Nenda kwa yaliyomo

Sirili wa Yerusalemu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha takatifu ya Mt. Sirili wa Yerusalemu

Sirili wa Yerusalemu (kwa Kigiriki Κύριλλος Α΄ Ἱεροσολύμων; 315386 au 387) alikuwa askofu wa mji huo nchini Israeli kuanzia mwaka 348 hadi kifo chake akijihusisha sana na mabishano kuhusu umungu wa Yesu Kristo hata akadhulumiwa sana na Waario na serikali ya Dola la Roma kwa ajili ya imani sahihi na kufukuzwa jimboni mwake mara kadhaa, pamoja na kufafanua vizuri ajabu kwa waamini imani hiyo, maandiko ya Biblia na mafumbo matakatifu kwa hotuba na katekesi.

Tangu zamani ametambuliwa kuwa mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1883 Papa Leo XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 18 Machi[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Sirili alizaliwa mwaka 315 katika familia ya Kikristo mwaka 315 mjini Yerusalemu au karibu nao. Baada ya kupata elimu bora upande wa lugha na fasihi, iliyokuwa msingi wa ujuzi wake wa kidini wenye kutegemea Biblia, alipadirishwa na askofu Masimo wa Yerusalemu.

Alipokufa (au alipoondoshwa) huyo, Sirili alichaguliwa kuwa askofu wa Yerusalemu na kuwekwa wakfu na Akasio, askofu mkuu wa Kaisarea Baharini. Alipewa daraja takatifu hiyo kwa sababu alidhaniwa kuelekea uzushi wa Waario, hivyo hata Wakatoliki walimuona amekubali uzushi.

Kumbe, alikuwa hatumii neno “homousios” lililopitishwa na Mtaguso I wa Nisea, kwa sababu hakupenda kutumia maneno yasiyopatikana katika Biblia, tena aliogopa litatafsiriwa vibaya.

Basi, alikuja kubishana na Waario mapema juu ya umungu wa Yesu, pamoja na kutetetea hadhi ya Kanisa la Yerusalemu kwamba halitakiwi kuwa chini ya Kaisarea. Kwa sababu hiyo mara tatu alifukuzwa kutoka nchini mwake (357, 360, 367-378).

Kaisari Valens alipofariki, Sirili aliweza kurejea Yerusalemu na kurudisha umoja na amani kati ya waamini.

Mwaka 381 alishiriki Mtaguso I wa Konstantinopoli akitoa mchango mkubwa. Baada ya hapo, usahihi wa imani yake, uhalali wa uaskofu wake na stahili za uchungaji wake vilithibitishwa na barua ya maaskofu wa mashariki kwa Papa (382).

Alifariki mwaka 386.

Maandishi na teolojia yake[hariri | hariri chanzo]

Moyo wake wa kichungaji unaonekana hasa katika kitabu chake Catecheses, yaani mafundisho 24 kwa wakatekumeni na kwa Wakristo wapya aliyoyatoa mwaka 350 hivi akiwa katika Kanisa la Kaburi na Ufufuo wa Yesu na pengine.

Humo anawaeleza masharti ya ubatizo, uongofu, sakramenti, mafundisho ya kweli ya Ukristo, sala ya Bwana na hatimaye mafumbo waliyoyashiriki katika liturujia.

Alifanya hivyo akiwaelekeza kwa Kristo, kiini cha ulimwengu, kwa kulinganisha Maandiko Matakatifu ya Agano la Kale na Agano Jipya na kutegemea mapokeo ya Kanisa la Yerusalemu pamoja na kupinga hoja za Wapagani, Wamani, Wakristo wa Kiyahudi na Waario.

Ni kati ya vitabu vya zamani vilivyo muhimu zaidi kuhusu katekesi, kikiwa wazi upande wa mawazo na wa ufafanuzi wake na kutumia mifano mingi. Kwa pamoja hotuba hizo zinaongoza kuelewa maana ya kuzaliwa upya.

Humo tunaona alivyotaka Wakristo wawe na imani ya dhati, na alivyowaelekeza njia ya kuishi kadiri ya imani hiyo: kuanzia Ubatizo, kupitia Ekaristi hadi maisha matakatifu. Kaulimbiu yake ilikuwa: “Mkristo anambeba Kristo”. Kwake imani na maadili vinakwenda pamoja.

Aliwaambia wakatekumeni: “Nyinyi mmenaswa katika wavu wa Kanisa. Basi, mtekwe wazima; msikimbie kwa sababu ni Yesu anayewavua si kwa lengo la kuwaua bali la kuwafufua baada ya kifo. Hakika, mnapaswa kufa na kufufuka… Fieni dhambi zenu na kuishi kwa uadilifu tangu siku hii”.

Baada ya ubatizo aliwaambia: “Wakati uleule nyinyi mlikufa na kuzaliwa; na yale maji ya wokovu yalikuwa kwa pamoja kaburi lenu na mama yenu… Kwenu wakati wa kufa umekuwa pia wakati wa kuzaliwa”.

Ugumu wa Sirili katika kuruhusu ubatizo wa wakatekumeni na udhati wa imani aliowafikishia ni ushahidi wa uhai wa Ukristo katika karne IV.

Aliona ubatizo kuwa “ukombozi wa wafungwa, msamaha wa makosa, kifo cha dhambi na kuzaliwa upya kwa roho” na alikanusha uwezekano wa kuokolewa kwa wasioupata ama kwa maji ama kwa damu.

Kuhusu ekaristi, alikuwa mwanateolojia wa kwanza kufafanua uwemo halisi wa Mwili na Damu ya Kristo kama tokeo la badiliko la dhati za mkate na divai likisababishwa na Roho Mtakatifu kuitwa juu ya vipaji hivyo. Alifananisha badiliko hilo na lile la maji kuwa divai kwenye arusi ya Kana.

Vilevile, Sirili alieleza jinsi ekaristi ilivyo sadaka ya kiroho na ya maombezi.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tafsiri za maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

 • Gifford, Edwin Hamilton. (1894) Nicene and Post-Nicene Fathers, Second Series, Vol. 7. Edited by Philip Schaff and Henry Wace. (Buffalo, NY: Christian Literature Publishing Co.) [translation of the Catechetical Lectures, available at http://www.newadvent.org/fathers/3101.htm]
 • McCauley, Leo P and Anthony A Stephenson, (1969, 1970). The works of Saint Cyril of Jerusalem. 2 vols. Washington: Catholic University of America Press [contains an introduction, and English translations of: Vol 1: The introductory lecture (Procatechesis). Lenten lectures (Catecheses). Vol 2: Lenten lectures (Katēchēseis). Mystagogical lectures (Katēchēseis mystagōgikai). Sermon on the paralytic (Homilia eis ton paralytikon ton epi tēn Kolymbēthran). Letter to Constantius (Epistolē pros Kōnstantion). Fragments.]
 • Telfer, W.(1955). Cyril of Jerusalem and Nemesius of Emesa. The Library of Christian classics, v. 4. Philadelphia: Westminster Press.
 • Yarnold, E., (2000). Cyril of Jerusalem. The early church fathers. London: Routledge. [provides an introduction, and full English translations of the Letter to Constantius, the Homily on the Paralytic, the Procatechesis, and the Mystagogic Catechesis, as well as selections from the Lenten Catecheses.]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 • The Penguin Dictionary of Saints, 3rd Edition, Donald Attwater and Catherine Rachel John, New York: Peguin Putnam Inc., 1995, ISBN 0-14-051312-4
 • Lives of the Saints, For Every Day of the Year edited by Rev. Hugo Hoever, S.O.Cist., Ph.D., New York: Catholic Book Publishing Co., 1955
 • Omer Englebert, Lives of the Saints New York: Barnes & Noble Books, 1994, ISBN 1-56619-516-0
 • Drijvers, J. W. (2004). Cyril of Jerusalem: Bishop and city. Supplements to Vigiliae Christianae, v. 72. Leiden: Brill.
 • Lane, A. N. S., & Lane, A. N. S. (2006). A concise history of Christian thought. Grand Rapids, Mich: Baker Academic.
 • Van, N. P. (January 1, 2007). 'The Career Of Cyril Of Jerusalem (C.348–87): A Reassessment'. The Journal of Theological Studies, 58, 1, 134-146.
 • Di Berardino, Angelo. 1992. Encyclopedia of the early church. New York: Oxford University Press.
 • In Cross, F. L., & In Livingstone, E. A. (1974). The Oxford dictionary of the Christian Church. London: Oxford University Press.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]