gallia imebaki nchi huru ya makabila yaliyojitawala. Mwaka 58 KK mwanasiasa na jenerali Mroma Caesar akawa gavana wa Gallia Cisalpina pia Narbonensis. Alichukua nafasi ya vita kati ya makabila ya Wagallia katika eneo la Uswisi kuingilia ndani ya mambo ya Gallia huru. Katika vita ya miaka nane alishinda wapinzani wote. Mwaka 51 KK Gallia yote ikawa chini ya utawala wa Kiroma.

Jimbo la Kiroma[hariri | hariri chanzo]

Katika karne zilizofuata Gallia imekuwa sehemu halisi ya Dola la Roma. Inaonekana Wagallia wenyewe walikubali utawala wa Kiroma hasa baada ya kupewa uraia wa Kiroma. Lugha ya Kilatini ilitumika kwa ajili ya habari za kiutawala ikapokelewa polepole na wenyeji. Kilatini hiki kilikuwa msingi wa lugha ya Kifaransa kilichotokea baadaye.