Nenda kwa yaliyomo

Mzungu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Wazungu)
Wote Watu wa Ulaya lakini si wazungu! (Waingereza wazawa mbunge Diane Abbott, mwigizaji wa filamu Adewale Akinnuoye-Agbaje, waziri Paul Boateng, modeli Naomi Campbell, mwimbaji Craig David)

Mzungu ni neno la Kiswahili kumtaja mtu anayeonekana ametoka Ulaya.

Neno la kumaanisha rangi ya mtu[hariri | hariri chanzo]

Ni neno ambalo zaidi linalenga rangi ya mtu na kumtofautisha yule anayetajwa na Mwafrika, Mwarabu, Mhindi au Mchina.

Si neno kamili sana kwa sababu watu wanaoitwa Wazungu wanaweza kutokea kila sehemu ya dunia; Wamarekani weupe huitwa Wazungu na pia makaburu kutoka Afrika Kusini, Wakenya weupe na pia Waaustralia. Vilevile mtu kutoka nchi za Ulaya ya Kusini kama Hispania au Ugiriki anaweza kusababisha wasiwasi kama yeye ni Mzungu au Mwarabu kwa sababu wengi wao hufanana na watu wa Afrika ya Kaskazini.

Ikitumiwa kwa maana ya "watu wa Ulaya" inaeleweka kwa jumla isipokuwa siku hizi nchi za Ulaya hujaa watu ambao wenyewe au mababu wao walihamia huko kutoka pande nyingi za dunia jinsi inavyoonekana kwenye nyuso yao.

Neno la kutaja sifa ya mbari pamoja na jiografia[hariri | hariri chanzo]

Kiasili neno lilijitokeza wakati ambako watu waliweza kuamini ya kwamba kila sehemu ya dunia ilikuwa na rangi yake. Kwa namna hiyo inafanana na maneno katika lugha nyingine kwa mfano "negroe/negre/Neger" katika lugha za Ulaya kwa watu wanaoonekana kama wenye asili ya Kiafrika. Haina dharau ndani yake kama neno la Kiarabu "abdi" linalotaja watu weusi pamoja na watumwa.

Kizungu kwa lugha[hariri | hariri chanzo]

Neno "Kizungu" latumiwa mara nyingi kwa maana ya lugha ya Kiingereza, lakini wakati wa ukoloni wa Ujerumani katika Tanzania bara ("Afrika ya Mashariki ya Kijerumani") lilitaja pia Kijerumani[1].

Asili ya neno[hariri | hariri chanzo]

Asili ya neno haijulikani kikamilifu.

Inaonekana kuna uhusiano na neno mzungu / mizungu lisilo kawaida tena katika Kiswahili cha kisasa lakini limetunzwa katika kamusi za Kiswahili zilizokusanya maneno yake mnamo mwaka 1900. Lilimaanisha mambo mbalimbali kama vile: 1) kitu cha ajabu au cha kushangaza, 2) mbinu ya kujiondoa katika tatizo, 3) aina ya muhogo, 4) silika au akili ya wanyama.[2]

Waswahili waliwahi kutumia neno "mzungu" kwa "akili" na pia kwa mafundisho ya "unyago" yaliyoitwa "kufundishwa mizungu".[3]. Kama asili ya "Wazungu" iko hapa iliweza kumaanisha "watu wa ajabu, wasio kawaida, wenye mbinu nyingi" au "wageni walio tofauti sana".

Wengine wamehisi kwa utani ya kwamba kuna uhusiano na kitenzi "kuzunguka" na "mzungu" ilitaka kutaja tabia ya wapelelezi, wamisionari na wafanyabiashara wa kwanza kutoka Ulaya ambao hawakukaa mahali pamoja bali walizungukazunguka kote Afrika.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. kamusi ya Carl Velten, Suaheli Wörterbuch, Suaheli-Deutsch, Berlin 1910, Mzungu I: "neno la kizungu - europäischer (deutscher) Ausdruck"
  2. kamusi ya M-J SSE "Mzungu (B)"
  3. kamusi ya Carl Velten, Suaheli Wörterbuch, Suaheli-Deutsch, Berlin 1910, Mzungu II