Nenda kwa yaliyomo

Wazigula

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Useguha)

Wazigula (au Wazigua) ni kabila la watu kutoka eneo karibu na Bahari Hindi baina ya Dar es Salaam na Tanga, nchini Tanzania. Baadhi ya kabila ya Wazigula wanapatikana kusini mwa Somalia.

Mwaka 1993 idadi ya Wazigula ilikadiriwa kuwa 355,000 [1].

Lugha yao ni Kizigula au Kinguu, ya jamii ya lugha za Kibantu.

Asili, mila na desturi

[hariri | hariri chanzo]

Wazigua ni mojawapo wa makabila ya asili ya mkoa wa Tanga. Wazigua yasemekana wamekuwepo mkoani Tanga, wilaya ya Handeni kwa karne nyingi zilizopita.

Wilaya ya Handeni iligawanywa kuwa na wilaya mbili ambazo ni Handeni yenye makao yake makuu mjini Handeni au Chanika, na wilaya ya Kilindi yenye makao yake katika mji wa Songe. Wilaya ya Kilindi ina aina ya Wazigua wanaojulikana kama Wanguu ambao hutofautiana kwa namna wanavyotamka baadhi ya maneno. Kwa mfano Wazigua wanatumia "Chi-" (Chi-te chi-kamzungule, chi-nambwila che-za nae) wakati Wanguu wanatumia 'Ki-" (Ki-te ki-kamzungule, ki-nambwila che-za nae) kwenye baadhi ya maneno. Maana ya sentensi hiyo ni "twende tukamtafute, tukimkuta tuje naye". Wazigua wengi wapo maeneo ya Handeni mjini kuelekea mashariki Segera, kabuku, Mkata, Kwamsisi. Wanguu wapo magharibu kuelekea njia za Kiteto, Turiani na Gairo.

Wazigua ni miongoni mwa watu wenye asili katika kabila kubwa lililojulikana kwa jina la Waseuta. Baada ya hao kupigana na Wareno na kuwashinda katika vita vikali vilivyojulikana kwa jina la "Nkondo ya kutula nyala" (Vita vya kuvunja mawe ya chakula), Waseuta walianza kugawanyika kwa kujimega makundimakundi na kuondoka. Makundi hayo ndiyo makabila yenye asili ya mkoa wa Tanga kwa sasa, isipokuwa Wadigo si miongoni mwa Waseuta. Baada ya Waseuta kusambaa milimani na kuitwa Wasambaa na wengine kurudi na kuishia mabondeni huko wakaitwa Wabondei Waseuta waliobaki Handeni waliyachukua maeneo yaliyoachwa na wenzao; hapo kundi hili likaitwa Wazigua kwa kuwa maana ya Zigua ni kuchukua au kukamata eneo. Ndicho chanzo cha majina ya makabila hayo, kwani kabla ya hapo walikuwa wakiishi pamoja kama koo za jamii moja (Waseuta au Boshazi ikimaanisha Bondei, Shambaa, Zigula).

Unaweza kumtambua Mboshazi kwa jina lake; kwa mfano Mzigua Samamboe, Sakuzindwa, Sannenkondo, Sankanakono, Samboni, Shundi, Butu, Sebbo, Chamdoma n.k. Kuzungumza kwao huvuta maneno, mfano wa kusalimiana, Ahooni niheedi hanginyuwe n.k.

Msambaa utamtambua kwa jina lake, mfano Shekimweli, Sherukindo, Shekiondo, Shekazi, Shemndorwa n.k. Hawa wote ni Wasambaa na hutamka maneno yao ulimini, kwa mfano, tinakwenda, titarudi, titaonana kesho n.k.

Katika karne ya sayansi na teknolojia, kutokana na utandawazi, makabila mengi ya Kiafrika yamekumbwa na mabadiliko yasiyoepukika katika mila na desturi zao, hivyo, ili kutunza mambo haya yasije kusahaulika ni vyema kuweka kumbukumbu ya asili zetu. Tumetumbukia katika masuala ya utandawazi kiasi ambacho tunashindwa hata kutambua miiko yetu ili kuwarithisha watoto, wajukuu, vitukuu au vizazi vijavyo kwa ujumla.

Mila ya kukeketa wanawake imekuwa ikipigwa marufuku na serikali mbalimbali za ulimwenguni kuwa ni kinyume cha haki za binadamu, hivyo basi kuna mila ambazo zinakomeshwa na serikali za nchi na nyingine zinapotea zenyewe taratibu, kutokana na kubadilika kwa hali ya maisha.

Katika kabila la Wazigua, kutoa majina kwa watoto wanaozaliwa huzingatia wakati, mahali, na mahusiano. Kila Mzigua lazima awe na jina la asili na la kidini, mfano Andrew Kizenga Shundi jina lake la asili anaitwa Chamdoma (dyauta netangwa Chamdoma, Dyamwale). Kiasili majina hutolewa wakati mtu anapozaliwa (Chamdoma), Dyamwale anapotoka kutahiriwa, kuchezewa ngoma na kukabidhiwa upinde, hivyo hupewa jina na kuwa kijana wa Kizigua aliyefikia utu uzima. Anapooa huitwa Samachau, na anaeolewa Wanamachau.

Idizina bya Ngasu netangwa Samachau ni jina apewalo mtu mzima aliyepata mchumba na kuoa. Wazigula hupewa jina litakalotumika wakati na baada ya ndoa, badala ya kuitwa Andrew hivi sasa naitwa Samachau na mke wangu anaitwa Wanamachau. Hivyo utaona kuwa “SA” inakwenda kwa mwanamume na “WA” inakwenda kwa mama wa watoto.

Kwa maana hiyo baada ya kumaliza tukio la kuoa na kumaliza deni la mahari na vihendo (zawadi au vitu vitolewavyo kutoka upande wa muoaji kwenda kwenye familia ya muolewaji) ulivyotakiwa kupeleka ukweni kwa mfano zawadi kama zogoro dya chunji, koti dya sachibwela, ngubula mlomo, kisingisa magutwi, kumwonelahi n.k.

Mila na desturi za Kizigua, kama zilivyo mila nyingine za Kiafrika zina miiko yake, kwa mfano, “Hachikungigwa kudya mbara unadya au unagonela umkota wa mbara wabambuka / Waholomoka mwili mjima”. Maana yake, Mzigua hatakiwi kula paa (mnyama).

“Kulagasama” ni tukio la kuagwa kwa waliooana mara baada ya kukamilisha mahari na taratibu zote za kimila. Katika mila za Kizigua, mtu anapofunga ndoa, yeye na mkewe hutakiwa kukaa katika familia ya mke wake huyo kwa muda fulani ili aweze kukamilisha mahari kama alikuwa hajamaliza. Hivyo kumaliza kulipa mahari na mambo mengine yanayohitajika, huomba ruhusa toka kwa wakwe zake ili akaanzishe maisha yake na mkewe.

Kama akishindwa kulipa ataendelea kuishi upande wa mkewe kwa maisha yake yote na hata kama akifariki atazikwa upande wa ukweni kama ukoo wa upande wa mume hautamlipia, ila kama wakimlipia watapewa mwili kuzika upande wa mume.

Wazigua wana ngoma nyingi za asili na huchezwa kutokana na wakati na tukio husika, mfano kuna ngoma za wakati wa mavuno, harusi, jando na msibani; hujulikana kwa majina ya Mkweso, Machindi, Tukulanga n.k.

Pia mtoto akishazaliwa hukaa ndani, na baada ya siku 40 hutolewa nje na kupewa jina la Lungo. Katika tukio hili la kumtoa mtoto nje, mtoto hupakwa unga na kunyolewa nywele zake za utotoni na bibi yake ambaye mara nyingi ni mama wa baba yake.

Vyakula vya asili vinavyopendelewa kuliwa na Wazigua ni ugali unaopikwa kutokana na unga wa mahindi yaliyokobolewa na kuvundikwa kwa muda mrefu kabla ya kusagwa au kutwangwa. Baada ya kusagwa hutoa unga mweupe na laini sana. Ugali huliwa na mboga za asili kama vile, Kungujulu, Sunga, Kididi, Mnavu, nyama za pori na uyoga.

Wazigua ni mojawapo wa makabila ya asili ya mkoa wa Tanga. Wazigua ambao lugha yao ni ya jamii ya lugha za kibantu yasemekana walikuwapo mkoani Tanga, wilaya ya Handeni kwa karne nyingi zilizopita hadi leo hii wameongezeka mara dufu kutokana na vizazi vyao kuzaliana siku hadi siku, mijini na vijijini kwa ujumla.[2]

Uhusiano na Wazulu

[hariri | hariri chanzo]

Katika hadithi za kale za Wazigua yasemekana kwamba hapo kale katika Uzigua, uliopo leo Tanzania, kulikuwa na familia ya wawindaji yenye watoto watatu: Zulu, dada yake na kaka yake. Katika harakati za uwindaji kaka yake Zulu aliuawa na nyati, hivyo Zulu alibaki na dada yake tu. Kulitokea ukame mkubwa, hivyo Zulu alikuwa akihamahama mpaka akafika eneo moja la Afrika ya Kusini na kuamua kukaa hapo na dada yake. Aliendeleza shughuli zake za uwindaji, hivyo wakinamama wa maeneo ya karibu walipokwenda kutafuta kuni porini ndipo walipokutana na mwindaji huyu hodari. Alikuwa akiwapa nyama alizowinda, hivyo akazoeleka na kuoa huko na kuanzisha familia yake na watu waliita eneo hilo Kwa Zulu. Kadiri ya hadithi hiyo, KwaZulu-Natal ya leo, asili yake ni Mzigua Zulu.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wazigula kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.