Angahewa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Tabaka za angahewa ya dunia

Angahewa ni ganda la gesi za hewa zinazozingira dunia yetu zikishikwa na nguvu mvutano yake. Angahewa inakinga uhai duniani kwa kupunguza mnururisho wa urujianimno wa jua, kutunza halijota duniani kwa kuakisisha mawimbi infraredi, kupunguza tofauti kati ya baridi na joto na kuwapa wanyama na mimea viwango vya oksijeni na nitrojeni wanayohitaji.

Magimba ya angani mengine kama sayari au jua huwa pia na aina za angahewa ingawa gesi zake ni tofauti na duniani.

Gesi zilizopa katika angahewa ya dunia ni hasa nitrojeni (78 %) na oksijeni (21 %) pamoja na viwango vidogo lakini muhimu vya arigoni (0.9 %), kaboni dioksidi (0.035 %), mvuke wa maji na gesi mbalimbali.

Angahewa haina mwisho kamili inazidi kuwa hafifu jinsi inavyofikia juu. Asilimia 75 ya masi ya hewa yake iko katika tabakatropo hadi kilomita 11 juu ya uso wa dunia. Uzito wa hewa hupimwa kama mkandamizo hewa.

Halijoto na tabaka za angahewa[hariri | hariri chanzo]

Sehemu za angahewa zina baridi au joto zaidi kutegemeana na kimo. Tukipaa juu ya uso wa dunia halijoto inazidi kuwa baridi, baadaye joto tena, kadiri jinsi tunavyopaa. Mabadiliko ya halijoto yanafuata muundo wa tabaka zinazootofautishwa na kiwango cha joto au baridi kinachopimwa.

Kwa jumla inawezekana kutofautisha tabaka 5 ambazo ni

  • Tabakatropo (troposphere) - inaanza kwenye uso wa dunia na kuishia mnamo kilomita 7 (juu ya ncha za dunia) - 15 (juu ya sehemu za tropiki) juu yake; baridi inazidi jinsi unavyopaa juu (kwa hiyo ni baridi mlimani kushinda chini); mawingu yako hapa na hii ni tabaka ambako halihewa inatokea.
  • Tabakastrato (stratosphere) - inaishia kwenyi kimo cha 50 km; hapa joto linaanza kuzidi tena. Eropleni kubwa zinapita hapa kwa sababu hakuna upepo mwenye nguvu inayosumbua mwendo
  • Tabakakati (mesosphere) - inaishia kwa kimo cha 80 - 85 km; hapa baridi inazidi jinsi unavyopaa; kuna upepo mkali.
  • Tabakajoto (thermosphere) - inaishia kwa kimo cha 500 - 600 km; joto linapanda pamoja kimo; tabaka hii ni muhimu kwa mawasiliano ya redio kwa sababu inaakisisha miale ya redio ya AM.
  • Tabakanje (exosphere) - ni tabaka la nje inayoanza kati ya 500- 1000 km na kuwa hafifu kadri unayopaa juu zaidi; inafikia kilomita maelfu hadi kwa kimo cha takriban 10,000 km ambako hewa haipimiki tena

Tabaka za juu yaani tabakajoto na tabakanje huitwa pia tabakaioni kwa sababu atomi za gesi zake zinapatikana katika hali ya ioni zilizopoteza elektroni kutokana na kupigwa na miale ya jua iliyo bado kali sana hapo nje.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]