Nenda kwa yaliyomo

Petroli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kontena ya petroli
Pampu ya petroli

Petroli ni aina ya fueli inayopatikana kwa kawaida kwa mwevusho wa mafuta ya petroli. Kikemia ni mchanganyiko wa hidrokaboni zaidi ya 100. [1]

Matumizi ya petroli ni hasa fueli za injini za motokaa, pikipiki na eropleni.

Historia

Petroli iligunduliwa wakati wa karne ya 19. Awali ilitumiwa kama dawa la viroboto na pia dawa la kuondoa uchafu kwenye nguo.

Ikatumiwa pia kama fueli ya kupikia na hadi leo kuna majiko madogo ya petroli kwa ajili ya upishi wakati wa camping.

Tangu kugunduliwa kwa motokaa za kwanza na Carl Benz mnamo mwaka 1885 petroli ilianza kutumiwa kama fueli ya injini za magari na ndiyo matumizi yake makuu kwa sasa.

Aina za petroli

Kuna aina mbalimbali za petroli.

Madereva wa motokaa hujua petroli ya kawaida na petroli ya supa; hasa injini zinazozunguka haraka zinahitaji petroli ya supa.

Ndege kwa kawaida hutumia petroli za pekee.

Uzalishaji

Sehemu kubwa kabisa ya petroli inayotengenzwa leo hii hutokea na mwevusho wa mafuta ya petroli katika viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta.

Mafuta hayo hupashwa moto hadi dutu mbalimbali ndani yake hufikia kiwango cha kuchemka na kuwa gesi. Mafuta ni mchanganyiko wa dutu za kikemia mbalimbali zinazofikia kiwango cha kuchemka kwa halijoto tofautitofauti.

Kwa hiyo gesi inayojitokeza inaelekezwa kwa chombo tofauti kila baada ya kufikia kiwango cha kuchemka kingine. Gesi hizi zinapozwa tena kuwa kiowevu.

Hidrokaboni mbalimbali hujitokeza kwenye halijoto kati ya 25 °C na 210 °C. Baadaye zinachanganywa tena kutokana na mahitaji maalumu ya matumizi kwa aina mbalimbali za petroli.

Kuna pia njia nyingine ya kuiondoa katika makaa kwa sababu kikemia mafuta ya petroli na makaa ni dutu za karibu kiasi. Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia Ujerumani ilitengeneza sehemu kubwa ya petroli kwa njia hii kwa sababu chemchemi za mafuta zilikuwa mkononi mwa maadui zake.

Nyongeza katika petroli

Kemikali mbalimbali huongezwa baadaye kwa kuboresha tabia za petroli. Zamani petroli za motokaa iliongezwa hasa metali ya risasi (plumbi) lakini hii hukatazwa siku hizi katika nchi nyingi kutokana na hasara za metali hii kwa ajili ya afya na mazingira. Petroli zenye risasi huitwa mara nyingi kwa neno la Kiingerea "leaded", ile bila risasi "unleaded". Injini kadhaa za kale huhitaji "leaded" na pale ambako aina hii haipatikani tena kuwa dawa la pekee linalopaswa kuongezwa kuongezwa katika tangi ya motokaa baada ya kujaza "unleaded".

Petroli na dizeli

Kwenye vituo vya pampu za petroli madereva wanakuta mara nyingi chaguo kati ya petroli na dizeli. Hazitakiwi kuchanganywa kwa sababu hata kama dizeli hutengenezwa pia kutokana na mafuta ya petroli ni fueli nzito zaidi inayohitaji injini tofauti (injini ya diszeli) haiwaki ndani ya injini za Otto ambazo ni injini za kawaida kwa motokaa ndogo. Lori mara nyingi huwa na injini ya dizeli lakini kuna pia motokaa ndogo. Kinyume chake petroli itaharibu injini ya dizeli.

Kwa kuzuia kuchanganyikiwa kwa aina hizi mbili za fueli mara nyingi pampu huwa na mipira yenye unene tofauti na vile mdomo wa tangi ya gari zina nafasi tofauti ya kupokea mpira wa pampu.

Petroli ikiwaka katika maabara ya utafiti

Hatari za ajali, kwa afya na kwa mazingira

Petroli ina hatari mbalimbali na inahitaji kushughulikiwa kiangalifu.

  • inatakiwa kutunzwa katika chombo kilichofungwa vizuri. Kwa halijoto ya kawaida inaanza kuvukizika kwa hiyo juu ya uso wake kuna daima wingu la gesi yake inayowaka haraka. Cheche kimoja kinatosha kusababisha mlipuko. Ajali mbaya zimetokea kama madereva walijaribu kutazama kwa msaada wa kiberiti kama tangi imejaa. Ajali mbaya zaidi hutokea mara kwa mara wakati lori la kubebea petroli limpatwa na ajali na watu wanaenda kuchota petroli kwa ndoo.
  • petroli ina kemikali ndani yake zinazisababisha kansa kwa hiyo hatari ni kubwa kama inamwagika na kuingia katika maji ndani ya ardhi na kutoka hapa katika kisima; vilevile ni hatari ya afya kwa watu wanaoshughulika petroli mara kwa mara na kuvuta mvuke wake ndani ya mapafu. Pia moshi yake ni hatari kama inachomeka hovyo wakati wa ajali.
  • moto ya petroli haiwezi kuzimika kwa maji kama kila moto ya mafuta. Ni afadhali kutumia mchanga, kufunika moto isiyo kubwa sana kwa blenketi au fadhali kutumia kizima moto ya pofu.
  • hata gesi zinazotoka kwenye eksosi ya motokaa zina hasara za kiafya kwa sababu hiyo serikali nyingi zinaongeza masharti kwa motokaa kupunguza matumizi ya petroli kwa mbio wake na pia kudai filta kwenye eksosi.

Marejeo

  1. http://www.geoexpro.com/articles/2013/12/east-africa-riding-high