Kuni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Kuni inapelekwa sokoni katika nchi ya Kiafrika
Kuni kwa umbo la donge hutengenezwa kutokana na ubao uliosagwa
Katika sehemu nyingi za Ulaya watu huandaa kuni kwa ajili ya majira ya baridi na kuipanga kwa namna inayosaidia kukauka na kupatikana kirahisi; huu mfungo utafunkiwa baadaye kwa plastiki
Mashine ya kupasua miti minene kiasi kuwa kuni inatumia hidrauliki

Kuni ni ubao unaotumiwa kama fueli ikichomwa motoni ya kupikia au pia ya kupashia nyumba moto.

Kwa kawaida kuni inakusanywa penye miti kwa kutafuta sehemu ziliokauka au kwa kukata miti inayopasuliwa kuwa vipande vya ukubwa unaofaa. Kwa kutumia teknolojia kuna pia kuni inayopitishwa kwenye mashine na kupewa umbo maalumu unaofaa majiko ya kisasa.

Matumizi ya kuni[hariri | hariri chanzo]

Watu wengi duniani kwenye nchi za joto hutumia kuni kwa kupikia chakula na kuchemsha maji ya kuoga au kuosha nguo. Tangu karne ya 19 na hasa 20 watu wengi wamehamia kutumia fueli nyingine kama makaa mawe, gesi na madawa yanayotengenezwa kutokana na mafuta ya petroli au pia umeme.

Lakini hata katika nchi baridi zilizoendelea kuna watu wengi kidogo katika mazingira ya misitu wanaopendelea kuendelea kutumia kuni kama mababu zao. Wengine wanafanya hivyo kwa sababu wana maeneo ya miti au msitu hivyo kuni kwao ni bure; wengine wamefuata majadiliano juu ya ekolojia na wanaona ni bora kimaadili kutumia fueli ya nishati mbadala kuliko fueli ya kisukuku‎; wengine wameona ya kwamba ubao ni fueli nafuu kama wanakaa karibu na misitu na wana uwezo wa kununua majiko ya kisasa kwa nyumba yao.

Kuni na mazingira[hariri | hariri chanzo]

Kuni ni fueli inayokua maana ubao unazidi kukua na kuandaa kuni mpya kwa matumzi ya kibinadamu. Lakini matumizi yanaweza kuzidi kasi ya ukuaji upya kwa eneo fulani na hapa kuna hatari ya kuharibu mazingira.

Sheria ya uchumi wa misitu ni kuondoa kuni katika eneo fulani sawa na kiwango cha ubao kinachokua kila mwaka katika eneo hili. Hata hivyo katika nchi mahitaji ya kuni na makaa pamoja na usimamizi hafifu upande wa serikali yamesababisha kupungukiwa kwa misitu na upotevu wa udongo, kukauka kwa visima, kupungukiwa kwa mvua na kuongezeka kwa mafuriko makali.[1][2]

Tabia za kuni[hariri | hariri chanzo]

Sifa muhimu ya kuni ni uwezo wake wa kutoa joto. Hapa kuni kavu huwaka na kutoa joto vizuri kushinda kui bichi yaani kuni yenye asilimia kubwa ya unyevi ndani yake.

Inasaidia kama kuni inakatwa wakati miti inapumzika kwa mfano wakati wa ukame au wakati wa baridi katika nchi nje ya tropiki. Katika vipindi hivi ubao hauna majimaji mengi ndani yake. Menginevyo kuni inahitaji muda mwingi hadi ikauke.

Pamoja na hii tabia kama herufi na namna ya kuchoma zinatazamiwa pia, kwa mfano inapendeza ikiwaka kimyakimya bila cheche nyingi. Tabia nyingine inayoangaliwa ni unene wa ubao maana watu wasio na vifaa wana matatizo kupasua miti minene lakini penye mashine si kitu.

Vilevile aina tofauti za miti huleta kuni tofauti. Kuna aina zinazowaka haraka na hizi zinafaa sana kwa upishi. Ainy nyingine huwaka polepole ni afadhali kwa majiko ya kupasha moto nyumba katika nchi penye baridi.

Uzito wa ubao ni pia tabia muhimu kwa ajili ya matumizi yake kama kuni. Kuni nyepesi inachukua nafasi kubwa wakati wa kuibeba sokoni kushinda kuni nzito zaidi; kiasi cha joto hutegemeana na uzito yaani kilogramu 1 ya kuni inaleta kiasi fulani cha joto ila tu kama kuni ni nyepesi inatumia nafasi kubwa zaidi.

Kuiandaa kuni[hariri | hariri chanzo]

Kwatika sehemu nyingi za Afrika kuni huchukuliwa kutoka kwa miti membamba au matawi. Hii hukatwa kwa kutumia panga au shoka. Pale ambako miti mineni hukatwa kwa kuni watu hutumia msumeno ama wa mkono au wa mashine.

Baadaye vipande hukatwa kwa urefu unaofaa kuisafirishwa hadi nyumbani au sokoni. Urefu huu unategemea na usafiri na pia ukubwa wa majiko ya kawaida.

Pale ambako miti minene hutumiwa kama kuni ni lazima kupasua vipande vikubwa. Hii inafanywa mara nyingi na wakata miti wenyewe lakini watu wanaotumia kuni kwa wingi wamejipatia vifaa vya kupasulia ili wanunue kuni yao kwa bei nafuu.

Katika nchi za kaskazini kuna watu wanaotumia kuni kwa kupashia moto nyumba wakati wote wa baridi na hapa teknolojia mpya imesambaa. Kwa wale wanaopenda kutumia kuni kwa sababu za ekolojia au gharama bila kazi ya kupasua na kujaza jiko mara kwa mara kuna teknolojia inayotumia kuni kwa umbo la donge. Hapo kuni husagwa kwanza halafu kusukumwa kwa umbo la donge. Donge hivi zinajazwakatika tangi na kuingia ndani ya jiko mfululizo karibu kama mafuta. Donge za kuni zinapatikana katika maeneo ya misitu mingi penye viwabda vya kupasilia miti. Viwanda hivi hutumia unga wa ubao pamoja na mabaki yote yasiyouzwa kama bao vinatengeneza donge hizi.

Namna ya pekee ya kuanda kuni ni kuichoma kuwa makaa. Hasa katika miji mikubwa ya Afrika makaa yamechukua mara nyingi nafasi ya kuni yenyewe kwa sababu yanawaka kwa moto safi zaidi na hii ni muhimu katika msongamano wa watu wegi mjini. Pamoja na hayo kuni inachukua nafasi kubwa kuliko makaa kwa kiasi kilekile cha joto inayotakiwa na bei za kusafirisha kuni mjini pamoja na gharama za kutumza akiba za sokoni ndani ya mji imeleta makaa kuwa nafuu.

Kutunza kuni[hariri | hariri chanzo]

Katika nchi za Arika kuni kwa kawaida haitunzwi. Inakatwa au kununuliwa jinsi inavyohitajika.

Hali hii ni tofauti katika nchi baridi. Hapa una haja ya kuwa na akiba ya kutosha kwa kupashia nyumba moto maana hata siku mbili bila kuni wakati wa baridi inaweza kuwa hatari. Kwa hiyo kuni huandaliwa na kuwekwa tayari kama akiba kwa majira yote ya baridi. Hapa ni muhimu kuiweka kwa namna inayoruhusu upepo kupitia kwenye vipande vya kuni na kuikausha vizuri; penye mvua nyingi sehemu za paa hutengenezwa kwa kuni lakini siku hizi vipande vikubwa vya plastiki vinatosha.

Donge za kuni kwa majiko ya kisasa huwekwa katika vyumba au matangi na kutoka hapa vinapelekwa kwa njia ya mitamo hadi jikoni.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. http://www.meac.go.tz/news/miradi-ya-nishati-inavyosaidia-kutunza-mazingira Majiko Banifu kama njia ya kupunguza matumizi ya kuni
  2. http://habarileo.co.tz/index.php/makala/25820-uharibifu-wa-mazingira-kiini-cha-umasikini-tanzania Uharibifu wa mazingira kiini cha umaskini Tanzania, Habrileo 1.6.2014

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu: