Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Bendera ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Nembo ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mwanzo wa utawala wa kikoloni 1885
Makao ya serikali ya kikoloni Bagamoyo hadi 1891 halafu Daressalam
Eneo 995.000 km²
Wakazi 7.700.000 (1913)
Wakazi Wajerumani 4100 (1913)
Pesa 1 Rupie= 64 Pesa,
kuanzia 1904
1 Rupie = 100 Heller
Nchi huru za leo 1961 Tanganyika, tangu 1964 Tanzania

Ruanda
Burundi

Ramani ya Kijerumani ionyeshayo Zanzibar na pwani (mnamo 1888)

Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (au: ya Kidachi) ilikuwa jina la koloni ya Ujerumani huko Afrika ya Mashariki kati ya 1885 hadi 1918/1919.

Eneo lake lilijumlisha nchi za kisasa za Tanzania bara (bila Zanzibar), Burundi na Rwanda. Ilikuwa koloni kubwa kabisa ya Dola la Ujerumani.

Chanzo cha koloni[hariri | hariri chanzo]

Utangulizi[hariri | hariri chanzo]

Hadi mnamo mwaka 1880 serikali ya Ujerumani chini ya chansella Otto von Bismarck ilikataa kuanzishwa kwa koloni. Sehemu ya wafanyabiashara Wajerumani walidai koloni. Walisikitika faida za wenzao Waingereza waliopata mara nyingi msaada kutoka kwa wanajeshi na serikali za koloni za Uingereza hasa Asia. Waliona pia faida ya viwanda vya Uingereza vilivyokuwa na soko la kulindwa katika nchi kama Uhindi kwa sababu serrikaliy a kikoloni ilidai kodi kali kwa bidhaa zisizotoka Uingereza.

Bismarck hakuamini ya kwamba koloni ingeleta faida kwa taifa kulingana na gharama kubwa kwa serikali. Lakini wapigania koloni walikuwa na wabunge waliokuwa muhimu kwa serikali na polepole Bismarck alianza kukubali hatua za kwanza. Mwenyewe aliamini mwanzoni ya kwamba itatosha kuwapa wafanyabiashara ulinzi kwa shughuli zao kwa kuwaruhusu matumizi ya bendera ya Ujerumani na kuwa na askari wao wa ulinzi kama wamepatana na viongozi wazalendo katika eneo fulani kuanzisha shughuli huko. Kwa njia hii alifungua mlango kwa harakati iliyoendelea kuwa mchango wa Ujerumani katika mbio wa kugawa dunia hasa Afrika.

Juhudi za Karl Peters[hariri | hariri chanzo]

Maeneo ya kwanza yaliyotwaliwa na Karl Peters

Koloni hii ilianzishwa na mfanyabiashara Mjerumani Karl Peters mwaka 1885 kwa niaba ya "Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki".

Peters aliyewahi kusoma chuo Uingereza aliona wivu juu ya ukoloni wa Uingereza akiamini ya kwamba Ujerumani ungestahili nafasi hiyo pia. Hivyo alianza kudai koloni katika mikutanno akaanzisha "Shirika kwa koloni za Kijerumani" mwaka 1884 iliyokuwa kitangulizi cha kampuni. Shirika hii ilimtuma pamoja na wenzake wawili kwenda Afrika na kutafuta nafasi ya kuanzisha koloni. Peters alifika Zanzibar alipoambiwa na konsuli ya Ujerumani ya kwamba hawezi serikali ya nyumbani haikubali mipango yake. Hivyo alivuka barani akapita kanda la neo la Kizanzibari kwnye pwani na kutembelea machifu na masultani barani.

Hapa alifaulu kushawishi watawala wa Usagara, Nguru, Useguha und Ukami kumpa sahihi kwenye mikataba ya Kijerumani ambayo hawakuelewa. Mikataba hii ilisema ya kwamba mtawala alikabidhi nchi yake pamoja na haki juu ya ardhi na mali yote kwa kampuni.

1885 Peters alirudi Berlin na kuonyesha mikataba yake kwa magazeti na serikali. Chansela Bismarck alikataa akacheka mikataba kama karatasi bila maana. Peters alitumia mbinu akatisha kupeleka mikataba yake kwa mfalme Leopold II wa Ubelgiji aliyekuwa kununua haki zake. Hapa Bismarck aliogopa kilio cha wapenda koloni akakubali kumpa Peters barua ya ulinzi kwa maeneo yalikuwa ya kampuni kufuatana na mikataba.

Upanuzi wa eneo la kampuni[hariri | hariri chanzo]

Upanuzi na ugomvi na Zanzibar[hariri | hariri chanzo]

Peters na wawakilishi wake walirudi wakaendelea kutafuta machifu waliokuwa tayari kutia saini mikataba yake. Sultani ya Zanzibari alipinga juhudi hizi. Zanzibar ilisimamia pwani la Afrika ya Mashariki na tangu karne watu wa miji ya pwani walikuwa na mawali wa Sultani. Zanzibar ilidai pia utawala ya bara hadi Ziwa Tanganyika na Kongo ingawa hali halisi athira yake haikuenda mbali na njia za misafara ambako ndovu na watumwa walipelekwa pwani. Tarehe 27 Aprili 1885 serikali ya Zanzibar ilituma barua Berlin kupinga kazi na madai ya kampuni na kutangaza maeneo ya ya tanzania ya leo kama milki yake. Iliongeza pia wanajeshi wake barani zilizokuwa chini ya amri ya mwanajeshi mstaafu Mwingereza Matthews. Hapa serikali ya Berlin ilituma kikosi cha manowari kwenda Bahari Hindi.

Mwezi wa Agosti manowari za Kijerumani chini ya amri ya admirali Eduard von Knorr zilifika mbele ya Unguja zikalenga mizinga yao kwa ikulu ya sultani. Akishauriwa na balozi wa Uingereza Sultan Bargadh alipaswa kutoa tamko kuwa "Kutokana na madai tunayopelekewa kwa matishio na Kaisari wa Ujerumani tunatambua ulinzi wa Ujerumani juu ya nchi za Usagara, Ngurow, Useguha, Ukami na juu ya wilaya ya Witu. Mipaka yake itaelezwa baadaye na sisi tunatambua ulinzi wa Kaisari juu ya mahali palipotajwa." [1]. Sultani alipaswa pia kutia sahihi mkataba wa biashara na Ujerumani alipokubali haki nyingi kwa Wajerumani katika milki yake. [2].

Mwaka 1886 Uingereza na Ujerumani walipatana juu ya ugawaji wa Afrika ya Mashariki na tena Sultani alipaswa kukubali. Katika mapatano haya Sultani alibaki na visiwa vya Unguja, Pemba, Mafia na funguvisiwa ya Lamu pamoja na kanda la pwani barani lenye upana wa maili 10 kati ya mito Rovuma upande wa Kusini na mto Tana upande wa Kaskazini,halafumiji ya Kismayu, Barawa, Merka na Mogadishu upande wa kaskazini zaidi. [3].

Mkataba kati ya Zanzibar na Kampuni juu ya kofo na pwani[hariri | hariri chanzo]

Mapatano ya 1886 yaliwapa Wajerumani nafasi ya kuendeleza upanuzi barani nyuma ya kanda la pwani la Kizanzibari na mstari wa mpaka ulichorwa kuanzia mdomo wa mto Umba kupitia mlima Kilimanjaro hadi Ziwa Viktoria. Lakini kwa ajili ya matumizi ya kibiashara swali la mabandari bado lilibaki wazi. Hapo Peters na kampuni yake walianza kujadiliana na Sultani Seyyed Bargash kuhusu utawala wa pwani katika sehemu ya Tanganyika.

Mnamo mwaka 1887 Bargash alikuwa amechoka alitafuta pesa tu kwa ajili yake binafsi alikuwa tayari kukodisha utawala wa kanda la pwani la Tanganyika kwa Wajerumani. Wajerumani walidai kuongezeka haki na Bargash alikufa bila kumaliza mapatano. Lakini mfuasi wake Sultani Seyyed Khalifa aliwapa Wajerumani walichotaka. Tarehe 15 Agosti 1888 wawakilishi wa kampuni ya Kijerumani walifika kwenye mabadari yote ya pwani wakatangaza utawala wao kwa niaba ya sultani.

Vita ya Abushiri na mwisho wa utawala wa Kampuni[hariri | hariri chanzo]

tazama Vita ya Abushiri

Badiliko hili lilisababisha upinzani na hatimaye ghasia ya wenyeji. Vipengele ya mkataba vilisema ya kwamba mali isiyokuwa na hati za kimaandishi haiwezi kutambuliwa. Wenye mali kama mashamba walitakiwa kununua hati kutoka kwa watawala wapya. Hapo Waswahili wa pwani walijisikia walisalitiwa na sultani asiyekuwa na haki kuchukua mali zao na kuzipa kwa wageni wa nje.

Mara baada ya kufika kwa Wajerumani kwenye miji ya pwani ghasia ilianza mjini Pangani na kuenea haraka kote pwani kati ya Tanga na Lindi.

Kampuni ilikuwa na Wajerumani wachache tu walioshindwa kujitetea. Walipaswa kukimbia au wakauawa. Bagamoyo pekee palikuwa na kikosi cha askari kzutoka manowari ikatetewa.

Serikali ya Ujerumani iliona lazima kuingia kati ya kutuma manowari pamoja na askari waliokandamiza ghasia.

Baada ya upinzani wa wenyeji wa pwani mwaka 1889/1890 wakiongozwa na Abushiri na Bwana Heri serikali ya Ujerumani iliamua kutwaa mamlaka kutoka kwa kampuni na kufanya eneo lote kuwa koloni ya Dola la Ujerumani badala ya shirika.


Koloni ya Dola la Ujerumani[hariri | hariri chanzo]

Utawala wa Kijerumani ulikwisha katika Vita Kuu ya Dunia ya Kwanza (1914 - 1918) kutokana na uvamizi wa Uingereza na Ubelgiji.

Katika Mkataba wa Versailles mwaka 1919 eneo la koloni ya Kijerumani iligawiwa. Sehemu ya Tanganyika ilikabidhiwa kwa Uingereza na maeneo ya Rwanda na Burundi yaliwekwa chini ya Ubelgiji.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. nukuu ya Kiingereza katika Franz Kotrba: William Astor Chanler (1867-1934) und Ludwig von Höhnel (1857-1942) und Afrika, Vienna 2008
  2. Mkataba inapatikana kwa Kiingereza na Kijerumani kwa wikisource
  3. Februari 1887 Sultani aliendelea kupungukiwa maeneo alipopatana na Mwingereza William Mackinnon kumkodisha pwani la Kenya pamoja na haki za utawala kwa malipo ya kila mwaka. Kisheria kanda hili lilibaki mali ya Zanzibar hadi uhuru wa Kenya 1964

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1
Hourglass.svg Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.