Umwilisho

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Umwilisho ni neno la teolojia linalotumika kulitaja fumbo la imani ya Ukristo la kwamba Mwana wa Mungu alijifanya binadamu kweli kwa kutwaa roho na hata mwili.

Mkazo juu ya mwili unatokana na dibaji ya Injili ya Yohane inayosisitiza ajabu la tukio hilo ikisema: "Neno akawa mwili akakaa kwetu" (1:14).

Kwa msingi huo Kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli inafundisha kukiri:

Alishuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu, akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.

Umwilisho ulifanyika pale ambapo Maria alikubali wito wa Mungu kwake alivyoletewa na Malaika Gabrieli huko Nazareti (Lk 1:38).

Dini nyingine ziliwahi kusimulia juu ya mungu fulani kuja duniani akionekana kama mtu (kwa mfano Avatar katika Uhindu), lakini umwilisho ni wa pekee kwa kuwa unatokana na imani ya kuwa Yesu tangu alipotungwa tumboni mwa mama yake ni binadamu halisi kama mwingine yeyote, ingawa nafsi yake ni ya milele kama ile ya Mungu Baba na ya Roho Mtakatifu.