Mkate

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Chapati
Tortilla
Mkate wa Kijerumani uliotengenezwa kwa ngano nyekundu
Mkate wa kifaransa


Mkate ni chakula kinachotengenezwa kwa kuoka kinyunga cha unga na maji. Mara nyingi viungo huongezwa kwa kubadilisha ladha. Kuna pia mikate inayotiwa kiasi kidogo cha mafuta.

Namna za mkate

Kimsingi kuna aina mbili za mkate:

  • mkate wa kinyunga kilichochachuka
  • mkate wa kinyunga kisichochachuka

Mikate bapa aina ya chapati hutengenezwa katika sufuria au kaango au hata juu ya jiwe la joto. Mikate minene huhitaji joko (oveni) yaani jiko lenye chumba ndani yake. Lakini kuna pia aina za mikate bapa inayotengenezwa katika oveni.

Kama kinyunga kinatengenezwa kwa kuongeza mafuta mengi, sukari na maziwa si mkate tena bali keki.

Aina ya mikate isiyochachuka

Chapati ni aina ya mkate usiochachuka pamoja na tortilla ya Mexiko na mikati mbalimbali za Ulaya. Hapa unga na maji hukorogwa kuwa aina ya ugali nzito halafu kinyunga huandaliwa kwa umbo la sahani bapa na kuwekwa juu ya jiwe la joto au ndani ya sufuria juu ya moto.

Aina mbalimbali za chapati hizi zinaongezwa ladha kwa kutia mafuta au viungo ndani yake.

Aina hizi zote ni nyembamba kwa sababu kinyunga huwa nzito mno bila kuchachuka.

Hii ni mbinu asilia wa kutengeneza mikate.


Mikate iliyochachuka

Kwa aina nyingi ya mikate kinyunga huchachuka. Kuna madawa mbalimbali zinazofaa kuwa chachu kama hamira. Vijidudu vya chachu viko hewani kwa hiyo kinyunga kitachachuka kikikaa hewani kwa muda wa siku moja au zaidi (chachu asilia).

Njia ya haraka ya na uhakika ni kutia dawa la hamira lililonunuliwa. Kama friji ipo inawezekana kuweka akiba ndogo ya kinyunga kilichochachuka kando kila safari. Kitaunzwa katika hali baridi halafu kukorogwa katika kinyunga kipya.

Mikati iliyochachuka huokwa katika oveni.

Kuna aina nyingi sana ya mkate duniani. Tofauti za rangi na ladha zatokana na aina ya unga na namna ya kuoka katika oveni. Kwa jumla mikate inayotumia unga wa nafaka yote huwa nyeusi zaidi. Mikate meupe-meupe hutokana na unga wa nafaka iliyokobolewa.

Nafaka kama ngano nyekundu na shayiri huleta pia mkate mweusi zaidi.

Mkate na utamaduni

Mkate kama chakula cha kila siku ni sehemu ya utamaduni wa nchi nyingi. Duniani ni Wajerumani wanaokula mkate mwingi kila siku wakifuatwa na watu wa Chile. Ujerumani kuna aina tofauti ya mkate kati ya 500-1,000 zinazookwa katika maduka ya mkate zaidi ya 16,000. Katika nchi nyingine sehemu kubwa ya mkate huokwa katika viwanda.

Nje ya miji mikubwa kuna bado kawaida ya kuoka mikate nyumbani katika nchi kadhaa hasa Asia.

Mkate uliingia pia katika sala kuu ya Ukristo "Baba yetu". Ombi la nne lataja "mkate wa kila siku". Katika tafsiri za Kiswahili za sala hii ombi limetafsiriwa kwa njia mbili tofauti. Utamaduni wa Afrika haukujua mkate kama chakula. Waprotestant walitafsiri hapa "riziki" wakielewa maana ya mkate katika sala si chakula kile tu lakini mahitaji ya kimwili kwa jumla. Wakatoliki walitumia neno "mkate" ulioanza kutumiwa kwa chakula hiki lakini halikujulikana bado kwa watu wengi Afrika bara.

Picha