Ukulu mtakatifu
Ukulu mtakatifu au Ukulu wa Kitume (kwa Kiingereza: Holy See au Apostolic See) kwa maana asili ni kiti maalumu alichowekewa Papa katika Kanisa kuu la Roma, ambacho ni ishara ya mamlaka ya kiaskofu ambayo Wakatoliki wanasadiki anayo ya kufundisha, kutakasa na kuongoza Taifa la Mungu kokote duniani.
Katika imani ya Kikatoliki
[hariri | hariri chanzo]Kwa msingi huo, ukulu unamwakilisha Papa kama kiongozi wa Kanisa Katoliki lote duniani na kuhusiana na dogma ya kwamba ana karama ya kutodanganyika anapofundisha "rasmi" (kwa Kilatini "ex cathedra", yaani "kutoka ukulu") kama mkuu wa kundi la maaskofu.
Katika liturujia
[hariri | hariri chanzo]Sikukuu ya ukulu huo inaadhimisha kila mwaka tarehe 22 Februari[1] kwa jina la Ukulu wa Mtume Petro, ambaye aliambiwa na Bwana, “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huo nitalijenga Kanisa langu” (Math 16:18) na anayeaminiwa kuwa ndiye aliyewarithisha Mapapa mamlaka yake kama mkuu wa Mitume wa Yesu.
Siku hiyo, ambayo Warumi walikuwa na desturi ya kufanya ukumbusho wa wafu wao, Wakatoliki wanaheshimu ukulu wa Mtume huyo, aliyemfia Yesu kitukufu katika kilima cha Vatikano, ambao unatakiwa kusimamia ushirika wa kimataifa wa upendo wa Kikristo.
Katika sheria za Kanisa
[hariri | hariri chanzo]Kadiri ya Mkusanyo wa Sheria za Kanisa la Kilatini (kanuni 361), "Ukulu mtakatifu" ni jina rasmi linalotumika kuwamaanisha Papa na miundo yote inayomsaidia kuongoza Kanisa Katoliki duniani ikiwa na makao makuu mjini Roma.
Ukulu usipokuwa na Papa
[hariri | hariri chanzo]Wakati Kanisa linapobaki halina Papa (kutokana na kifo au kujiuzulu), uongozi wake unashikwa na Kundi la Makardinali ambalo pia lina wajibu na haki ya kumchagua mwandamizi wake.
Katika mafungamano ya kimataifa
[hariri | hariri chanzo]Ukulu mtakatifu una hadhi ya nafsi ya kisheria katika sheria za kimataifa kutokana na umbile lake, mapokeo ya historia na mahitaji ya utume wake.
Ukulu mtakatifu unawakilisha kwa pamoja Kanisa Katoliki na nchi huru ya Mji wa Vatikani (ambayo iko chini ya mamlaka yake) katika mafungamano ya kimataifa na nchi yoyote duniani na miundo ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, ambapo unatambulika kama mojawapo kati ya watazamaji wa kudumu.
Ukulu mtakatifu na Vatikani
[hariri | hariri chanzo]Kisheria, ukulu mtakatifu ni tofauti na Mji wa Vatikani ambayo ni nchi huru inayotawaliwa na Papa na ilianzishwa rasmi tarehe 11 Februari 1929 kwa makubaliano kati ya Ukulu mtakatifu na Ufalme wa Italia. Eneo dogo la nchi hiyo (kilometa mraba 0.44) linadaiwa na kutosha ili kuhakikisha uhuru wa miundo ya Kanisa katika kutekeleza majukumu yake, lisije likaingiliwa na serikali yoyote kama ilivyotokea mara nyingi katika historia ya Kanisa.
Katika diplomasia ya kimataifa, mabalozi wanaowakilisha nchi huru nyingine (184, mwanzoni mwa mwaka 2023) wanatumwa kwa Ukulu mtakatifu, si kwa nchi ya Vatikani, na huitwa "balozi kwa Ukulu mtakatifu".
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Kuhusu kiti kama ishara ya mamlaka: Kikalio cha dhahabu
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Köck, Heribert F. (1975). Die Völkerrechtliche Stellung Des Heiligen Stuhls: Dargestellt an Seiner Beziehungen Zu Staaten Und Internationalen Organisationen. Berlin: Duncker und Humblot. ISBN 3-428-03355-8.
- Köck, Heribert F. (1995). "Holy See". Katika Bernhardt, Rudolf; Macalister-Smith, Peter (whr.). Max Planck Encyclopedia of Public International Law. Juz. 2. Amsterdam: North-Holland. ISBN 0-444-86245-5.
- La Due, William J. (1999). The Chair of Saint Peter: A History of the Papacy. Maryknoll, N.Y: Orbis Books. ISBN 1-57075-249-4.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Tovuti rasmi ya Ukulu Mtakatifu
- The Holy See News Portal (News.va) Archived 28 Juni 2011 at the Wayback Machine.
- YouTube Vatican Channel
- Primacy of the Apostolic See
- CIA World Factbook on Holy See Archived 7 Januari 2019 at the Wayback Machine.
- Between Venus and Mars, the Church of Rome Chooses Both Archived 6 Juni 2006 at the Wayback Machine.—The Holy See’s geopolitics analyzed in the light of the dominant doctrines
- The Holy See in the course of time, from an Orthodox perspective
Makala hii kuhusu Kanisa Katoliki bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ukulu mtakatifu kama historia yake au maelezo zaidi? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |