Mwezi (gimba la angani)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Miezi)
Jump to navigation Jump to search
Chombo cha angani Galileo ilipiga picha hii ya Ardhi na mwezi
Picha maarufu sana ya dunia yetu iliyopigwa na mwanaanga Mmarekani Bill Anders wakati wa ujumbe wa Apollo 8 tarehe 24 Desemba 1968. Apollo 8 ilikuwa mara ya kwanza chombo cha angani cha kubebea watu kushikwa na graviti ya mwezi na kuzunguka mwezi kwa ajili ya graviti hiyo.

Mwezi ni gimba la angani linalozunguka sayari fulani. Kuna miezi mingi katika anga la nje, lakini maarufu zaidi kwetu ni ule pekee unaozunguka dunia yetu.

Mabadiliko ya kuonekana kwake yalisababisha katika Kiswahili neno "mwezi" litumike kama kipindi cha wakati. Awamu zake nne pengine ndizo chanzo cha majuma ya siku sabasaba.

Miezi ya sayari[hariri | hariri chanzo]

Sayari inaweza kukosa mwezi au kuwa na miezi mingi. Mshtarii ina miezi zaidi ya 60, mingine mikubwa kama sayari ndogo, mingine midogo yenye kipenyo cha km 1 tu. Dunia yetu ina mwezi mmoja tu. [Utaridi]] haina mwezi.

Mwezi hauna nuru ya kwake wenyewe bali unang'aa kutokana na nuru ya jua inaoakisiwa usoni mwake kama kwenye kioo.

Sayari yenye miezi katika mfumo wa jua:

Sayari zisizo na miezi katika mfumo wa jua:

Awamu za mwezi katika kipindi cha mwezi wa kalenda

Mwezi wa Dunia yetu[hariri | hariri chanzo]

Mwezi wa dunia yetu ni kati ya miezi mikubwa kwenye mfumo wa Jua. Hakuna jina tofauti kuliko "mwezi" isipokuwa watu wametumia pia jina la Kilatini "Luna" wakitaja mwezi wetu ili kuutofautisha na miezi ya sayari nyingine.

Mwezi wetu huwa na umbo la tufe lakini si tufe kamili. Kipenyo cha wastani ni kilomita 3,476 (dunia yetu ina kipenyo cha km 12,756 kwenye ikweta). Mwezi unazunguka dunia yetu kwenye obiti (njia yake) chenye umbo la duaradufu kwa umbali baina ya kilomita 363,300 hadi 405,500 kutoka dunia. Pamoja na dunia unazunguka jua.

Huwa tunaangalia uso wake upande mmoja, tena uleule tu. Sababu yake ni ya kwamba mzunguko wa Mwezi kwenye mhimili wake ni sawa na kipindi cha obiti ya kuzungka Dunia mara moja. Kipindi cha obiti yake ni siku 27 , masaa 7, dakika 43 na sekunde 11.5. Upande wa nyuma wa mwezi uko gizani wakati sisi tunaona mwezi mpevu. Wakati wa mwezi mwandamo kwetu upande wa nyuma unapokea nuru ya Jua. .

Nuru ya mwezi hautoki kwake bali ni nuru ya jua inayoakisiwa na uso wake.

Uso wa mwezi unajaa mashimo ya kasoko yaliyosababishwa kwa kugongwa na meteoridi. Mwezi hauna angahewa inayozuia mapigo ya meteoridi ndogo au kupunguzu nguvu yao jinsi ilivyo duniani.

Picha inayoonyesha umbali baina ya dunia na mwezi kulingana na ukubwa wake. Umbali wa wastani baina ya mwezi na dunia ni kilomita 384,400. Kipenyo cha mwezi ni takriban robo moja ya kipenyo cha dunia. [1].

Mwezi kama kipimo cha wakati[hariri | hariri chanzo]

Awamu za mwezi kuanzia mwezi mwandamo (1) kupitia hilali (2), robo ya kwanza, nusu mwezi, robo ya tatu, mwezi mpevu (5) hadi mwezi mwandamo tena

Uso wa mwezi jinsi unavyoonekana duniani hubadilikabadilika. Mwezi mpevu unaonekana kama duara kamili la kung'aa lakini baada ya kuonekana hivi umbo lapungua kila siku hadi kutoonekana kabisa na hali hii huitwa mwezi mwandamo. Baadaye mwezi unaonekana tena kama hilali nyembamba na kuongezeka hadi kuwa duara tena. Muda wa mabadiliko yote kupita mara 1 ni siku 29 1/4.

Muda wa mabadiliko kati ya mwezi mwandamo hadi kupotea na kuwa mwezi mwandamo tena ni kati ya siku 28 - 29. Kipindi hiki kinakumbukwa kirahisi, kinatazamiwa na watu wote wakati uleule kwa hiyo pamoja na kipindi cha siku kilikuwa kati ya vipimo vya kwanza vya wakati kwa binadamu.

Inawezekana kwamba juma la siku saba lilianza kwa kuzingatia robo 4 za mwezi wa siku 28.

Awamu za mwezi zilikuwa vipindi vya kuhesabu wakati tangu mwanzo wa kalenda. Hadi leo kuna kalenda ya mwezi ndiyo kalenda ya Kiislamu inayopanga wakati kutokana na hali halisi ya awamu za mwezi.

Safari kwenda mwezini[hariri | hariri chanzo]

Nyayo za mwanaanga Edwin Aldrin (Apollo 11) mwezini.

Mwezi wetu ni gimba la angani la kwanza ambako wanadamu wamefika. Tarehe 21 Julai 1969 mwanaanga Mmarekani Neil Armstrong alikuwa mtu wa kwanza wa kukanyaga uso wa mwezi. Wamarekani 11 walimfuata hadi mwaka 1972. Baadaye safari za kwenda mwezini hazikufanywa tena kutokana na gharama kubwa.

Mwezi mali ya watu?[hariri | hariri chanzo]

Hata kama Warusi na Wamarekani walifikisha bendera zao mwezini, hakuna anayedai mali huko. Katika mkataba wa kimataifa kuhusu anga wa nje nchi 192 za dunia zimepatana ya kwamba mwezi utaangaliwa sawa na maeneo ya kimataifa ya bahari. Walipatana pia ya kwamba itakuwa marufuku kupeleka silaha kali kama za nyuklia angani. Mataifa mengi ya dunia yamejiunga na mkataba huo, isipokuwa nchi chache hasa za Afrika hazikutia sahihi kama vile Tanzania.

Lakini kuna watu binafsi wanaodai mali ya mwezi.

Kwanza kuna familia ya Jürgens wanaoishi Westerkappeln (Ujerumani) walipewa hati ya kumiliki mwezi na mfalme wa Prussia Friederich II tarehe 15 Julai 1756 BK. Mfalme alitoa hati kama zawadi ya shukrani kwa huduma bora akiamuru ya kwamba Martin Jürgens atakuwa mwenye mwezi na haki hii itarithiwa na mtoto wa kwanza.

Bila shaka ilhali hakujua haki za mali za Mjerumani katika mwaka 1980 Mwamerika Dennis M. Hope alifika mbele ya msajili wa viwanda mjini San Francisco akidai mwezi ni wake. Kufuatana na sheria ya Marekani kiwanda ni mali ya mtu akiandikisha dai lake na katika muda wa miaka minane hakuna upingamizi dhidi ya dai lake. Kwa njia hii - iliyowahi kufaulu tayari karne zilizopita Wazungu walipojipatia Amerika ya Kaskazini (hakuna aliyepinga madai yao mbele ya msajili) - alipata hati ya kumiliki akijaribu kuuza sasa mwezi polepole.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

  1. ["http://solarsystem.nasa.gov/planets/profile.cfm?Object=Moon" "NASA Solar System Exploration: Planets"]. NASA. Iliwekwa mnamo 2010-10-01.
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mwezi (gimba la angani) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.