Nenda kwa yaliyomo

Mkoa wa Tanga (DOA)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkoa wa kihistoria wa Tanga (DOA) mnamo 1913 (na. II)
Mtaa wa Kaizari (Kaiserstraße) mjini Tanga wakati wa DOA

Mkoa wa Tanga ilikuwa mkoa mmoja kati ya mikoa 21 ya koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (DOA, Deutsch Ostafrika) iliyokuwa mtangulizi wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wa leo.

Eneo na mipaka

[hariri | hariri chanzo]

Mkoa huu ulikuwa na eneo la kilomita za mraba 4,600 kwa hiyo ilikuwa kati ya mikoa midogo zaidi ya koloni hii. Makao makuu (jer. Bezirksamt) yalikuwepo Tanga mjini.

Mkoa huu ulipakana na

Kwenye mpaka na Afrika ya Mashariki ya Kiingereza kulikuwa na kituo cha forodha huko Yasini.

Mwaka 1913 kulikuwa na wakazi wazalendo 108,400, pamoja na 2,393 Waasia (Wahindi, Waarabu hasa) na Wazungu 581.

Mji wa Tanga ulikuwa na wakazi 12,000, kati yao Wazungu 298.D

Mkoa wa Tanga wa DOA ulikuwa kitovu cha uchumi ya mashamba ya kibiashara. Sababu ya kuenea mapema zilikuwa kwanza bandari ya Tanga na pili njia ya reli ya kuelekea Kilimanjaro. Kutokana na miundombinu hii ilikuwa rahisi zaidi kusafirisha mazao na bidhaa nje. Kabla ya 1914 yalikuwepo makampuni 24 ya kizungu na walowezi 72 walioendesha mashamba ya kibiashara, hasa ya mikonge. Mashamba haya ya kizungu yalikuwa na eneo la km² 877. Wazungu hao walifuga ng'ombe 259, kondoo na mbuzi 239, nguruwe 12, punda 124 na farasi 29. Wajerumani walihesabu mifugo ya wakazi wazalendo kuwa ng'ombe 2,400, kondoo 13,490, mbuzi 27,300, punda 112 na nguruwe 20.

Mji na bandari ya Tanga

[hariri | hariri chanzo]

Tanga yenyewe iliwahi kuwa mji muhimu wa Waswahili kabla ya ukoloni. Tofauti na miji mingine ya Waswahili bandari ya Tanga ilifaa pia kwa meli kubwa hivyo mji ulianza kupanuka haraka. Tangu mwaka 1893 njia ya reli kwenda milima ya Usambara ilianzishwa iliyoendelea baadaye hadi Moshi. Idadi ya wakazi ilifikia 5,689 (kati hao Wazungu 141) mwaka 1908 ikaongezeka hadi 1913 kuwa wakazi 12,000. Mwaka 1913 kulikuwa na makampuni ya biashara 12 na makampuni mengine ya Kizungu 26, ya Kihindi 50. Tanga ilikuwa na hoteli 4, hospitali, duka la dawa, gazeti na ofisi mbalimbali za serikali.

Meli 286 zilifika bandarini mwaka 1912, pamoja na jahazi 384. Thamani ya bidhaa zilizoingizwa ilikuwa mark milioni 11.994, hapa nafaka zilikuwa milioni 2, vyakula vingine mio 1.2, nguo mio 2,57 , bidhaa za metali mio 3.25.

Bidhaa zilizotoka zilikuwa na thamani ya mark milioni 13.327, hapo kahawa (kutoka milima ya Usambara hasa) mio 1.16, katani mio 4.67, bidhaa za msituni (hasa mpira) mio 6.5.