Wazigula

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Wazigula (au Wazigua) ni kabila la watu kutoka eneo karibu na Bahari Hindi baina ya Dar es Salaam na Tanga, nchini Tanzania. Baadhi ya kabila ya Wazigula wanapatikana kusini mwa Somalia,

Mwaka 1993 idadi ya Wazigula ilikadiriwa kuwa 355,000 [1].

Lugha yao ni Kizigula.

Asili, mila na desturi[hariri | hariri chanzo]

Wazigua ni mojawapo wa makabila ya asili ya mkoa wa Tanga. Wazigua ambao lugha yao ni ya jamii ya lugha za kibantu yasemekana wamekuwepo mkoani Tanga, wilaya ya Handeni kwa karne nyingi zilizopita.

Maana ya Zigua ni kuchukua au ukamata eneo. Miaka mingi iliyopita Wazigua walipigana vita na kuyashinda makabila ya Wabondei na Wasambaa. Makabila hayo yaliyoshindwa vita yalikimbiliia maeneo ya mabondeni na mengine kusambaa milimani, Wabondei huko Mabondeni, na Wasambaa walisambalia milima ya Usambara. Na ndio chanzo cha majina ya makabila haya, kwani kabla ya hapo walikuwa wakiishi pamoja kama koo za jamii moja. Na walijulikana kwa jina la Boshazi maana yake Bondei, Zigua, Sambaa.

Kumtambua m-Boshazi[hariri | hariri chanzo]

Unaweza kumtambua m-boshazi kwa jina lake kwa mfano mzigua Samamboe, Sakuzindwa, Sannenkondo, Sankanakono,Samboni, Shundi, Butu,Sebbo, Chamdoma nk. Kuzungumza kwao huvuta maneno, mfano wa kusalimiana, Ahooni niheedi hanginyuwe, nk.

Msambaa utamtambua kwa jina lake, mfano Shekimweli, Sherukindo, Shekiondo Shekazi, Shemndorwa, nk. Hawa wote ni wasambaa na hutamka maneno yao ulimini, mfano, tinakwenda, titarudi, titaonana kesho, nk.

Wilaya ya Handeni pia kuna makabila mbalimbali kama Wakilindi, Wanguu, na Wasambaa. Katika karne hii ya sayansi na tekinolojia, na kutokana na utandawazi, makabila mengi ya kiafrika yamekubwa na mabadiliko yasioepukika katika mila na desturi zao.

Mila ya kutahiri wanawake imekuwa ikipigwa marufuku na serikali mbalimbali za ulimwenguni kuwa ni kinyume cha haki za binaadamu, hivyo basi kuna mila ambazo zinakomeshwa na serikali za nchi na nyingine zinapotea zenyewe taratibu kutokana na kubadilika kwa hali ya maisha, hivyo ili kutunza mambo haya yasije kusahaulika vyema kuweka kumbukumbu ya asili zetu. Tumetumbukia katika masuala ya utandawazi kiasi ambacho tunashindwa hata kutambua miiko yetu au asili zetu, kwa kweli ni mambo ya kusikitisha sana si ajabu kwetu sisi wazee tutakapoondoka basi haya nayo yatapotea.

Mimi kama mzigua ningependa kuandika haya na kujaribu kukumbuka mambo ya kiasili ya “Kizigua” kwa yale ambayo nayafahamu na nisiyo yafahamu nitafurahi na kushukuru sana endapo nitakosolewa na kupewa mwelekezo wa kizigua nami niweze kuwarithisha watoto, wajukuu, vitukuu au vizazi vyangu kwa ujumla.

Katika kabila la Wazigua, kutoa majina kwa watoto wanaozaliwa huzingatia wakati, mahali, na mahusiano. Kila mzigua lazima awe na jina la asili na la kidini, mfano Andrew Kizenga Shundi jina lake la asili anaitwa Chamdoma (dyauta netangwa Chamdoma, Dyamwale), kiasili majina hutolewa wakati mtu anapozaliwa (Chamdoma), Dyamwale anapotoka kutahiriwa na kuchezewa ngoma na kukabidhiwa upinde, na hivyo hupewa jina na kuwa kijana wa kizigua aliyefikia utu uzima. Anapooa huitwa Samachau, na anaeolewa Wanamachau.

Idizina bya Ngasu netangwa Samachau ni jina apewalo mtu mzima aliepata mchumba na kuoa. Wazigula hupewa jina litakalo tumika wakati na baada ya ndoa, badala ya kuitwa Andrew hivi sasa naitwa Samachau na mke wangu anaitwa Wanamachau. Hivyo utaona yakuwa “SA” inakwenda kwa mwanaume na “WA” inakwenda kwa mama wa watoto.

Kwa maana hiyo baada ya kumaliza tukio la kuoa na kumaliza deni la mahali na vihendo (zawadi au vitu vitolewavyo kutoka upande wa muoaji kwenda kwenye familia ya muolewaji) ulivyotakiwa kupeleka ukweni kwa mfano zawadi kama zogoro dya chunji, koti dya sachibwela, ngubula mlomo, kisingisa magutwi, kumwonelahi, Nk.

Basi hayo mambo ya asili ya kizigua, ambayo kabila hili hujivunia. Wazee wa kizigua kama Marehemu Mzee Gerald Fredrik Kizenga Shundi ambaye ni mzaliwa wa Handeni (Mandela), alikuwa mtoto wa kwanza wa mzee Fedrik Kizenga Shundi na ni mmoja kati ya watoto 8 wa Mzee huyu alizaliwa na mama Teresa, huyu bibi asili yake ilikuwa Vugiri huko Kwa magome. Mzee huyu (Gerald) alikuwa akihimiza vijana kwa wazee kudumisha mila na desturi za kizigua katika uhai wake.

Kwahiyo miji ya asili ya Wazigua wa ukoo wa Shundi na chimbuko la Mzee Gerald Shundi ni Mandela ya Handeni na alikuwa ni wa MWEMNUN’GULI SAMNANDUGWA upande wa Baba yake, ni Chiva na Nunguli ni upande wa mama mwanae Andrew Kizenga Shundi, asili yake ni Pongwe ya KIDELEKO kama unakwenda Kwa Magome.

Mila na desturi za Kizigua kama zilivyo mila nyingine za kiafrika zina miiko yake kwa mfano, “HACHIKUNGIGWA KUDYA MBARA UNADYA AU UNAGONELA UMKOTA WA MBARA WABAMBUKA/ WAHOLOMOKA MWILI MJIMA” Maana yake Mzigua hatakiwi kula Paa (mnyama).

“KULAGASAMA” ni tukio la kuagwa kwa waliooana mara baada ya kukamilisha mahari na taratibu zote za kimila. Katika mila za Kizigua, mtu anapofunga ndoa, yeye na mkewe hutakiwa kukaa katika familia ya mke wake huyo kwa muda fulani ili aweze kukamilisha mahari kama alikuwa hajamaliza. Hivyo kumaliza kulipa mahari na mambo mengine yanayohitajika, huomba ruhusa toka kwa wakwe zake ili akaanzishe maisha yake na mkewe.

Na kama akishindwa kulipa ataendelea kuishi upande wa mkewe kwa maisha yake yote na hata kama akifariki atazikwa upande wa ukweni kama ukoo wa upande wa mume hautamlipia, kama wakimlipia watapewa mwili kuzika upande wa mume.

Wazigua wana ngoma nyingi za asili na huchezwa kutokana na wakati na tukio husika, mfano kuna ngoma za wakati mavuno, harusi, jando na msibani, hujulikana kwa majina ya Mkweso, Machindi, Tukulanga, nk.

Pia mtoto akishazaliwa hukaa ndani na baada ya siku 40 hutolewa nje na kupewa jila la Lungo. Katika tukio hili la kumtoa mtoto nje, mtoto hupakwa unga na kunyolewa nywele zake za utotoni na bibi yake na mtoto ambaye mara nyingi huwa ni mama wa baba yake na mtoto.

Vyakula vya asili vinavyopendelewa kuliwa na wazigua ni ugali unaopikwa kutokana na unga wa mahindi yaliyokobolewa na kuvundikwa kwa muda mrefu kabla ya kusagwa au kutwangwa. Baada ya kysagwa hutoa unga mweupe na laini sana. Ugali huliwa na mboga za asili kama vile, Kungujulu, Sunga, Kididi, Mnavu, nyama za pori na uyoga.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Flag of Tanzania.svg Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wazigula kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.