Hewa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Yaliyomo katika hewa.
Parapela ya fan kama hii inasukuma hewa na kusababisha mwendo kama upepo.

Hewa ni kitu kinachotuzingira; ilhali haionekani lakini tunaweza kuisikia. Tukifungua mashine ya friji tunasikia baridi ya hewa ndani yake; tukisikia upepo, huu ni mwendo wa hewa; tukitikisa mkono haraka tunasikia hewa kama upepo kidogo. Kila tukipumua tunajaza mapafu kwa hewa na tukimwona ndege jinsi anavyoruka anapiga hewa kwa mabwawa yake.

Hewa kwa macho ya sayansi[hariri | hariri chanzo]

Hewa yenyewe ni gimba la gesi. Sayansi ya kemia inatuambia ni mchanganyiko wa gesi mbalimbali hasa nitrojeni (78 %) na oksijeni (21 %) pamoja na viwango vidogo vya arigoni (0.9 %), kaboni dioksidi (0.035 %), hidrojeni (0.01%), neoni (0.00123%), helium (0.0004%), kriptoni (0.00005%) na xenoni (0.000006%).[1] Ndani ya hewa wakati wowote kuna viwango tofauti vya mvuke wa maji na vumbi za aina nyingi. Kwa kawaida hewa haina rangi, ladha wala harufu.

Hewa na uhai[hariri | hariri chanzo]

Wanyama wanahitaji oksijeni ya hewa kwa maisha yao wakiipata kwa njia ya kupumua. Kinyume chake mimea hutumia kaboni dioksidi ya hewani kwa usanisinuru na kwa njia hiyo wanapata kaboni iliyo lazima ya kujenga miili yao na hii ni pia kaboni tunayotumia tukichoma mimea mikavu, kwa mfano kuni.

Uzito wa hewa[hariri | hariri chanzo]

Hewa ina uzito wake. Kwenye uwiano wa bahari kila mita ya mjao]] huwa na uzito wa kilogramu 1,2041. Kwa sababu angahewa inafikia kilomita mia kadhaa juu ya uso wa dunia kuna uzito wa tani 10 au kilogramu 10.000. Huu ni uzito tunaobeba kila siku lakini hatuusikii kwa sababu kwetu ni kawaida na tunaihitaji. Kama tungeondoka kutoka eropleni bila kinga katika kimo kirefu sana kama juu ya kilomita 50 tungekufa haraka sana, si tu kwa sababu huko hakuna hewa ya kutosha kwa kupumua, lakini kwa sababu uhaba wa kanieneo ungesababisha damu yetu kuchemka.

Hewa kama gesi, kiowevu, mango[hariri | hariri chanzo]

Katika mazingira ya dunia yetu hewa hutokea kama gesi. Lakini inawezekana kupata hewa katika hali ya kiowevu kwa msaada wa mitambo ambapo halijoto ya hewa inapozwa hadi sentigredi 170 chini ya 0 ambako inaanza kugeuka kuwa majimaji. Ikitunzwa katika chupa imara chini ya kanieneo kubwa inaendelea kupatikana kama kiowevu hata kama halijoto yake inapanda tena. Kama halijoto inashuka zaidi hadi kufikia -220 °C kuna pia uwezekano wa kupata hewa mango. Kwenye sayari katika mfumo wa jua letu zilizo mbali na jua na baridi vile hewa yaani elementi kama nitrojeni, oksijeni au methani hazipatikani kama gesi lakini kama barafu au theluji. Kama sehemu ya sayari hizo zinaingia katika kipindi cha "joto" kiasi barafu hizo zinaweza kuyeyuka kuingia katika hali ya kiowevu au gesi na kuunda aina ya angahewa inayoganda tena kipindi cha joto kikiisha na halijoto inashuka tena katika mazingira yale.

Hewa nje ya dunia[hariri | hariri chanzo]

Nje ya angahewa ya dunia katika anga-nje hakuna hewa isipokuwa kwenye sayari za jua na miezi yake kama yana masi ya kusababisha graviti ya kutosha inayoshika gesi za angahewa. Lakini hewa kwenye sayari nyingine ni mchanganyiko tofauti wenye gesi nyingine. Viumbehai kutoka duniani wasingeweza kupumua huko hata kama kanieneo na halijoto zingeruhusu kukaa bila kinga.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hewa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.